Habari za Punde

Wakulima wa Mazao ya Viungo Wilayani Muheza Mkoani Tanga Waaza Kurudisha Matumaini.

Wakulima wa mazao ya viungo wakiwa shambani wakionyesha namna ya pilipilimanga zinavyozaliwa.
Wakina mama wakichambua pilipilimanga zilizokausha tayari kwa kupakiwa kwenye viroba.
Vijana wakikwangua magome ya viungo vya amdalasini kiwandani hapo ili kabla ya kukaushwa.
Mfanyakazi wa Kiwanda cha TRINON SPICES akisafisha pilipili manga kwenye mashine maalum baada ya kutoka shambani tayari kwa kuzikausha kwa matumizi 

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

Wakulima wa mazao ya viungo na wananchi wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wameanza kupata manufaa baada ya uwepo kwa karibu Kampuni ya TRIANON SPICES ambacho kinajihusisha na ununuzi wa mazao hayo ikiwa ni pamoja na kuwa karibu nao kwa kuwapa msada wa kilimo bora.

Kampuni hiyo yenye miaka miwili tu tangu kuanzishwa kwake ambayo ina masoko yake nchi za Ulaya imeanza kurudisha imani na mwamko kwa wakulima wengi ambao walianza kukata tamaa kutokana na kutokuwa na uelewa wa kuhudumia mimea mashambani pindi inapopata matatizo ya kushambuliwa na wadudu waharibifu.

Ndani ya muda mfupi wameweza kuwasaidia wakulima hao katika kuwapatia madawa ya kuua wadudu waharibifu waliovamia mazao yao ambayo yalianza miaka takribani 10 iliyopita na kuwasababishia hasara kubwa wakulima kwa kukosa mavuno ambayo ndio tegemezi lao katika kuendeshea maisha yao ya kila siku.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Edward Rukaka ameeleza kwamba kiwanda kinajihusisha na ununuzi wa mazao ya wakulima ambayo ni viungo na wanayaandaa kiwandani kwa kuyaongezea thamani na baada ya hapo wanasafirisha nje ya nchi.

"Soko letu kubwa liko Bara la Ulaya, tuna mwaka wa pili huu na kwasasa tunapanua wigo zaidi kwani kiwango cha uzalishaji kinaenda kinapungua kwasababu kule kwenye soko tuna wanunuzi wengi, kwahiyo tusipofanya mkakati wa kuwawezesha wakulima ili wazalishe zaidi itafika hatua tutajikuta hatuna mazao ya kutosha kwa ajili ya kuendesha kiwanda" alisema.

"Kwahiyo tunachokifanya ni kwamba tunanunua mazao kwao halafu pia tunawahamasisha wapande zaidi, lakini sisi tumepanda vitalu vya kuzalisha mbegu bora za viungo na kuwapatia bure wakulima ili waweze kuzalisha na kuongeza wigo kwa kutumia tekinolojia ya kilimo hai pamoja na kilimo msitu, hii inawawezesha wao kulima zaidi bila kukata miti mingi" alibainisha.

"Lakini pia tunafanya mikakati ya kushirikiana na wadau wetu Kampuni ya TAHA katika kudhibiti ugonjwa ambao umeikumba Wilaya ya Muheza kwenye mazao yetu ya viungo, na hii ilikuwa inasababisha wakulima wengi waache kulima na kuzalisha kwasababu wanapata mavuno kidogo hivyo kufanya mauzo yao kuwa kidogo zaidi" aliendelea kueleza.

Aidha Rukaka alifafanua, "lakini pia hawakuwa wanajua ni suluhisho gani watatumia kwa ajili ya kudhibiti haya magonjwa, hii imesaidia sana na sasa imani yao imerudi na tunakaribia kumaliza awamu ya kwanza ya udhibiti wa haya magonjwa na baada ya hapa tuna uhakika kuanzia mwakani mazao yataongezeka na wakulima wengi wamehamasika kwasababu wana uhakika wa soko".

Rukaka alibainisha kwamba kiwango cha uzalishaji ambacho wanakifanya kinakidhi uwezo wao ambao wamewekeza hivyo hata wakipanua zaidi ukubwa wa kiwanda na kuhitaji kuongeza uzalishaji wataweza kurudi kwa wakulima ambao wamewekeza kwao kwa kuwapatia mbegu kwakuwa watakuwa wameongeza kiwango cha uzalishaji.

Hata hivyo alibainisha kero ya ubovu wa miundombinu ya barabara kwenda mashambani ambapo aliiomba serikali kufanya maboresho kwakuwa mazao hayo yaningiza mapato ya halmashauri kwa wingi lakini pia ni katika kuwasaidia wakulima wapate wepesi wa kutoa mazao yao wakati wa mavuno.

"Niombe halmashauri iangalie namna ya kurudisha fedha kwa wakulima, katika yale mapato wanayochukua basi watenge kiasi cha fedha kwa ajili ya kukarabati barabara za mashambani ili kuwasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwani wapo wengine ni wazee na wanalima mazao kidogo hivyo wanaona gharama ya kuleta kwa wanunuzi na kuishia kuuza mashambani huku wakiuza kwa bei ndogo" alisisitiza.

Kwa upande wa wakulima wa mazao hayo walieleza kwamba awali walipoona kilimo hicho kinasuasua kwa mazao kuharibika mashambani walikata tamaa ya kuendelea kulima lakini tangu wameanza kupata msaada wa kilimo hicho wengi wamepata mwamko na kuongeza mashamba wakati wengine wakianza kulima.

Wakulima hao walibainisha kwamba baada ya kupata changamoto ya mazao yao kuingiliwa na ugonjwa walisumbuka kwa muda mrefu lakini baada ya kupatiwa dawa za kukabiliana na ugonjwa huo wamepata imani kutokana na mimea kukaa vizuri na kuleta matumaini ambapo mazao yanaendelea kunawiri na wana uhakika wa kuanza kuvuna kuanzia mwezi wa kumi mwaka huu.

"Baada ya mazao yetu kupata ugonjwa wa unyaufu tulikata tamaa ya kuendelea kulima lakini baada ya kupeleka kilio chetu halmashauri tulipata msaada wa dawa kupitia kwenye Taasisi, tunashukuru dawa imeanza kufanya kazi na imetusaidia sana, wapo wengine ambao mazao yao yamepona kabisa na mwezi ujao tunatarajia kuanza mavuno" alisema Hassan Chakusaga mkulima wa zao la pilipilimanga katika kijiji cha Bombani.

Waliendelea kusema pamoja na msaada mkubwa waliopatiwa bado wanaiomba halmashauri na wafadhili kuwapatia dawa hizo kwa karibu lakini pia ikiwa ni katika punguzo la bei ambapo walidai dawa hizo zinapatikana mkoani Arusha kwa bei ya shilingi laki mbili na nusu kwa kopo moja hali ambayo inawawia vigumu kwa wakulima kumudu gharama hizo.

Chakusaga pia alisema "kwa sasa tuna changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora ambazo zitatupatia mazao katika viwango ambavyo vitaingia sokoni bila pingamizi kutokana na kwamba mbegu tulizonazo siyo bora ni bora mbegu, lakini pia kingine tuna changamoto ya miundombinu ya barabara za kuingia mashambani, tunapata tabu sana wakati wa kuvuna na kukusanya mazao kufika sokoni".

Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Nassib Mmbagga alisema tayari TARURA wapo kazini na barabara zote zilizoko Tarafa ya Amani ambako ndio kuna kilimo cha mazao ya viungo zinatengenezwa.

"Barabara tunatengeneza, kwasababu maeneo yote hayo wanayolima mazao ya viungo katika Tarafa ya Amani na maeneo ya Ngomole barabara zinatengenezwa, ni kwa taratibu huwezi kusema unatengeneza barabara leo ukiamka tayari, TARURA wako wanaendelea na matengenezo katika barabara hizo zinazopita maeneo ya mashambani" alieleza. 

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba mazao hayo yanaingiza mapato kwa kiasi kikubwa na kuna Muwekezaji mwengine ambaye ameshachukua eneo lenye takrini hekta mia tano na tayari ameshaanza kilimo hicho kwa ekari mia mbili katika maeneo ya Kambai lakini pia yuko kwenye harakati za ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao hayo.

"Lakini pia tuna maeneo mengine ambayo yanalima na yatakuwa na uzalishaji mkubwa kuliko kule juu Amani, ni Tarafa hiyo hiyo lakini ni meneo ya chini tuna Muwekezaji kule ana hekta mia tano na tayari ameshalima na kupanda hekta zaidi ya mia mbili kwahiyo utaona kwamba kutakiwa na uzalishaji mkubaa sana kuliko maeneo ya Amani na kwengineko kwakuwa ukienda kule utakuta wamechanganya mazao kama migomba lakini Kambai ni kilimo hicho pekeyake" alisema Mmbagga.

Nao wananchi wakazi wa kijiji cha Lusanga wilayani Muheza ambapo ndipo palipo na kiwanda hicho walisema wanshukuru kwa uwepo wa kiwanda kwakuwa kinawasaidia kwa kiwapatia ajira kwa kufanya kazi za kuandaa viungo baada ya kutoka mashambani kabla ya kuingizwa kiwandani.

"Tunamshukuru sana huyu aliyeanzisha kiwanda hiki maana tunaponea hapo, tunapata ajira za kuchambua viungo kwa kutoa uchafu ambao hautakiwi kuingia kiwandani, anatusaidia sana tunamaliza matatizo yetu madogo madogo hivyo tunaomba kiwanda kiendelee kuwepo ili nasisi tupate ahueni" alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la 

Naye Ofisa Biashara wq halmashauri ya Qilaya hiyo Gregory Shangai alitoa ufafanuzi kuhusu masoko, mafanikio na changamoto katika mazao hayo na kusema kuwa hali ya biashara ni ya wastani kulingana na mavuni ya wakulima.

"Niseme tu hali ya biashara ni ya wastani, hivi karibuni nimekutana na wakulima kumekaa kikao wakanieleza changamoto zao ambazo kubwa kibiashara ni uhifadhi na ukaushaji wa mazao, katika mnyororo wa thamani wao wanaishia kuweka kwenye madaraja kwa maana ya kukausha ili yaweze kudumu kwa muda mrefu kabla ya kuingizwa sokoni" alisema.

"Tuna masoko aina mbili ambayo ni wanunuzi wa viwandani na wqfanyabiashara wadogo wadogo ambao wanakwenda kuyaongezea thamani viwandani na wao wanayauza katika masoko ya nje ya nchi" alifafanya.

Aidha Shangai alisema mbali na changamoto za wakulima pia zipo za wafanyabiashara wadogo wadogo ambao ndio wanunuzi wa ndani, kwamba hawana mitaji hivyo wanatumia tekinolojia duni katika kuyaongezea thamanu mazai na kujikuta wanakinzana na hali ya hewa hasa katika ukaushaji wa mazao ya iliki na karafuu.

"Mazao haya yanatupatia faida katika halmashauri yetu kupitia ushuru lakini pia kitendo cha mkulima kupata kipato chake cha kila siku na kujitengenezea maisha yake inatosha kuona ni jinsi gani maxao ya viungo yana faida kubwa kwetu" alifafanua".
"Nipende kutoa wito kwa hawa wanunuzi ambao ni wafanyabiashara wadogowadogo, wajiunge na vikundi wawe na umoja wao utakaowawezesha kupata mitaji na kununua zana za kisasa za kuongeza thamani ya mazao kwani wataweza kujiimarisha zaidi na watamudu kupata mazao yenye viwango vya ubora ambayo yataingia kwenye masoko" alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.