Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Umoja wa UMAWA Zanzibar Ikulu.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi  akizungumza na Uongozi wa Jumuiya ya UMAWA Zanzibar, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Mussa Miraji Vuai akiwa na ujumbe wake
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongeza kwa Umoja wa Maaskari Wastaafu (UMAWA), kwa kujenga chombo hicho ambacho kinawaweka pamoja askari waastaafu.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Umoja wa Maaskari Wastaafu (UMAWA), Ikulu Zanzibar wakati walipofika kwa ajili ya kujitambulisha na kumjuulisha Rais nia na dhamira za Umoja huo.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana katika Umoja huo kwa kuendeleza miradi kadhaa ikwiemo ulinzi, mradi wa ulazaji wa gari,milango ya maduka na mradi wa kituo cha mafuta huku akipongeza lengo la Umoja huo la kuanzisha miradi mipya.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa kauli kwa uongozi huo kwamba kwa zile Taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na (UMAWA) atahakikisha zinalip madeni yake kama alivyoeleza azma hiyo  hivi karibuni katika hotuba yake ya mwaka mmoja tokea aingie madarakani kwa kupitia zile fedha za mkopo za UVIKO 19 baada ya kuzingatia uhakiki.

Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza haja kwa (UMAWA) kufuata taratibu na kanuni za Ushirika kama ulivyosajiliwa pamoja na kufuata Katiba yake ili kuondosha manunguniko kwa wanachama na hatimae kuiwezesha Serikali kuwauga mkono.

Pamoja na  hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kutengeneza kituo kikuu cha Mabasi cha aina yake hapa Zanzibar katika eneo la Kijangwani ambacho kitakuwa na maduka pamoja na huduma nyengine ambapo anamatumaini kwamba Umoja huo utafaidika na mradi huo iwapo wataridhia.

Rais Dk. Mwinyi, alieleza kwamba kwa vile kundi hilo ni kubwa na kwa vile Serikali imeamua kuviwezesha vikundi mbali mbali basi kikundi hicho nacho kwa vile kina sifa zote za kusaidiwa basi hilo linawezsekana.

Nao Umoja wa Maaskari Wastaafu (UMAWA), katika risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wake Kanali Mstaafu Miraji Mussa Vuai, ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na kupongeza kwa kutimiza mwaka mmoja madarani.

Uongozi huo ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuimarisha usalama, amani, utulivu na utengamano nchini wka kuondoa chuki na uhasama wa kisiasa na ukabila sambamba na kuvijenga vyombo vya ulinzi, usalama na sheria.

Aidha, uongozi huo ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kujenga na kusimamia nidhamu, uwajibikaji na heshima kazini inayoleta utawala bora bila ya muhali huku akisimamia haki za wananchi kwa nguvu zake zote.

Pia, watoa pongeza kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kupambana na udhalilishaji na ukatili wa kijinsia na watoto, kupiga vita dawa za kulevya, kuwajali na kuwanyanyua wazee na vijana,kuimarisha huduma za kijamii na kuleta maendeleo na wepesi wa maisha pamoja na kueleta maendeleo ya kiuchumi  kwa kuwawezesha wananchi kupunguza umasikini.

Uongozi huo ulieleza kwamba wamekusudia kwenda na wakati kwa kujipanga kwenda sambamba na Sera ya uchumi wa buluu inayohimiza ujenzi wa viwanda na uvuvi wa bahari kuu.

Hivyo, uongozi huo waliomba  kupatiwa nyenzo za uvuvi kama vile boti, mishipi, nyavu na zana nyengine ambazo zinaendana na hali ya uvuvi wa kisasa, kwani tayari wanao vijana mahiri ambao wanawaandaa kwa kazi hiyo.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa (UMAWA) inafuata mfumo wa kidemokrasia wa uongozi unaoheshimu utawala wa sheria, haki za binaadamu, amani, usawa, haki, heshima na uadilifu.

Uongozi huo ulieleza dhamira ya (UMAWA) ikiwa ni pamoja na kuimarisha hali ya Wastaafu kiuchumi na kimaisha ili kupunguza ukali wa maisha pamoja na kuendeleza shughuli za ulinzi  wa Taifa na kuwafunza uzalendo vijana wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, umoja huo ulieleza changamoto inazozikabili ikiwa ni pamoja na baadhi ya Taasisi kulimbuikiza madeni kwa huduma za ulinzi na usafi wanazotoa na kukwamisha shughuli zao.

Imetayarishwa na kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.