Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla Ahimiza Wananchi Kujitokeza katika Chanjo ya Uviko 19.

Mlezi wa Ccm Mkoa wa Tanga na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah akiongea na wananchi wa Kibirashi.
Wanachama wa Ccm wa shina namba 5 lililopo kijiji cha Kibirashi, kaka Kibirashi wilayani Kilindi wakimsikiliza mlezi wa chama hicho kwa Mko wa Tanga Hemed Suleiman Abdullah.
Mbunge wa Jimbo la Kilindi Omari Kidua akiongea na wananchi kabla ya kumkaribisha mlezi wao.

  Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adamu Malima akiongea na wananchi mbele ya mlezi wao.

Na Hamida Kamchalla, KILINDI.

Mlezi wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemedi Suleiman Abdallah amewahimiza wananchi kuachana na maneno yanayopotosha badala yake kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo ya Uviko 19 ili kuendelea kuwa salama ikiwa ni pamoja na kujitokeza kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi pindi itakapoanza.

Makamu huyo aliyasema hayo jana  wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kibirashi wilayani Kilindi alipofanya ziara ya kikazi na pia kuzindua mashina ya chama hicho.

"Wananchi wenzangu, tunafahamu kama kuna huu ugonjwa wa Uviko 19, na serikali imechukua juhudi kubwa ya kuleta chanjo, wapo watu ambao wanababaisha, wanajaribu kutoa lugha tofauti kuwapotpsha watu, ndugu zangu wa Kibirashi na maeneo mengi ya jirani, chanjo zipo nadhani utaratibu kwenye Mkoa upo, twendeni tukapige chanjo tujikinge, chanjo ni bora kuliko kutibu" alisisitiza.

"Jingine ni kuhusu suala la sensa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano ameshazindua zoezi la sensa, madhumuni ya sensa hii ni kuhesabiwa na tujulikane hesabu yetu ili serikali iweze kupanga mahesabu yake, kwahiyo niwaombe Wanakilindi na Watanzania wote, wa vyama vyote nimiombeni mjitokeze kwa wingi tukahesabiwe muda utakapowadia" alisema.

Aidha Makamu huyo alitoa ahadi ya kushirikiana na viongozi mkoani humo kuhakikisha wanaifanyia matengenezo barabara itokayo Handeni hadi Songe huku akisisitiza kwamba barabara hiyo ni muhimu na ina manufaa makubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa kutokana na mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari.

"Tulipokuja tumetembea kwenye barabara ya lami, lakini tulipofika Handeni tumeingia kwenye barabara hii ambayo mmeizungumza, nimepata maelezo yake, na nimeona umuhimu wa barabara hii, naomba niwahakikishie kwamba sikuja Wilaya hii wala Mkoa wa Tanga kutembea, nimekuja kuhakikisha ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa" albainisha.

"Nitashirikiana na viongozi wenzangu, wapo waheshimiwa wabunge wanafanya kazi nzuri na mimi nitashirikiana nao, na mimi kwa nafasi yangu kule kwenye kamati nitapata kuchomekachomeka kwa sababu mwenyekiti anakuwa hayuko mbali" aliongeza.

Alibainisha kwamba "faida ya barabara hii ni kubwa sana na siyo kwa Wanakilindi tu bali ni kwa Watanzania wote, Tanga tuna Bandari, ikitumika vyema Bandari ya Tanga na barabara hii ikawa rafiki, nakuhakikishieni uchumi wa Mkoa wetu utakua kwa kiasi kikubwa, kwahiyo nikuhakikishieni suala hili la barabara tutaenda nalo pamoja".

Hata hivyo aliwahakikishia wananchi hao kuwatatulia kero nyingine mbalimbali zilizopo ambazo katika sekta ya maji, elimu pamoja na afya huku akisema watashirikiana kwa ukaribu katika utekelezaji kwa maslahi ya wananchi hao.

Awali akizungumza katika mkutano huo, mbunge wa Kilindi Omari Kigua alielezea kero zinazoikabili wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za utekelezaji na hatua zilizofanywa na serikali.

"Katika sekta ya maji, elimu, afya na umeme, katika shina hili tunayo shule ya sekondari na hivi leo ninavyozungumza tumeshapewa sh milioni 55 kwa ajili ya madarasa manne na matundu 12 ya vyoo kwa ajili ya vijana wetu, lakini pia tumeongezewa sh milioni 48 kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika kata hii ya Kibirashi ambayo shina hili namba tano ipo" alisema.

"Halikadhalika barabara hii ni ya vumbi muheshimiwa lakini serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mwaka huu wa fedha imetutengea fedha takribani sh milioni 500 na wana dhamira ya kutengeneza kilomita 20 za barabara kuanzia Handeni na kwavile wewe ni mlezi utaondoka nalo" aliobngeza.

Mbunge huyo pia alifafanua kwamba
"Kilindi hii ina madini, mifugo na rasilimali nyingine lakini uchumi wa wananchi haukui kwasababu ya barabara haipitiki, tunaomba sana, sisi kwetu tunaona kama leo ni ukombozi, ukitoka hapa utupelekee salamu zetu kwa mwenyekiti kwamba, mbunge na wananchi wa Ccm wanaomba uwatengenezee barabara".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.