Habari za Punde

ZEC yashauriwa kushirikiana na Asasi za kiraia

 Na Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeshauriwa kushirikiana na Asasi za Kiraia katika kufanya ushawishi kwa Vyama vya Siasa kuwashirikisha wanawake kugombea nafasi mbali mbali za Uchaguzi

Ushauri huo ulitolewa na Mjumbe kutoka Jukwaa la Mtandao wa Asasi za Kiraia ambaye pia ni Mjumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Tawi la Zanzibar Bi Hawra Mohammed Shamte wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi Maalum katika kikao kilichofanyika Afisi za Tume Maisara Mjini Zanzibar.

Bi Hawra alisema, Tume ya Uchaguzi ilianzisha Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi Maalum  ya kijamii ya mwaka 2015 kwa lengo la kuhakikisha Makundi yote ya kijamii  yakiwemo Wanawake, vijana na Watu wenye ulemavu wanashiriki katika hatua zote za Uchaguzi ikiwemo kugombea katika chaguzi zinazoendeshwa  Zanzibar .

Aliendelea kusema kuwa, Jukwaa la Mtandao wa Asasi za Kiraia ambalo limeundwa na TAMWA Upande wa Zanzibar, Jumuiya ya Waandishi wa Habari wenye ulemavu Zanzibar, Mtandao wa Vijana Zanzibar na Mtandao wa Asasi za Kiraia wameipitia Sera na kufanya utafiti wa utekelezaji wake kwa kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania Upande wa Zanzibar Dkt. Mzuri Issa aliipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuandaa Sera nzuri yenye nia ya kuendesha Uchaguzi unaowashirikisha Wadau wa Makundi Maalum ya Kijamii katika hatua zote za Uchaguzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali Watu, Mipango na Uendeshaji Saadun Ahmed Khamis aliwaomba Wadau wa Uchaguzi wakiwemo vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia kuipitia Sera hiyo na kuwasilisha changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Bwana Saaduni aliipongeza TAMWA kwa vile ni Taasisi ya mwanzo kuipitia na kuifanyia kazi Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi Maalum ya Kijamii ya mwaka 2015 iliyotungwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuwasilisha changamoto zao ambazo wameziona ni kikwanzo katika utekelezaji wake.

Naye, Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano ya Umma ZEC Juma Sanifu Sheha alisema Tume inafanya kila jitihada kuhakikisha Wanawake, Watu wazima na Watu wenye ulemavu wa aina zote wanashiriki katika Uchaguzi bila ya Kikwanzo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya kiuchaguzi kwa kuzingatia mahitaji ya Makundi yao, kutoa vitambulisho siku ya kupiga kura ili wasipange foleni na kuandaa kifaa maalumu cha kupigia kura kwa Watu wasioona kinacho wawezesha kupiga kura wenyewe bila kuhitaji msaada.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.