Habari za Punde

Mhe Hemed aagiza kuchukuliwa kwa hatua kwa wote wanaofanya biashara holela ya tiba asilia

Washiriki wa Mkutano wa Tiba asili wakiskiliza hotuba ya Mgeni rasmi alioitoa katika Maadhimisho ya 19 ya siku ya tiba asili Barani Afrika katika Ukumbi wa Rahaleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwakumbusha wataalamu wa Tiba asili kuungana pamoja ili kutoa huduma bora kwa jamii wakati akihutubia katika Maadhimisho ya 19 ya siku ya tiba asili Barani Afrika katika Ukumbi wa Rahaleo.

 Mmoja ya washiriki wa maonesho ya tiba za asili akimpatia maelezo Mhe. Hemed wakati akiyakagua maonesho hayo mara baada ya kuwasili katika Ukumbi wa Rahaleo katika maadhimisho ya 19 ya siku ya tiba asili Barani Afrika


Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelitaka Baraza la tiba asili Zanzibar kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaofanya biashara holela za tiba hizo bila ya kusajiliwa.

Mhe. Hemed alitoa wito huo katika maadhimisho ya kumi na tisa ya siku ya tiba asili Barani Afrika yaliyofanyika katika Ukumbi wa Rahaleo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alifafanua kwamba sio jambo la kuridhisha kutokana na wimbi kubwa la waganga wasiosajiliwa kutoa huduma za tiba asilia katika misikiti, masoko pamoja na maeneo mengine ya wazi jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya za wananchi.

Katika hatua nyengine Mhe. Hemed aliwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuwa makini na kuachana na tabia ya kununua dawa kiholela, dawa ambazo hazijafanyiwa utafiti na kuthibitishwa na mamlaka husika.

Aliwataka wataalamu hao wa tiba asilia kuitumia vyema fursa waliyonayo katika jamii kwa kuacha kusababisha farka miongoni mwa jamii pamoja na kuepuka vitendo vya udhalilishaji kwa watu wanaofika kwao kupata tiba hizo.

Alisema kuwa kitendo cha kuitumia vibaya fursa waliyonayo ya kutoa huduma ya tiba asili kwa wananchi itasabisha kuharibu taswira nzima ya tasnia ya tiba asilia Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Nae Waziri wa Afya Usatwi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui alilitaka Baraza la tiba asili na tiba mbadala Zanzibar kuendelea kushirkiana na wizara anayoiongoa kwa lengo la kukuza tiba hiyo, hasa kuona namna bora ya kuanzisah maabara kwa ajili ya kuchunguza dawa asili ili dawa hizo ziwe na viwango sahihi kwa matumizi ya binadamu.

Alisema tiba asili zina mchango mkubwa katika kuisaidia Wizara ya Afya kwa kuwapatia tiba wananchi wa Zanzibar, hasa kwa kuwapatia wagonjwa huduma ya kwanza mara tu wanapopata tatizo la kiafya..

Akitoa salamu za Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) Wuwakilishi wa Shirika hilo Dk. Simon Verndelin alisema shirika hilo limefurahishwa na maamuzi ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungani wa Tanzania katika kupambana na Uviko 19 kwa kuwataka wataalamu wa tiba asilia kujumuika pamoja na wataalamu wengie, kwa lengo la kutoa ushauri wao katika kukabiliana na janga hilo.

Alisema Shirika la Afya Duniani kwa kutambua mchango wa tiba asili limendelea kuwaunga mkono wataalamu wa tiba hizo kwa kutoa kila aina ya msaada ikiwemo rasilimali fedha kwa ajili ya kufanikisha kazi za wataalamu hao Nchini.

 “Tumekuwa tukishirikiana na wataalamu wa Tiba asili kwa kuwawezesha katika kuwapatia rasilimali kwa ajili ya kuendesha tafiti mbali mbali” Alieleza Dk. Simon

Akisoma Risala Kaimu Mrajisi wa Baraza la Tiba asili Zanzibar Ndugu Muhamed Mshenga Matano, alieleza kuwa, Baraza limekuwa likiwafahamisha na kuwaelekeza zaidi waganga wa tiba asilia kujua namna bora zitakazoweza kuboresha huduma zao ili ziwe na viwango sahihi vya matumizi pamoja na kuendana na kasi ya kukuwa kwa teknolojia.   

Bw. Matano alisema Baraza limekuwa likifanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Waganga kwa kutumia njia ya kuendesha semina elekezi pamoja na mikutano mbali mbali lengo ikiwa kupata nguvu kazi ya pamoja katika kutoa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa, tangu Baraza hilo lianzishwe mwaka 2006 limekuwa likifanya ukaguzi na limefanikiwa kuwakagua waganga 624, maduka 156, pamoja na Kliniki mbali mbali.

Alisema pamoja na jitihada hizo walizozichukua lakini bado kumekuwa na muitiko mdogo kwa baadhi ya waganga kujitokeza na kusajiliwa na baraza hilo jambo linalopelekea waganga wengi kufanya kazi bila kufuata taratibu.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.