Habari za Punde

Hotuba ya Makamu wa Rais Dr Mpango alipofungua Viwanda vya Ushoni/Nguo na Viatu vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)


 




JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP ISDOR MPANGO, MAKAMU 

WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI

 WA UZINDUZI WA VIWANDA VYA IDARA MAALUM ZA SMZ 

(KIWANDA CHA USHONI NA KIWANDA CHA VIATU), 

MTONI KVZ-WILAYA YA MAGHARIBI A, UNGUJA



TAREHE 08 JANUARI, 2022

Mheshimiwa Massoud Ali Mohammed, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ;


Mheshimiwa Omar Said Shaaban, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar;


Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka Wizara Mbalimbali;


Mheshimiwa Idrissa Kitwana Mustafa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;


Ndugu Issa Mahfoudh, Katibu Mkuu Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ;


Makatibu Wakuu Mliopo;


Makamanda Wakuu wa Idara Maalum za SMZ;


Maafisa Kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama;


Viongozi wa Chama na Serikali Mliopo;


Viongozi wa Dini;


Wapiganaji Wote Mliohudhuria Hafla hii;


Mkurugenzi Mtendaji wa Viwanda;


Wageni Waalikwa;


Wanahabari;


Wananchi wote mliofika;


Mabibi na Mabwana;


ASALAAM ALEYKUM


Kwanza, naomba nianze kwa kuwatakiwa HERI YA MWAKA MPYA 2022. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia kuuona Mwaka Mpya tukiwa na afya njema na kwa kutuwezesha kushiriki katika tukio hili muhimu sana na la kihistoria la Uzinduzi wa Viwanda vya Ushoni/Nguo na Viatu vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) unaofanyika hapa Mtoni katika eneo la Kikosi cha Valantia Zanzibar (Mtoni-KVZ), Wilaya ya Magharibi A, Unguja.

Pili, napenda nichukukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendeleza utamaduni ulioanzishwa na Waasisi wetu wa kuadhimisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, sherehe ambayo inakwenda sambamba na matukio mbalimbali, likiwemo tukio hili kubwa la uzinduzi wa viwanda vya ushoni na viatu vya Zanzibar Quality Tailoring Ltd (ZQTL) na Zanzibar Leather and Shoe Factory (ZLSF).

Tatu, pamoja na salamu za pongezi, naomba kuwashukuru kwa mapokezi mazuri ya kindugu.  Aidha, ninawapongeza kwa maandalizi mazuri yanayoakisi utamaduni wa kuendeleza umoja na ushirikiano wa Watanzania. Huu ndio Muungano tunaoutarajia, muungano wa kupendana, kusaidiana na kutembeleana maana Watanzania sote ni wamoja. Ninawashukuru sana kwa kunialika kushiriki katika hafla hii adhimu.

Ndugu Viongozi, Wananchi na Wageni Waalikwa;

Serikali zetu mbili chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi zimedhamiria, pamoja na mambo mengine, kuimarisha sekta ya viwanda ili kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira.  

Kwa upande wa Tanzania Bara Serikali imedhamiria kujenga uchumi shindani wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati cha juu.  Dhamira hii inakwenda sawia na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukuza na kuvutia uwekezaji hususan katika viwanda ili kutimiza ile dhana ya Uchumi wa Buluu. Vilevile, azma hii ya kuendeleza viwanda, imeelezwa vizuri katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha Mwaka 2020-2025 (Ibara ya 156 na 157).


Napongeza sana Idara Maalum za SMZ kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuanzisha viwanda hivi vya ushoni na viatu. Wengi tunafahamu umuhimu wa bidhaa zinazozalishwa hapa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Baadhi ya faida tunazozipata ni pamoja na zifuatazo: Baada ya mahitaji ya chakula na malazi,  nguo na viatu ni hitaji la msingi la binadamu na ni kiashiria cha kuongezeka kwa kiwango cha maendeleo ya mwanadamu; Viwanda vya viatu/ushoni vinatumia nguvukazi zaidi kuliko mashine, hivyo hutoa fursa kubwa ya ajira hasa kwa vijana na wanawake; Viwanda vya ushoni/viatu vina uhusiano mkubwa na Sekta nyingine hususan Kilimo, Mifugo na Kemikali (hivyo kuwa na backward & forward linkages); Mauzo ya nguo/viatu nje ya nchi ni chanzo cha fedha za kigeni; Sehemu ya mapato ya viwanda vya viatu na nguo yanatumika kulipa kodi Serikalini kwa ajili ya maendeleo; Viatu vinatukinga na magonjwa, miiba, misumari, nyoka/wadudu wakali; na vinarahisisha au kunogesha michezo mbalimbali (mpira, riadha) na shughuli za utamaduni. Hivyo, nawapongeza sana kwa kupata fursa ya kunufaika na faida zote hizo.


Ndugu Viongozi, Wananchi na Wageni Waalikwa;


Nilipofika hapa nimetembelea viwanda vyote viwili, nimeona jinsi Serikali ilivyowekeza fedha nyingi katika majengo, mashine pamoja na malighafi. Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali kuwaomba muitunze miundombinu ya viwanda hivi kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. 


Jambo linalotia moyo na kunipa matumaini, ni kwamba mmeanza vizuri. Nimeelezwa hapa kuwa mmeanza kujitangaza kimataifa na kwamba hivi sasa mmeingizwa katika Jarida la Maonesho ya Kimataifa (EXPO). Ninawapongeza kwa hatua hii nzuri sana kwani itawasaidia kuingia katika masoko huru ya kikanda na kimataifa kupitia EAC, SADC, AfCFTA na AGOA. 


Viongozi wa Viwanda Vilivyozinduliwa;


Katika risala yenu mmeainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili. Kwa upande wa ombi lenu la wataalamu wa viwanda kutoka Tanzania Bara, hili linakubalika na ni hatua mojawapo ya kuimarisha Muungano wetu.  Hivyo, namwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ajipange kuleta wataalam kutoka Jeshi la Magereza Tanzania ili wasaidie kuongeza ujuzi, maarifa na utaalamu kwa wafanyakazi wa viwanda hivi.

Kuhusu suala la Mtaji, nawaelekeza viongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kutafuta fedha za kusaidia viwanda hivi. Nami napenda kutumia jukwaa hili kuzishawishi Benki na Taasisi nyingine za Kifedha kubuni na kuona uwezekano wa kutoa mikopo ya muda mrefu na ya gharama nafuu kwa viwanda vyetu hivi.  Hii ni fursa kwa benki zetu kukuza biashara zao. Binafsi, naamini kuwa Taasisi za Fedha zitaweka utaratibu mzuri wa kukopesha viwanda vyetu kwa gharama nafuu, vitaweza kabisa kuongeza uzalishaji, ajira na kufanya maisha ya Wazanzibari kuwa bora zaidi.   

Vilevile, napenda kuwaelekeza Viongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wakala kwa Maendeleo ya Viwanda Vidogo na vya Kati (SMIDA), watumie Balozi zetu nje ya nchi katika kupata teknolojia rafiki, mitaji na fursa ya kujifunza namna wenzetu wanavyosimamia viwanda vya namna hii na vingine vidogo na vya kati.  Mfano nchi ya China, asilimia 90 ya viwanda vyake ni viwanda vidogo na vya kati ambavyo kwa wastani vinachangia asilimia 60 kwenye Pato la Taifa (GDP) na asilimia 80 ya ajira. Kwa upande wa India, viwanda vidogo na vya kati vinachangia asilimia 95 ya Pato la Taifa na asilimia 45 ya mauzo nje. Hivyo, naamini tunaweza kujifunza mengi kutoka kwao na nchi nyingine kama hizi.  

Ndugu Viongozi, Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;


Naomba nihitimishe hotuba yangu kwa kuwapeni ushauri kidogo kama ifuatavyo: 


  1. Uongozi wa viwanda hivi uweke nguvu toka mwanzo kutafuta masoko na kwa kuzingatia mahitaji mahsusi ya wateja wa ndani (skuli, askari, migodi, michezo nk.) na masoko ya nje ya nchi kama Comoro. Aidha, hakikisheni  kuwa bidhaa mnazozalisha zinakidhi viwango na hata kushindana na zile zinazotoka nje. Pia ziwe za gharama nafuu ili wale ambao wanaoagiza bidhaa hizo kutoka nje hivi sasa, wavutiwe kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini;


  1. Wafanyakazi katika viwanda hivi nawasihi mjitume kufanya kazi kwa bidii. Tunzeni mashine hizi ipasavyo ili zidumu, ikiwa ni pamoja na kuzifanyia matengenezo kwa wakati; na


  1. Bado kuna tatizo la uchafuzi wa mazingira hapa nchini unaotokana na sababu mbalimbali. Pamoja na nia njema ya kuhimiza uanzishwaji wa viwanda, lakini lazima mzingatie pia taratibu za uhifadhi wa mazingira. Ni muhimu pia kuhakikisha viwanda hivi vinalinda mazingira mazuri ya Zanzibar.  Hii ni pamoja na kubuni matumizi mbadala ya mabaki ya viwanda (waste).  Aidha, ni muhimu sana kulinda maslahi, afya na usalama wa wafanyakazi wa viwanda hivi.  

Mwisho kabisa, ninawashukuru tena kwa mwaliko huu adhimu na sasa kwa heshima na taadhima natamka rasmi kuwa Viwanda vya Idara Maalum za SMZ vikijumuisha Kiwanda cha Ushoni na Kiwanda cha Viatu sasa vimezinduliwa rasmi.



MUNGU IBARIKI ZANZIBAR, MUNGU IBARIKI TANZANIA 


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.