Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa
Serikali imeamua kuchukua maamuzi magumu ya kuziuza meli zote za Shirika la Meli
la Zanzibar kutokana na gharama kubwa za
uendeshaji.
Akitoa hotuba yake katika majumuisho ya ziara yake kwa mikoa miwili ya Pemba, yaliyofanyika katika ukumbi wa kiwanja cha kufurahishia watoto Gombani, Chake Chake Pemba, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uamuzi huo umekuja kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa meli hizo za Serikali.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa meli hizo za Serikali zilizo chini ya Shirika la Meli la Zanzibar zitauzwa kwa lengo la kununua meli ambazo hazitokuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Aidha, Rais DK. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inaimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuendelea kuliimarisha na kulipa hadhi yake zao la karafuu.
Akizungumzia juu ya suala la udhalilishaji, Rais Dk. Mwinyi alitilia mkazo kwamba wale wote wanaotenda vitendo hivyo waendelee kutopewa dhamana na hata mahabusu ikijaa basi wapelekwe katika vyuo vya mafunzo wakisubiri kesi zao.
Pamoja na hayo, aliwataka viongozi wa Mikoa na Wilaya kusikiliza kesi za wananchi waliodhulumiwa haki zao huku akisisitiza kwamba watumishi wote ambao hawawajibiki ataendelea kuwachukulia hatua wakiwemo wale wabadhirifu na wezi wa mali za umma ataendelea kwuafukuza.
Mapema asubuhi akizungumza na wanannchi wa Wilaya ya Mkoani mara baada ya hafla ya kukabidhi boti kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Makongwe na Kisiwapanza alisema kuwa Serikali itafanya juu chini kuweza kuwaletea maendeleo wananchi kama ilivyowaahidi wakati wanapita kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na kuwa tena Madarakani.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa
anatambuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo katika kipindi kilichopita ni
kukosekana umoja wa wananchi na
mshikamano na ndio Serikali ya awamu ya nane imetengeneza serikali ya Umoja wa
kitaifa ikiwa na lengo la kuleta amani na umoja utakaokuza maendeleo ya haraka.
Alifahamisha kuwa ni jambo la
kushukuru kuwa nchi kwa sasa imetulia ina amani na hakuna sababu kusipatikane
maendeleo na aliwapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi hizo zilizochukuliwa
na viongozi wao.
Aliongeza kuwa hatua aliyoichukua
ya kuwakabidhi boti za kusafiria wananchi wanaoishi ndani ya visiwa vidogo
ndogo vilivyoko Pemba ni kutokana na
kuwa na haja ya kusaidiwa ili waweze kupata vivuko vya uhakika badala ya
kutumia vivuko visivyo na uhakika vyenye kuhatarisha maisha yao.
Alieleza vivuko hivyo viwili
amevikabidhi katika bandari hiyo kwa niaba ya visiwa vyengine vitano (5) vya
Zanzibar, ni wazi kuwa wananchi hao wanaoishi visiwani watapata usafiri wa
uhakika na kuwaomba wavitunze
vizuri ili vitowe huduma kwa wananchi
mbali mbali .
Akizungumzia uimarishaji wa
Bandari ya Mkoani alitowa agizo kuwa wakati umefika wa kuziimarisha Bandari zote
hapa Zanzibar na hakuna sababu kwa meli zinatoka Mombasa zikateremshe bidhaa Unguja
na ndipo ziende Pemba.
Hata hivyo, alisema hakuna
sababu meli kutoka Dar-es-Salaam zikateremshe mzigo Unguja na ndipo ziende kisiwani Pemba hali ambayo inaongeza gharama ya
usafirishaji na inapelekea bidhaa Pemba kuwa ghali.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa ameliagiza
mamlaka ya Bandari sasa waanze kuweka
mtaji wao (fedha ) ili Bandari hizi ziweze kupokea meli kutoka nje moja kwa
moja na kuna habari njema kuwa kuna meli
kadhaa zimeshaonesha nia yakuzileta moja kwa moja kutoka Dar-es-salaam na
Mombasa mpaka Bandari ya Mkoani Pemba.
Sambamba na hayo Dk. Mwinyi
alisema, kuna kila sababu sasa ya kuweka mazingiza ya kusubiria usafiri abiria
kuwa bora zaidi kwani faida tayari imeweza kupatikana baada ya kufunga mianya
ambayo imekua ikipoteza fedha hivyo, aliitaka Wizara ya bandari kuzitumia fedha
hizo kwa matengenezo ya bandari zote ikiwemo Mkoani na Wete.
Wakati huo huo,
Dk. Mwinyi alitembelea hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani na kuwapongeza
Madaktari wa kichina wanaomaliza muda wao kwa vile wanatowa huduma katika hiyo
na kusema mchango wao ni mkubwa unathaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwani kuna baadhi ya huduma bila ya mchango wao zengeyumba.
Aidha Dk, Mwinyi aliwapongeza
wafadhili waliotowa misaada ya vifaa mbali mbali kwa ajili ya Hospitali ya
Abdalla Mzee, Mkoani akiwemo Said Bopar na kusema kuwa misaada hiyo ni muhimu sana.
Aidha, alimpongeza na kumshukuru Mwakilishi wa Jimbo
la Mkoani Mhe.Abdalla Hussein Kombo kwa kukabidhi gari la kubebea wagonjwa katika
Hospitali hiyo ya Abdalla Mzee Mkoani na kuisaidia Serikali yake kwani kwa
Hospitali kama hiyo ni muhimu kuwa na gari ya aina hiyo.
Dk, Mwinyi aliwashukuru
wafanyakazi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani kwa kufanya kazi katika
mazingira magumu na kusema amesikia matatizo mbali mbali wanayokabiliana nayo
kutoka kwa mganga mkuu wa Hospitali hiyo
Dk, Haji Mwita.
Sambamba na hayo,
Rais Dk. Mwinyi leo aliungana na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Msikiti wa
Ibadhi, Mkanjuni Chake Chake Pemba katika sala ya Ijumaa na kusisitiza suala
zima la amani, umoja na mshikamano wakati akitoa salamu kw awaumini hao.
Rais Dk. Mwinyi amemaliza ziara
yake ya siku tano kisiwani Pemba na kurudi Unguja ambapo katika ziara hiyo
alifutana na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serrikali akiwemo Mama
Mariam Mwinyi.
No comments:
Post a Comment