Habari za Punde

NAUSHAD: MCHANGO WAKE KWA SOKA YA ZANZIBAR

 


Na Ally Saleh Alberto

KAMA kuna mtu katika uhai wangu ninaye muona kutoa mchango mkubwa katika soka ya Zanzibar basi huyo atakuwa ni Naushad Muhammed Suleiman.

Nimepata taarifa iliyonihuzunisha ya kifo cha Naushad ambaye kwa hakika angepaswa kuandikiwa kuhusu historia yake wakati yeye mwenyewe akiwa hai, watu wajue makubwa mno aliyoyafanya. 

Lakini baada ya maisha ya soka Naushad alizama katika biashara zake na hakutaka pia kwa sababu za kidini niweze kumuandikia juu ya namna alivyolifanya soka la Zanzibar kuwa katika kiwango cha juu Afrika.

Naushad alikua ni mpenzi na mfadhili wa timu moja tu ya Malindi ambako alitia moyo na pesa zake na klabu hio ikatawala soka ya Zanzibar, ikawa moja ya kuogopewa Tanzania na hata Afrika Mashariki  na kuijengea heshima Zanzibar barani Afrika.

Naushad binafsi alicheza mpira na kufikia kiwango cha ligi kuu akiwa ni mlinzi wa kulia wa timu ya Malindi. Alikuwa beki aliyetumia nguvu na moja  ya makocha waliomdundisha ni Ali Fereji. 

Mwenyenzi Mungu alipomjaalia kuinuka kiuchumi Naushad alichagua mpira wa miguu ndio raha na furaha kama matajiri wengi wa hapa ndani na nje.

Kwa kutumia pesa zake Naushad, wakati huo, vipaji vya soka viko kiwango bora Zanzibar ns Tanzania, aliweza kuwaleta nyota kadhaa kutoka Bara kucheza ligi kuu yetu. 

Baadhi ni mlinda mlango Yassin, Athanas Maiko, Twaha Hamidu Noriega, Edibily Jonathan Lunyamila ambae wengi hawajui alianzia Malindi kabla kucheza kwa mafanikio huko Young Africans.

Hapa Unguja alikokoa wachezaji wote wakubwa akina Rifat Said, Ali Bushir, Juma Kidishi, Bakar Mmakonde, Othman Abdullah Foreman, Sheha Khamis, Innoscent Haule, Bambo na wengine wengi.

Walikuwepo wachezaji visiki wengi wazaliwa na wakuaji wa Malindi akina Samih, Ali Nassor, Amour Aziz, Zahor na wengine.

Alileta wachezaji kutoka Zambia kama Malitoli na pia kukawa na mchawi wa mapigo ya frikiki kutoka Bulgaria ambapo kikosi cha mchanganyiko huo kilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika. 

Pia Naushad alileta makocha kadhaa wa kigeni kama kutoka Bulgaria na mchawi wa mipango ya soka Hussein Kheti ambaye pia alifundisha Harambee Stars. 

Mara nyingi huwa nasema kwa mchango wake katika tasnia ya soka basi kwa hakika Nausha aliishi kabla wakati wake ambapo falsafa yake ya soka ingefaa wakati huu.

Aliyoyafanya Naushad ndio baada ya miaka tukayaona yakitikea Bara lakini hasa matajiri kujiingiza kwenye soka kama Chelsea, PSG na kwengine. Kabla taasisi fadhili ilikuwa ni makampuni. 

Kikosi cha Malindi ndicho pia kilichochangia Zanzibar kushinda Kombe la Challenge Afrika Mashariki na Kati 1995 kule Mbale, Uganda

Bila ya shaka kila zama na mambo yake. Huwa nikijiuliza hali ingekuwaje Naushad angekuwepo Malindi ya miaka kumi kabla kuibuka na pesa lakini ikiwa na wachezaji wa zama za Mansab, Muhd Issa na wengine.

Sidhani Naushad ambae washauri wake walikuwa kina Seid Rashid, Seif Nassor, Jeff Babu, Mujtaba Marashi na viongozi wengine aliwahi kushauriwa kuwacha msingi wa kudumu wa klabu hio. Na ndio hasara kubwa kwa nchi. 

Tokea mwanzo sio kuwa Malindi ya Naushad haikufungika kama vile pale Shangani ilipochukua ubingwa 1993/1994 na baadae Mlandege ya Abdulsatar Dawood kutawala na Naushad akiwa hai.

Nakumbuka Naushad alivyokuwa mkali wa saikolojia ya soka na mimi nikiwa karibu na Salim Turkey, Rahim Bhaloo na Muhammed Raza tukipanga na kucheza soka nje ya viwanja. Tulikuwa maestro wa fitna ya soka. 

Naushad anapaswa kukumbukwa kwa mchango wake na hasa msingi wa ushindani wa soka aliouasisi ambao ulijenga kiwango cha juu cha ushindani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.