Habari za Punde

Zanzibar Inaunga Mkono Azma ya Bohari ya Dawa (MSD) Kujenga Kiwanda cha Dawa Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Mej. General Saali Mhidze, alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Mej.General Saali Mhidze alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono azma ya Bohari ya Dawa (MSD) ya kutaka kujenga kiwanda cha dawa hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Meja Jenerali Saali Mhidze Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba azma ya Bohari ya Dawa (MSD), ya kuja kuekeza viwanda vya dawa hapa Zanzibar itasaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika wakati huu wa janga la COVID 19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje sio mzuri.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na (MSD), za kutaka kuanzisha viwanda hapa Zanzibar ambazo zitapelekea kutotegemea sana dawa kutoka nje ya nchi hali ambayo athari yake imeweza kuonekana hasa katika kipindi hichi cha maradhi ya COVID 19 duniani.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo ya kuanzisha viwanda inaungwa mkono na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba tayari imeshatenga maeneo maalum ya viwanda na Serikali iko tayari kutoa ushirikiano wake.

Rais Dk. Mwinyi alieleza ipo haja ya kuonekana kwamba bidhaa zinazozalishwa  Zanzibar nazo ni sehemu za biashara kutoka Tanzania  na kuondoavikwazo vya kibiashara ambavyo  hapo siku za nyuma  vilikuwepo na kusababaisha biashara kati ya  sehemu mbili za Muungano kuwa ngumu.

Pia, alieleza azma ya Zanzibar ya kufanya bidhaa zozote zinazozalishwa hapa nchini kuagizwa nje ya nchi huku akieleza jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoiungana na Bohari ya Dawa(MSD)  ya kuanzisha viwanda vya ndani hapa hapa nchini.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Bohari ya Dawa(MSD), ili kuhakikisha azma yao hiyo inapatiwa ufumbuzi wa haraka hasa ikitambua kwamba ina uwezo na uzoefu mkubwa katika fani hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuwa na viwanda vya aina mbali mbali lakini soko lake ni dogo ikilinganishwa na soko la Tanzania Bara na soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza haja kwa Bohari ya Dawa(MSD) kueleza taratibu zinazohitajika ili kuondoa usumbufu kwa biadhaa zinazotoka Zanzibar.

Alisema  kuwa ni vyema Bohari ya Dawa(MSD), ikatoa maelekezo mazuri ili  kuepuka kufanyika uzalishaji  wa bidhaa kutoka Zanzibar na baadae kupata usumbufu wa soko la nje ya Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza haja ya (MSD) kuleta vijana ili kutoa utaalamu na mafunzo kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujifunza  juu ya mfumo wa ununuzi, uhifadhi, usambazaji dawa, vifaa na vifaa tiba.

Alisema kwamba iwapo Zanzibar itapata utaalamu kutoka (MSD) mafanikio zaidi yatapatikana katika mfumo mzima wa utoaji wa huduma hiyo hasa ikizingatiwa kwamba utaalamu huo kwa Zanzibar haujawa wa kuridhisha zaidi.

Mapema Meja Jenerali Saali Mhidze akitoa maelezo yake kwa Rais wa Zanzibar, alisema kuwa (MSD), inadhamiria kuja kuekeza Zanzibar kiwanda cha dawa ambacho kitakuwa kikubwa kwa Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na hata nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema kuwa dhamira ya (MSD), ya kuja kujenga kiwanda cha dawa hapa Zanzibar inatokana na mahitaji ya dawa pamoja na vifaa tiba vyenginevyo hapa nchini hasa katika wakati kama huu wa uwepo wa maradhi ya COVID 19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi ni mgumu.

Alieleza kuwa Bohari ya Dawa(MSD), imekuwa ikichukua hatua za makusudi za kuhakikisha inajenga viwanda kwa ajili ya utoaji wa vifaa hivyo na tayari kwa upande wa Tanzania Bara tayari wameshaanza ujenzi wa viwanda kama hivyo.

Alisema kuwa(MSD)  imekusudia kupanua upatikanaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini na tayari viwanda vinne vimeshakamilika kazi ambayo imeanza tokea mwezi wa kumi mwaka jana na kusema kwamba baada ya miezi mitatu uhaba wa dawa unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Aidha, alisema kuwa kuna haja kwa Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika suala zima la ujenzi wa viwanda vya dawa sanjari na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Meja Jenerali Mhidze alisisitiza kwamba hatua za ujenzi wa kiwanda  cha dawa hapa Zanzibar pia, kutasaidia kuleta ushirikiano wa uzalishaji wa dawa katika viwanda kati ya vile watakavyojenga Tanzania Bara na vile vya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Meja Jenerali Mhidze alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba kufanikiwa kwa azma yao hiyo ya ujenzi wa kiwadna cha dawa hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa hapa hapa nchini.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk. 


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.