1.0 UTANGULIZI
Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais inasimamia maeneo manne ya utekelezaji ambayo ni uratibu na
udhibiti wa dawa za kulevya, usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi,
uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na uratibu wa juhudi za
kupambana na ukimwi.
Ofisi ya Makamu ya
Makamu wa Kwanza wa Rais, inasimamia taasisi zifuatazo:-
i)
Ofisi ya Faragha ya Mhe. Makamo
wa Kwanza wa Rais;
ii)
Idara
ya Mipango, Sera na Utafiti;
iii)
Idara
ya Uendeshaji na Utumishi;
iv)
Idara ya Mazingira;
v)
Baraza
la Taifa la Watu Wenye Ulemavu;
vi)
Tume
ya Kitaifa ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya;
vii)
Tume ya Ukimwi; na
viii)
Mamlaka ya Usimamizi wa
Mazingira.
2.0
UTEKELEZAJI
WA MAJUKUMU
2.1
Usimamizi
wa Mazingira na Mabadaliko ya Tabianchi
i.
Ofisi imeendelea
kudhibiti uchimbaji holela wa maliasili zisizorejesheka kwa kutenga maeneo
maalum kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa mchanga na kifusi. Jumla ya maeneo
5 ya mchanga na 2 ya kifusi yamekaguliwa na kupewa ruhusa za kimazingira za
kuchimbwa rasilimali hiyo. Maeneo ya mchanga ni Donge Kipange, Donge Mchangani,
Pangatupu, Zingwezingwe na Matetema. Maeneo ya kifusi ni Jendele na Fumba. Operesheni 35 za kusimamia maliasili
zisizorejesheka zimefanyika Unguja na Pemba kati ya operesheni 50 zilizopangwa
kufanyika.
ii. Ofisi imeendelea kudhibiti uingizaji, biashara
na matumizi ya mifuko ya plastiki. Jumla ya tani 2.8 zimekamatwa na kuteketezwa
na watu 104 wamefikishwa katika vyombo vya kisheria. Hali hii inaonyesha kuendelea kuwepo
kwa wafanyabiashara
ambao wamekuwa wanaingiza na kuuza mifuko hiyo.
iii. Katika
kusimamia matumizi mazuri ya fukwe na bahari, maeneo 23 (13 Unguja na 10 Pemba)
yamefuatiliwa, kusafishwa na baadhi yao kupandwa mikoko. Maeneo hayo ni
Kilimani, Kisakasaka, Kibele, Nyamazi, Nungwi, Kiwengwa, Matemwe, Michamvi,
Jambiani, Kihinani, Paje, Makunduchi na Chukwani kwa upande wa Unguja na Mkoani, Ole Kichanganazi,
Mtangani, Kangani, Wambaa, Tundaua, Vumawimbi, Makangale, Pangawatoro, na
Kichanjaani kwa Pemba.
iv. Katika
kuzuia kuendelea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda na ufukwe
wa pwani wa Msuka Magharibi uliopo Wilaya ya Micheweni Pemba, ukuta wenye urefu
wa mita 350 umejengwa ikiwa ni sehemu ya ukuta wa mita 500 unaokusudiwa
kujengwa. Aidha, misingi midogo ya
kupitisha maji ya mvua ndani ya ukuta huo wa mita 350 imekamilika.
v. Shughuli za kiuchumi zisizozingatia mazingira,
zimeendelea kufanyika katika mitaa na maeneo yetu hapa Zanzibar. Hali hii imepelekea kuwepo kwa kesi
32 (viwanda
vya matofali, magereji, maeneo ya kukata mbao na maeneo yanayofanya shughuli za
weldings) zinazohusiana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira kwenye makaazi ya watu.
vi. Ofisi imeandaa Muongozo wa Kimazingira wa
uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kusaga mawe, kifusi na utengenezaji wa
matofali. Kwa kushirikiana na Masheha,
tunakamilisha utaratibu wa jinsi gani shughuli hizo zifanyike bila ya kuwa na
athari za kimazingira katika maeneo ya kilimo, ufugaji, afya na makaazi kwa
ujumla.
vii. Ofisi
pia imeandaa
Muongozo wa Ufuatiliaji wa Kimazingira kwa ajili ya Hoteli za Kitalii. Muongozo
huo umelenga kuziwezesha Hoteli za kitalii kufanya ufuatiliaji binafsi katika
utunzaji wa mazingira. Kupitia
Muongozo huo Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, itaweza kuzifuatilia hoteli hizo ili kuimarisha
utunzaji wa mazingira na
kushajihisha utalii endelevu katika visiwa vya Zanzibar.
viii. Jumla
ya miradi ya kiuchumi na maendeleo 89 imefanyiwa
tathmini za kimazingira, kati ya miradi 99 iliyokuwa imepangwa. Tathmini hizo
zinahusu athari za kimazingira (miradi 40), ukaguzi wa kimazingira (miradi
tisa) na ripoti za kimazingira (miradi 40).
ix. Serikali
imenununa kifaa cha kukusanya taarifa za hali ya hewa ‘Automatic Weather
Station” na kufungwa katika eneo la Skuli ya Mohamed Juma Pindua; Mkoani Pemba
ili kuhakikisha taarifa za awali za hali ya hewa kwa ajili ya kuimarisha
uhimili wa mabadiliko ya tabianchi zinapatikana kwa wakati. Kifaa chengine kama hicho
kinategemewa kufungwa Makunduchi Unguja.
x.
Katika kuimarisha
usimamizi wa mazingira ya ukanda wa pwani ya Hifadhi ya Bahari ya Mkondo wa
Pemba (PECCA), Serikali imesafisha bwawa la maji machafu (Waste Water Treatment
Facility) lililopo eneo la Bandataka linapokea maji machafu yanayotoka katika
Shehia nne za Msingini, Chanjaani, Kichungwani na Madungu za Wilaya ya
Chakechake. Usafishaji huo ni katika hatua za awali katika kufanya marekebisho
ya mfumo wa bwawa hilo kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa usafishaji wa maji
machafu ya bwawa hilo.
2.2
Udhibiti
na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya
Zanzibar
inakadiriwa kuwa na vijana zaidi ya 10,000 ambao wamo katika matumizi ya dawa
za kulevya. Hadi mwishoni mwa mwaka 2020, watu ambao wako katika
nyumba za upataji nafuu ni 349. Katika kuimarisha
mapambano dhidi ya uingizaji, ulimaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za
kulevya, Serikali imetekeleza yafuatayo:-
i.
Rasimu ya sheria mpya ya
Udhibiti wa Dawa za Kulevya imeandaliwa na inatarajiwa kuwasilishwa katika
kikao cha Baraza la Wawakilishi cha mwezi wa Disemba 2021. Sheria hiyo mpya
itaiwezesha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya kuwa na nguvu kisheria za kupambana na dawa za
kulevya. Kupitia sheria hiyo, tutakuwa na maabara ya pamoja ambayo itahakikisha
kwamba tunabaini uhalifu mapema zaidi, pamoja kuwa na kikosi maalumu ambacho
kitakuwa na kazi ya kusimamia udhibiti wa uhalifu huu. Lengo letu pia ni
kufupisha muda wa usikilizaji wa kesi zinazohusiana na dawa za kulevya.
ii.
Katika kuimarisha udhibiti wa
dawa za kulevya zisirudi tena mitaani, jumla ya kilogram 94.573 zimeteketezwa.
Dawa hizo ni bangi, heroini, kokeni na mirungi.
Aidha, tumepitia upya muongozo wa uteketekezaji wa dawa hizo kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mrajis wa Mahakama Kuu.
Hatua kadhaa zinaendelea kuchukuliwa, zikiwemo za udhibiti wa ushahidi wa dawa
na usimamizi imara zaidi.
iii.
Katika kupunguza usambazaji na
matumizi ya dawa za kulevya, operesheni 52 zilifanyika katika mitaa
iliyobainika kuwa ni hatarishi zaidi kwa pindi hiki. Mitaa hiyo ni Kikwajuni,
Sogea, Kidongochekundu, Miembeni, Chuini, Jangombe, Migombani, Maeneo ya Mji
Mkongwe kwa Wilaya ya Mjini, Nungwi, Chakechake, Pujini, Wete, baadhi ya maeneo
ya Makunduchi (Kijini, Miwaleni na Mtegani) na maeneo yote yanayofanyika
shughuli za utalii. Doria za mara kwa mara zitaendelea kufanyika ili kupunguza
matumizi na biashara ya dawa za kulevya mitaani na kuimarisha mashirikiano
baina ya wananchi na Serikali katika kupunguza wimbi la usambazaji wa dawa za
kulevya.
iv.
Ofisi imebaini ongezeko la
matukio 52 (sawa na asilimia 15) ya ukamataji ambapo ujumla ya matukio 393
yameripotiwa kwa kipindi cha Januari – Septemba 2021 ikilinganishwa na matukio
341 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliyopita. Matukio hayo
yamepelekea kukamatwa kwa 8.5kg za heroine na kufunguliwa kwa kesi 168, sawa na
ongezeko la kesi 19 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo gramu 761 za
heroine zilikamatwa na kufunguliwa kesi 149. Aidha, jumla ya kilogramu 189.3 za
bangi zilikamatwa na kufunguliwa kwa kesi 220, sawa na ongezeko la kesi 5
ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo kilogramu 39 za bangi zilikamatwa na
kufunguliwa kesi 189. Vilevile, 180g za mirungi zilikamatwa na kufunguliwa kesi
5. Jumla ya gramu 191 za skanka zilikamatwa na kufunguliwa kesi 2.
v.
Ofisi, inakamilisha Ujenzi
wa Nyumba ya Kurekebisha Tabia iliyopo Kidimni kwa lengo la kuimarisha
upatikanaji wa huduma za afya kwa walioamua kuachana na dawa za kulevya na
kujenga uwezo wao wa kichumi kwa kuwapa nyenzo za elimu na mafunzo ya stadi za
maisha kabla ya kurudi kuungana na jamii katika shughuli za kiuchumi. Kwa
upande wa Pemba, imefanikiwa kupata eneo kwa ajili ya
ujenzi wa Kituo kama hiki katika kijiji cha Kiembe Raha, Kangagani. Uwepo wa vituo hivi utapunguza unyanyapaa na kuzidisha
kukubalika kwa vijana hao ambao wameamua kuachana na matumizi ya dawa za
kulevya.
vi.
Ofisi imefanikiwa kuanzisha
huduma ya simu ya bure (free line) kwa ajili ya kuripoti taarifa za uhalifu wa
dawa za kulevya. Kwa sasa, jamii inawasiliana na Tume
moja kwa moja kupitia namba ya bure ya 0774 33 33 00 au kupitia simu binafsi za
viongozi na watendaji wa Tume. Kupitia huduma hii,
Ofisi tayari imeshapokea taarifa 37 na inaendelea kuzifanyia kazi. Huduma hii
inawarahisishia wananchi kutoa taarifa zao juu ya uhalifu kwa usiri na kwa
haraka jambo ambalo limerejesha imani kwa wananchi katika kutoa taarifa.
vii.
Ofisi imeendesha mafunzo ya
ulinzi na usalama wa bandari (port security) kwa maafisa kutoka taasisi
mbalimbali zinahusika na ulinzi na usalama wa bandari zikiwemo TRA, KMKM, Jeshi
la Polisi, ZMA, ZAECA, Zimamoto na Uokozi, na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha ulinzi na ukaguzi wa abiria na mizigo
bandarini.
viii.
Jumla ya Asasi Zisizo za
Kiserikali 15 zinashirikiana na Ofisi yangu katika mapambano dhidi ya matumizi
na biashara ya dawa za kulevya na kutoa elimu kwa jamii.
2.3
Uratibu
wa masuala ya UKIMWI
Kufikia Juni 2021, Zanzibar inakadiriwa kuwa na watu
8,147 wanaoishi na virusi vya ukimwi ambapo wanawake ni 5,621 na wanaume ni
2,526. Katika kipindi cha mwaka mmoja, Ofisi imetekeleza yafuatayo:-
i.
Upimaji wa hiari umeongezeka
hususan kwa vijana ambapo jumla ya vijana 3,098 walipima VVU (1,577 wanaume na
1,521 wanawake) na mmoja tu kati yao aligundulika kuwa na maambukizo ya VVU.
Katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, vijana 833 tu ndio waliweza
kuhamasika kupima kwa hiyari ambapo wanaume ni 562 na wanawake ni 271.
ii.
Zanzibar bado inakabiliwa na
tatizo la unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU. Ofisi imeendelea kutoa elimu juu ya
athari za unyanyapaa kwa njia ya sanaa shirikishi katika shehia 9 za Wilaya ya
Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Aidha, tunaendelea kuhakikisha kuwa masuala
ya UKIMWI yanazingatiwa katika sekta zote kwa kuhamasisha Wizara, Taasisi za
Serikali na Binafsi pamoja na Mashirika ya Umma kuwa na programu za kupambana
na maradhi ya UKIMWI ili kudhibiti maambukizo mapya ya VVU kwa jamii yetu. Kwa
sasa, tunashirikiana na Asasi Zisizo Za Kiserikali 47 kwa ajili ya kuendelea na
kazi hizo.
iii.
Asilimia kubwa ya maambukizo
yapo kwa makundi maalum yakiwemo wanawake wanaofanya baishara ya miili yao
(12.1%), wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga (5.1%) na wanaume wanaofanya
mapenzi na wanaume wenzao (5%). Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya
Afya mwaka 2018, jumla ya wanawake 5,554 (4,854 unguja, 700 Pemba) wanakisiwa
kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao, wanaume 3,300 (3,000 Unguja na 300
Pemba) wanajihusisha na uhusiano wa jinsia moja na watu 2,600 (2,200 Unguja,
400 Pemba) wanakisiwa kutumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano.
Ofisi imeendelea na jitihada za kuyafikia makundi hayo kwa lengo la kuyapa
elimu na kupima maambukizo ya VVU kupitia programu za masafa (outreach) Unguja
na Pemba. Hadi kufikia Septemba 2021, jumla ya watu 10,378 wa makundi maalumu
wamefikiwa na 6,424 walikubali kupima VVU ambapo 69 waligundulika na maambukizo
ya VVU.
iv.
Kuanzia Julai 2020 hadi Juni
2021 jumla ya mama wajawazito 56,165 wamefanyiwa uchunguzi wa VVU ambapo kati
yao 104 (0.2%) waligundulika na VVU. Aidha watoto 381 waliozaliwa na mama
wajawazito walichunguzwa afya zao na 5 waligundulika na maambukizo ya VVU ikiwa
ni sawa na asilimia 1.3. Katika kudhibiti maambukizo ya VVU kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto kiwango cha maambukizo chini ya asilimia 5 kinachukuliwa kama
ni ishara ya ufanisi katika kuwalinda watoto na maambukizo kutoka kwa mama zao.
v.
Katika kuibua mbinu za
kudhibiti mazingira hatarishi yanayoweza kupelekea kuongezea kwa maambukizo ya
VVU, Ofisi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
Unguja na Pemba imeweka utaratibu kudhibiti upigaji wa ngoma na muziki;
kufungia kabisa utoaji wa vibali vya ngoma kwa baadhi ya maeneo; kufungia baa
na nyumba za kulala wageni na hoteli zinazoendeshwa kinyume na utaratibu au
zinazochochea tabia hatarishi; pamoja na kudhibiti bandari zisizorasmi kwa
kusimamia uingiaji wa wageni wasiokuwa na shughuli zinazoeleweka.
vi.
Elimu ya kuhamasisha mabadiliko
ya tabia katika jamii imeendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari, mikutano,
machapisho, vipeperushi na mitandao ya kijamii ya Instagram, youtube na
facebook.
2.4
Usimamizi
wa masuala ya Watu wenye Ulemavu
Zanzibar inakisiwa kuwa na idadi ya watu wenye Ulemavu
74,500. Hata hivyo, Mfumo wa kidigitali wa Baraza la Taifa la Watu wenye
Ulemavu (Jumuishi Database), umefanikiwa kusajili watu 8,488 wenye ulemavu
wakiwemo wanawake 4,043 na wanaume 4,445. Ili kuhakikisha kwamba haki na fusra
zinapatikana kwa Watu wenye Ulemavu, yafuatayo yametekelezwa:-
i.
Ofisi imeimarisha Jumuishi
Database kwa kuanzisha moduli ya usajili wa visaidizi (Asset Register)
vinavyotolewa kwa wenye ulemavu ili kuleta ufanisi katika utoaji wa visaidizi
hivyo na kuweka kumbukumbu sahihi za watu waliopatiwa visaidizi.
ii.
Jumla ya visaidizi 302 vya aina
mbali mbali vimetolewa, kati ya hivyo visaidizi 104 vimepelekwa Pemba ambavyo
wamepewa wanawake 56 na wanaume 48 na visaidizi 198 vimetolewa Unguja ambavyo
wamepatiwa wanawake 113 na wanaume 85. Visaidizi hivyo ni viti vya magurudumu
miwili 94, fimbo nyeupe 7 na kigari kimoja cha kisasa kinachotumia umeme.
iii.
Katika kupunguza wimbi la
vitendo vya unyanyasaji kwa Watu wenye Ulemavu, ofisi imepokea na kufuatilia
malalamiko 6 ya udhalilishaji Unguja na Pemba na kupelekea kesi 5 kufunguliwa
mahakamani ambapo 3 zinaendelea kusikilizwa, mtuhumiwa mmoja ametiwa hatiani na
2 zinaendelea na uchunguzi wa polisi.
iv.
Katika kuimarisha zaidi
usimamizi wa fursa na haki za watu wenye ulemavu, Ofisi imefanya mapitio ya
awali ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu (Haki na Fursa) No.9 2006 ambapo rasimu
yake inaendelea kupata maoni ya wadau. Ofisi inaamini kuwa marekebisho ya
sheria hii yataongeza ufanisi katika utoaji wa haki na fursa kwa Watu wenye
Ulemavu pamoja na kuimarisha ukondoishaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu
katika sekta mbalimbali zinazogusa maisha yao hali itakayoongeza kasi ya
kuwafanya waishi maisha bora zaidi.
v.
Ili kuhamasisha uelewa juu
ya haki na fursa za watu wenye ulemavu, Ofisi inashirikiana na Taasis Zisizo za
Kiserikali 10 kuhamasisha marekebisho ya miundombinu ya majengo hususan ya
Serikali kwa ajili ya kuweza kufikika kwa urahisi zaidi. Aidha, miundombinu ya
barabara ambayo inaendelea kurekebishwa hususan kuwekwa kwa njia za watembea
kwa miguu (walkways), kumesaidia kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye ulemavu
kupunguza vihatarishi vilivyokuwa vikitokea hapo awali katika barabara zetu.
2.5 Usikilizaji na utatuzi
wa kero na malalamiko ya Wananchi
i.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais, imeanzisha utaratibu wa kuwasikiliza wananchi mbalimbali na kupatiwa
ufumbuzi wa hoja zao. Ofisi imefanikisha kupatiwa suluhu ya mgogoro wa ardhi
kati ya wananchi wa Nungwi na Serikali ya Mkoa. Aidha, malalamiko ya wananchi
wa Kendwa kuhusu kuchukuliwa eneo la soko, yanaendelea kufanyiwa kazi. Ofisi
pia ilisimamia na hatimaye kuupatia suluhisho mgogoro baina ya mwekezaji wa
kiwanda cha kusaga kokoto na wakulima wa Shehia ya Mwambe, Pemba.
ii.
Katika kuweka mbele masuala
yenye maslahi kwa umma, Ofisi imefuatilia na kuyafanyia kazi malalamiko ya
wananchi dhidi ya wamiliki wa viwanda vinavyofanya shughuli zao katika maeneo
ya makaazi ya watu na kuleta kero kwa wananchi. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja
na kuzuia ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha waya za umeme cha kampuni ya ZANTEXAS
LTD katika maeneo ya Bweleo baada ya mjenzi kuthibitika kutokuwa na vibali vya
mazingira na ZIPA pamoja na kuleta athari za kiafya na kimazingira kwa
wanajamii wanaoishi jirani na kiwanda hicho.
iii.
Ili kuimarisha mawasiliano yake
na umma, Ofisi inatumia mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa na kupokea maoni
ya wananchi kupitia “facebook”, “instagram” na tovuti yenye anuani ya www.omkr.go.tz
.
iv.
Ofisi pia imeendelea kuyafanyia
kazi malalamiko mbalimbali yanayowasilishwa katika mfumo wa “Sema na Rais” ambapo
malalamiko 13 yamepokelewa, 6 kati ya hayo yamepatiwa ufumbuzi na 7 yanaendelea
kufanyiwa kazi.
v.
Ofisi imeandaa Mkataba wa
Huduma kwa Mteja (Customer Service Charter) ikiwa ni hatua ya kuimarisha mfumo
wa utoaji wa huduma za Ofisi.
vi.
Hatua za kupunguza athari za
Uviko 19 kwa watumishi wa umma zimeendelea kuchukuliwa kwa kuwajengea uelewa
watumishi 273 juu ya kujikinga na maambukizo ya Uviko 19 kwa lengo la kupunguza
na kukabiliana na maradhi hayo kwenye maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.
Aidha, vifaa vya matumizi kwa ajili ya kinga ikiwemo vitakasa mikono
(sanitizers) vimewekwa katika maeneo ya ofisi.
3.0
CHANGAMOTO
1. Ukosefu wa vifaa vya kisasa
vya utambuzi wa dawa za kulevya katika viwanja vya ndege na bandari Unguja na
Pemba.
2. Baadhi ya Watu
wenye Ulemavu kushindwa kupata matibabu kutokana na kutomudu gharama za
matibabu pamoja na uhaba wa dawa hospitalini kwa wenye ulemavu mchanganyiko.
3. Maradhi ya UKIMWI kuzoeleka na
kuonekana si tatizo tena katika jamii jambo linalopelekea kuongezeka kwa tabia
na mazingira hatarishi pamoja na
maambukizo ya VVU.
4. Umwagaji ovyo wa maji machafu
yanayotapishwa kwenye vyoo na makaro katika Manispaa ya Zanzibar.
5. Kuendelea kuwepo shughuli za
uchimbaji holela wa mchanga na maliasili nyengine zisizorejesheka
4.0
HITIMISHO
Ofisi itaendelea na jitihada za kusimamia
masuala ya usimaizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa dawa
za kulevya, mapambano dhidi ya UKIMWI na kulinda haki na fursa kwa watu Wenye
Ulemavu ili kuinua uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa
wananchi kupitia dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.
No comments:
Post a Comment