Habari za Punde

Tuimarishe Sera ya Watoto kwa Maendeleo ya Taifa - Mhe.Othman.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akikakabidhiwa Jarida la UNICEF na  Kiongozi Mkuu wa UNICEF anayefanyia Kazi zake Ofisi ya Zanzibar, Bi Laxmi Bhawani, alipofika Ofisin kwa azungumzo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Maspud Othman akizungumza na mgeni wake Kiongozi Mkuu wa UNICEF Anayefanyia Kazi zake Ofisi ya Zanzibar, Bi Laxmi Bhawani, mazungumzo hayo yamefanyika Ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuna haja ya kuifanyia mageuzi na mapitio muhimu Sera ya Mtoto ili kuhamasisha maendeleo na ujenzi wa ustawi bora wa maisha ya jamii na Taifa.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) uliomtembelea Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa.

Amesema mageuzi ya Sera hiyo ni pamoja na yale yatakayozingatia huduma za msingi zikiwemo lishe kamili, ambayo ni kichocheo katika kujenga ufahamu na kusaidia makuzi ya jumla ya watoto wa nchi hii.

Akiongelea ulazima wa sera ya maendeleo ya mtoto, Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa sekta hiyo ni muhimu katika kuasisi msingi wa maisha ya baadae na ustawi bora wa Taifa kwa ujumla.

Aidha Mheshimiwa Othman ameeleza namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyotambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mashirika ya Umoja ya Mataifa katika kusaidia maendeleo ya nchi, ikiwemo misaada ya huduma za kijamii.  

Naye Kiongozi Mkuu wa UNICEF Ofisi ya Zanzibar, Bi Laxmi Bhawani ameeleza azma ya Shirika lake katika kuungamkono kasi ya maendeleo ili kwenda na wakati, sambamba na kusaidia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar.

Bibi Bhawani amebainisha pia wajibu wa UNICEF katika kutilia-nguvu miradi ya maendeleo inayogusa sekta za mazingira, watu wenye ulemavu, usafi na usanifu wa taka ngumu (wastes management system) katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika msafara wake, Bibi Bhawani aliongozana na Mtaalamu na Mshauri wa Mambo ya Afya wa UNICEF Zanzibar, Bi Maryam Seif Hemed.


Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
10/11/2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.