Habari za Punde

Zanzibar imepiga hatua kubwa kupunguza virusi vinavyosababisha maambukizi ya maradhi ya UKIMWI

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais OMKR Dkt Omar Dadi Shajak akiwa na Mkurugenzi wa Unaids TANZANIA  Dkt Leopold Zekeng Ofisini Kwake Migombani

Na.Raya Hamad- OMKR.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak amesema kwamba Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kupunguza virusi vinavyosababisha  maambukizi ya maradhi ya UKIMWI.

Dkt Shajak ameeleza hayo leo  alipozungunza na Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI Dkt Leopold Zekeng Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Amesema jitihada zinazofanywa na serikali kupitia Tume ya inayoratibu mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar zimesaidia sana kuwepo mafanikio makubwa na kwamba maambukizi yamepungua kutoka asilimia 0.6 hadi 0.4

Dk shajak amefahamisha kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na jitihada zake hizo ili kuwezesha kutimiza lengo la Zanzibar ifikapo mwaka 2025 kusiwepo tena maambukizi mapya ya maradhi ya UKIMWI Zanzibar.

Aidha alishukuru Shirika la Umoja wa Matafa la kupambana na UKIMWI (UNAIDS) kwa kuonesha nia ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika harakati za mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI.

Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Tume ya UKIMWI inaendelea kutoa elimu na kuhakikisha kuwa jamii inaongeza uelewa juu ya masuala mbali mbali yanyohusu UKIMWI ili kuisaidia jamii  kujiepusha na tabia  hatarishi zinazochangia  kasi ya maambukuzi ya virusi vya maradhi ya Ukimwi.

Nae Mkurugenzi mkaazi wa UNAID Dkt Leopold Zekeng amesema Shirka hilo  litaendelea kuisaidia Zanzibar  kuunga mkono jitihada  za kupambana na  UKIMWI ili kuhakikisha hakuna maambukizi mapya kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.