Habari za Punde

Mizengwe ya Sheria Kwa Wanahabari

 

Na.Adeladius Makwega Mbagala.

Pale unapokutana na kinyago mbele yako, utakitazama kwa umakini sana utaangalia namna kilivyo, kilivyochongwa na kuwekewa mapambo. Mara nyingi ukiwa mchambuzi wa kazi za sanaa za uchongaji kama ndugu yangu Profesa Elias Jengo unaweza kwenda mbali kidogo kwa kuangalia namna kinyango hicho kilivyochongwa na hata sababu ya kuwepo kwa baadhi ya vitu.

Hata kama si mchambuzi mwisho wa yote utabaini ahaha kazi hii ni nzuri, ehh amechonga nani? Hapo ndipo utapata jibu kuwa hii ni kazi Lilanga ambaye huchonga vinyago vya mashetani. Hiyo ndiyo kazi ya sanaa namna ilivyo.

Frank Kashonde, Dkt. Ayubu Ryoba, Sudi Mnette, Batlet Milanzi na Shabani Kissu. Hawa ni miongoni mwa wanahabari wachache wa Tanzania wanaofanya kazi katika vyombo vya hapa nyumbani na nje ya Tanzania. Frank Kashonde akitangazia Redio Maria,Dkt Ayub Ryoba TBC,Sudi Mnette Dw Kiswahili, Batleti Milanzi Redio Japan,na Shaban Kissu Chaneli 10.

Ukiwatazama kwa kina wanahabari hao wana elimu kutoka ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu

Hawa ndugu kwanza tunawapa alama za utambulisho Frank kashonde A1, Dkt. Ayub Ryoba A2, Sudi Mnette A3, Batlet Millanzi A4 na Shaban Kissu A5.Badala ya kutumia majina yao tutumie alama za utambulisho tu A1,A2, A3, A4, na A5.

Hawa ndugu tunawapa kazi moja ambayo wote wanatakiwa kuifanya na kila mmoja asitambue kuwa mwenzake anaifanya kazi hiyo ya kihabari. Wakishamaliza kazi zao zote zikusanywe akabidhiwe mtu mwingine ili atazame ubora wa kila kazi.

Kwanza utabaini kuwa kila mmoja atakuwa ni kitu ambacho mwenzake hana. Pili utabaini kuwa kati yao lazima atakuwepo mmoja ambaye atakuwa na kazi bora sana kuliko wenzake.

Tatu ukibahatika kupata mtu ambaye atazipima kazi hizo bila ya kuwafahamu waliozifanya na viwango vyao vya elimu utabaini jambo lingine kubwa sana pengine Watanzania hatujalitilia maanani kama la ubora wa vinyago vya Lilanga vya Mashetani.

Wanahabari wanapokwenda shuleni ni sawa na kalamu ya risasi ambayo haijachongwa vizuri pale mwanahabari anapokwenda shuleni anakwenda kuichonga kalamu yake ili aweze kuandika vizuri.

“Unaweza kuwa na muhitimu ngazi ya diploma akawa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi zaidi muhitimu wa shahada.”Aliwahi kuniambia Profesa Mshana.

Suala la kuwatenga wenye elimu ya cheti kutofanya kazi za kihabari ati hadi wawe ni diploma au shahada ni kosa kubwa sana ambalo halivumiliki. Unapofanya kazi za kihabari siyo cheti kinachofanya kazi hiyo bali ni ule ujuzi wako wa kuifanya kazi hiyo vizuri ambao mtu anaweza kujifunza ata kwa kumuona wenzake namna wanavyofanya kazi.

Wale waliowahi kufanya kazi na Redio Tanzania Dar es Salaam watakusimulia shuhuda nyingi sana za watumishi waliobadilisha kada kutoka kada nyingine na kuwa watangazaji wakubwa wenye sifa za kitaifa na kimataifa.

Wengine walikuwa mafundi mitambo, wakutubi, makarani na wahasibu wakafanya vizuri sana. Leo hii kwa faida ya kujifunza nakutajia majina machache sana kwa mfano Mohammed Darhman Karama (Mohammed Darhman) huyu alikuwa mhasibu wa RTD baadaye akawa mtangazaji wa RTD, akaenda, Redio Japan (NHK) na hadi umauti unamkuta alikuwa mtangazaji wa DW Kiswahili akitangaza vipindi kama Afrika Juma hili na Mbiu ya Mnyonge na hata pengo lake la namna alivyokuwa akitangaza, sauti nzito halijazibika hadi sasa.fano mwingine ni Bi Valeliani Msoka nimewahi kusimuliwa kuwa alikuwa ni Fundi Mitambo wa RTD baadaye alikuja kuwa mtangazaji mzuri wa RTD hadi Sauti ya Ujerumani na akawa mwenyekiti wa TAMWA.

Tanzania kama nchi tunaposema tuwatenge wana habari wenye ngazi ya cheti tukaja na hoja ohh wenye diploma na shahada halina maantiki yoyote ile. Kitendo hiki ni cha kuwabagua wenye elimu ya cheti kwani kwa muda mrefu ndiyo walioweza kuisaidia na taaluma hii kufika hapa ilipo. Kitendo cha kuwaacha wenye elimu ya cheti na hata wenye elimu nyingine kufanya kazi za kihabari kinatoa nafasi kwao kujifunza zaidi na kujiongezea ujuzi wakiwa kazini.

Pia hata taaluma yetu inapata nafasi ya kutumia ujuzi wao wa taaluma zao nyingine kuandika, kuandaa ripoti kwa ujuzi wao mwingine na tunakuwa ripoti zilizoshiba.

Kumekuwa na nadharia ya sheria na kanuni ambalo binafsi ninaliona halina maana wala faidi kwa kuwa kazi ya sheria au kanuni ni kumtia hati yule anayekiuka sheria na kanuni hizo au kutoa mwongozo wa lipi la kufanya pale penye ukinzani tu. Kinyume na hapo sheria inakaa tu katika makabati haina manufaa mengine.

Shida kubwa ya wanahabari Watanzania wengi wanazungumza lugha mbili nazo ni Kiingereza na Kiswahili tu. Wakati mataifa mengine kama Kenya na hata ndugu zetu Wazanzibari ambao wapo katika vyombo vya kimataifa wanazungumza lugha nyingi. Ndugu zetu wa Zanzibar mara baada ya mapinduzi wengi walienda nje ya nchi wakati huku bara Watanganyika wachache sana hasa wale amabao wazazi wao walifanya kazi za kibalozi ndiyo waliweza kwenda nje ya nchi.

Unaweza kuwa na cheti cha uandishi wa habari hapo misingi yote muhimu ya habari unayo alafu mtu huyu anakuwa anazungumza Kiarabu, Kifaransa, Kijeremani , Kiswahili na Kiingereza ukifanya naye usaili mtu huyu hata kama wewe una PHD lazima atakutoa nje.

Wanaopanga sera wasipoteze muda na sheria na vijikanuni vingi tuwekeze nguvu katika kuwaboresha wanahabari wa Tanzania katika kuwa na sifa za ziada za lugha na uwezo wa kufanya kazi nyingi mtu mmoja.

Mathalani mwanahabari mmoja aweza kuandika vizuri, aweza kuandaa taarifa za sauti vizuri , aweza kuandaa taarifa za video vizuri na huku akiweza kupiga picha vizuri na ukimjumuisha na uwezo wake wa lugha zaidi nne hapo Watanzania tunaweza kufika mbali katika taaluma hii.

Chukulia mfano Bi Ummi Kheri Hamiduu ambaye alikuwa mtangazaji wa DW Kiswahili yeye anazungumza kwanza Kiarabu, Kiswahili, Kingazija, Kifaransa, Kingereza,na Kijerumani na aliniambia hata Kiitaliano anazungumza. Bibi huyu ukiweka kando sauti yake yenye mikwiruzo inayovutia masikioni vigumu kumshinda kwenye usaili hata kama wewe una PHD. Anaweza kufanya kazi nyingi hata kuwa ukalimani.

Aliwahi kunisimulia kuwa Wajerumani huwa wanamtumia hadi mahakamani kwenye kesi za watu ambao wanazungumza lugha hizo. Bibi huyu aliniambia kuwa alizaliwa Zanzibar lakini mara baada ya mapinduzi ya 1964 alirudi Komoro kwao yeye na wazazi wake huku akiwa tayari anakijua Kiswahili vizuri kutoka Zanzibar.

Kwa hiyo wapanga sera wanatakiwa kuhimiza watoto wetu wa Kitanzania shuleni kuanza kufundishwa lugha nyingi tangu shule za msingi ili litatoa fursa za jaira nyingi za kitaifa na kimataifa.

Naweka kalamu yangu chini kwa siku ya leo na kusema kuwa Watanzania wenye ngazi yoyote ile ya elimu na hata wenye taaluma zingine wanatakiwa kuendelea kufanya kazi za kihabari huku tuongeze juhudi za kuiboresha taaluma hii kwa kuwapa ujuzi zaidi vijana wanaosomea taaluma hii.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.