Habari za Punde

Wanufaika mradi wa Viungo waeleza mazuri ya mwaka mmoja

Bwana shamba kutoka wilaya ya kaskazini B Unguja Juma Kona Mossi akieleza ni kwa kiasi gani utekelezaji wa mradi wa Viungo katika kipindi cha mwaka mmoja umeweza kubadilisha maisha ya wanufaika wa mradi huo.
Meneja Mkuu utekelezaji wa mradi huo, Amina Ussi Khamisi alipokua akifungua mkutano huo wa siku mbili na ulilenga kusikiliza maoni ya wakulima wasaidizi na mabwana shamba kwa lengo la kububoresha zaidi shughuli za utekelezaji kwa mwaka wa pili.
Mkulima msaidizi Khadija Msonda kutoka shehia Mbaleni Kitope akieleza jinsi mradi wa viungo ulivyoweza kumbadilisha na kuwasaidia wengine katika jamii yake.
Washiriki 72 kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja wakifuatilia mkutano wa siku mbile katika ofisi za utekelezaji mradi huo Mwanakwerekwe mjini Unguja. 

Na Muhammed Khamis.

 

Wakati ikiwa imetimia mwaka mmoja wa utekelezaji mradi wa viungo visiwani Zanzibar imelezwa kuwa uwepo wa mradi huo umeleta tija kubwa na kubadilisha maisha  ya wanufaika kwa hatua ya awali.

 

Kauli hio imetolewa na baadhi ya washiriki wa mkutano wa siku mbili wenye lengo la kutazama fursa na changamoto za mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa utelezaji mradi huo.

 

Awali akichangia mada  katika mkutano huo Bwana shamba kutoka Wilaya ya kaskazini B Unguja Juma Kona Mosi, alisema kupitia mradi wa viungo umewawezesha hata wao watalamu wa kilimo kufahamu kuwa kila sehemu inawezekana kufanya kilimo cha mboga mboga na sio kama walivyokuwa wakidhani hapo awali kuwa kilimo hicho kinahitaji maeneo maalumu tu.

 

Alitolea mfano shehia ya Donge kiongwe kidogo mkoa wa kaskazini Unguja, alisema kuwa miaka mingi wao kama watalamu wa kilimo waliamini kuwa eneo hilo halifai kuanzisha kilimo cha mboga mboga kutokana na ardhi yake kuwa ya mchanga lakini kumbe zipo mbinu mbali mbali ambazo zinawezesha kilimo hicho kufanya vizuri katika eneo hilo.

 

Alieleza kuwa kupitia elimu waliopatiwa na kisha kuwawezesha wakulima hivi sasa ndani ya shehia ya donge kiongwe kidogo akinamama wengi wanajihusisha na kilimo cha mboga mboga na tayari wanavuna kila baada ya muda.

 

Sambamba na hilo alisema wao kama mabwana shamba  walikua na sehemu nyengine za kazi hawakuwahi kufika kutokana na chanagmoto mbali mbali na waliami n kusingekua na haja ya kufika kutokana  na walio wengi kukosa muamko pamoja na kukata tamaa lakini hivi sasa wengi wa watu hao wamekua wakulima na wenye kupata faida kubwa.

 

Nae Khadija Msonda kutoka shehia ya Mbaleni alisema awali kabla ya ujio wa mradi wa viungo walitumia nguvu nyingi kwenye kilimo kiasi cha kwamba kama wanawake wapo walioshindwa kutekeleza majukumu mengine ya msingi kwenye familia zao na wakati mwengine kusababisha hata ugomvi ndani ya ndoa.

 

Alisema kufuatia ujio wa mradi huo umeleta faraja kubwa kwao kwani hivi sasa hawatumii muda mwingi kwenye kilimo lakini wanapata faida kubwa na kuwashirikisha wengine zaidi samba nan a kuepusha migogoro isiokua ya lazima ndani ya ndoa.

 

Aidha alisema inawezekana kukosekana kwa mbinu mbadala hapo awali kuliwafanya akinamama wengi kushindwa kujikita kwenye kilimo, waliamini kuwa wasingeweza kunufaika badala yake walijikita na shughuli nyengine zikiwemo kilimo cha mwani lakini, hivi sasa watu wengi wamehamasisha na wamejikita kweye mradi huo.

 

Nae Amina Kheri alisema ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji mradi huo umewaamsha akinama wengi kufahamu umuhimu wa kulima na kula mboga mboga kinyume na ilivokua mwanzoni.

 

Alisema  licha ya mradi huo kujikita na kilimo lakini pia utapunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la akinamama wanaohitaji damu wakati wa kujifungua baada ya kujiwekea utaratibu wa kula mboga mboga  wanazolima kwa muda na siku wanayotaka wenyewe.

 

Awali akifungua mkutano huo meneja mkuu utekelezaji wa mradi huo Amina Ussi Khamis aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia fursa hio kueleza yale walioyaona na kupendekeza mambo gani mapya yafanyike kwa mwaka wa pili ili kuongeza kasi ya uzalishaji na mafanikio zaidi kwa wakulima na Serikali kwa ujumla.

 

Mkutano huu wa siku mbili unaofanyika katika ofisiz za utekekelezaji mradi huo Mwanakwerekwe mjini hapa ,umewashirikisha mabawana shamba pamoja na wakulima wawezeshaji wapata 72 kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja kupitia mradi wa Viungo ambao unafadhiliwa na umoja wa Ulaya na kutekelezwa na PDF,TAMWA,ZNZ pamoja na CFP huku ukilenga kuwafikisha wanufaika 57,000 kutoka Unguja na Pemba. 


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.