WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Joachim Mhagama (MB) (kulia) akimkabidhi mkoba wenye Nyaraka mbalimbali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF). Bw. Emmanuel Humba, mara baada ya kuzindua Bodi hiyo mkoani Morogoro Oktoba 4, 2021
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge,
Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Joachim Mhagama (MB),
amezindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) leo Tarehe
4/10/2021 Mjini Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Jenista Mhagama
amempongeza Mwenyekiti Mpya wa Bodi hiyo Bw. Emmanuel Humba kwa kuaminiwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa
kushika wadhifa huo na pia amewapongeza Wajumbe wa Bodi aliowateua na kuwataka
waende kuusimamia Mfuko kwa kushirikiana na Menejimenti ili kufikia matarajio
ya Serikali.
Wajumbe wapya wa Bodi walioteuliwa na Mhe. Waziri Jenista Mhagama ni pamoja na Ornorius John Njole, Perfect Raphael Kilenzi, Ibrahim Barnabas Mahuni, Abdulaziz Alladin Shambe, Rifai A. Mkumba, Raymond Kaseko, Julian C.N. Mpanduji, Rehema Rashid Ludanga na Felix Kagisa Rugarabamu.
Mhe. Jenista Mhagama amewataka wajumbe hao kuyaelewa vema
majukumu yao kama yalivyoanishwa kisheria katika kifungu cha 13, 14, 15 na 16, na
sehemu ya majukumu hayo ni pamoja na kusimamia maslahi ya wafanyakazi
yanayotokana na kuanzishwa kwa sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
“ Kumekuwa na
Mafanikio makubwa ya Mfuko katika kipindi hiki cha miaka sita na mnatakiwa
kuyalinda kwa wivu na kwa nguvu zenu zote.” Alifafanua na kutoa mfano………katika
kipindi ambacho bodi haikuwepo, thamani ya Mfuko imekuwa hadi kufikia shilingi
za Kitanzania bilioni 445.49 kutoka thamani ya Mfuko ya shilingi bilioni 112.83 mwaka 2016/2017, huu ni ukuaji mkubwa sana na
tunaona kuna kazi kubwa imefanyika, lindeni mafanikio haya.” Alisisitiza.
Akizungumzia ulipaji wa Mafao, Mhe. Waziri Mhagama alisema kufikia mwaka 2020/2021 Mfuko ulilipa Mafao ya Wafanyakazi waliopata ajali kazini shilingi bilioni 12.43 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017 ambapo zililipwa shilingi bilioni 1.55 tu.
Aidha aliwaasa Wajumbe wa Bodi kuelewa vema lengo la uwepo
wa Mfuko ambapo ni kuhakikisha Wafanyakazi wanaoumia, Kuugua ama Kufariki
kutokana na Kazi zao kwa mujibu wa Mikataba ya Ajira zao basi Serikali kupitia
WCF iwalipe fidia au iwatibu na wakipona warejee kazini kuendelea na majukumu
yao.
“Kubwa ni kuendelea kuweka mkazo kwenye utoaji elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili waujue Mfuko na majukumu yake sambamba na kutoa mafunzo kwa madaktari wengi zaidi iwezekanavyo ili waweze kutoa huduma kwenye maeneo mengi ya nchi yetu, " alisema Mhe. Mhagama na kuongeza ......hivi sasa tunasema tuko kwenye uchumi wa viwanda, viashiria vingi vya uwepo wa ajali kazini na eneo mojawapo ni kwenye sekta ya Viwanda na Usafirishaj kwahiyo huduma za WCF zinahitajika sana katika kutoa hakikisho kwa wafanyakazi kuwa wachape kazi na hivyo kuongeza uzalishaji.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuael Humba alimuhakikishia Mheshimiwa Waziri
Mhagama kuwa watahakikisha Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake kulingana
na malengo ya Mfuko na matarajio ya Serikali.
“Mashirika mengi yanakufa kutokana na kujisahau kwa
waliopewa dhamana ya kusimamiwa mashirika haya, sisi ni wadhamini tu, na
kwahiyo udhamini wetu lazima tuulinde kwa hali na mali kwa kutenda haki.”
Alisema Bw. Humba.
Bw. Humba alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kuongoza Bodi hiyo na kutoa
hakikisho ya kufanya kazi kwa uwezo wake wote.
“Naomba wajumbe wenzangu tuutendee haki uaminifu ambao
Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais wametupatia kwa kufanya kazi kwa Weledi na
bidii kwa hiyo nawaombeni tutende haki.” Alibainisha.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma alimpongeza
Mwenyekiti wa Bodi Bw. Emmanuel Humba kwa kuaminiwa kupewa dhamana hiyo kwa
kipindi cha pili lakini pia kuwapongeza wajumbe wote walioteuliwa na Mheshimiwa
Waziri katika kuendesha gurudumu la Mfuko.
Alimpongeza Mhe. Waziri kwa kuteua wajumbe kwa kuzingatia
kubakia kumbukumbu ya Taasisi kwa kuwabakisha wachache waliokuwepo na kuteua
wengine wapya hali itakayosaidia kuufikisha Mfuko mahala panapostahili.
No comments:
Post a Comment