Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip
Isdor Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali katika eneo la
ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko mara alipowasili kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa hospitali hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip
Isdor Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasanda wilaya ya Kakonko Mkoani
Kigoma akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa ziarani Mkoani Kigoma hii leo Julai 18, 2021 ametembelea wilaya ya Kakonko ili kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Akiwa kijijini Kasanda, Makamu wa Rais amepokea changamoto ya vijana waeneo hilo kushindwa kupata ajira katika mradi wa ujenzi wa barabara licha ya kwamba mradi huo unatekelezwa katika maeneo yao.
Makamu wa Rais amesema serikali ilikwisha kutoa muongozo kwa wakandarasi kuzingatia ajira kwa wazawa na kumuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi mhandisi Godfrey Kasekenya kulifuatilia suala hilo na kupata ufumbuzi.
Aidha Makamu wa Rais ameweka jiwe la msingi Hospitali ya wilaya ya Kakonko ilioanza kwa ujenzi wa majengo saba yanayogharimu shilingi Bilioni 1.8 na kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka 2021.
Makamu wa Rais ameagiza wizara ya fedha kurejesha kiasi cha fedha shilingi milioni 187.7 zilizochukuliwa na mfuko mkuu wa serikali wakati wa kufunga mwaka wa fedha 2019/2020 ili zitumike katika kukamilisha miundombinu mingine ya hospitali hiyo. Makamu wa Rais ameagiza fedha zinazoletwa katika mradi huo kuhakikisha zinatumika vizuri na thamani ya fedha ilingane na matokeo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uwekaji wa jiwe la msingi wa hospitali hiyo Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Kakonko kuendelea kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Amewahakikishia kwamba serikali ya awamu ya sita iataendelea kuboresha huduma za jamii katika wilaya hiyo na kutekeleza ahadi zilizoahidiwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment