HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI, KATIKA
KILELE CHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 58 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
TAREHE: 11 JANUARI, 2022
Assalamu Aleikum
Tunamshukuru
Mwenyezi Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa kutujaaliya uhai na afya njema na
kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukielekea katika kilele cha Maadhimisho ya
Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 12 mwaka 1964 yatakayofanyika
kesho tarehe 12 Januari, 2022 katika uwanja wa Amani.
Tunasherehekea
na kuadhimisha kutimia miaka 58, tangu wananchi wa Zanzibar tulipojikomboa na
kuondokana na unyonge wa kutawaliwa kwa miongo kadhaa. Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ni mwanzo wa safari ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar kwa kupata
mamlaka ya kujiamulia wenyewe mambo yetu ya msingi kwa mustakabali wa maisha
yetu.
Ni
dhahiri kuwa, mafanikio tuliyoyapata katika sekta mbali mbali kwa kipindi cha
miaka 58, yametokana na uongozi thabiti wa Waasisi wa Taifa letu na viongozi
wote wa awamu za Uongozi zilizotangulia. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunayalinda
na kuyadumisha Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Tanzania
tukijuwa kwamba hizi ni tunu muhimu tulizoachiwa na waasisi wetu.
Ndugu wananchi,
Tunapoadhimisha
siku ya Mapinduzi kila mwaka, tuna wajibu wa kuwakumbuka Waasisi wetu
wakiongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wetu wote
waliotangulia mbele ya haki, ambao walijitoa muhanga kwa ajili ya Taifa letu na
kuitumikia nchi yetu kwa moyo, ujasiri na uzalendo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu
awalaze pema peponi. Na wale walio hai, Mola awape afya njema na umri mrefu
tuendelee kunufaika kwa hekima na busara zao katika safari yetu ya maendeleo.
Haya
ni Maadhimisho ya pili kwangu tangu kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi. Mwaka jana nilieleza kwamba sote tuna kazi ya kutafsiri
kivitendo Malengo ya Mapinduzi kwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kustawisha
maisha ya Wazanzibari. Tumedhamiria kushirikiana kujenga uchumi mpya wa Zanzibar
kwa umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya
kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa.
Katika
shamra shamra za Maadhimisho haya ya miaka 58 ya Mapinduzi yenye kaulimbiu;” Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo Endelevu”,
jumla ya miradi 30 imefunguliwa na 13 imewekewa mawe ya msingi. Nawashukuru
sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika shughuli zilizopangwa ikiwa ni
ishara nzuri za kuunga mkono jitihada zetu za kuleta maendeleo.
Ndugu Wananchi,
Kwa
hakika, miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kipindi kirefu. Katika kipindi
hicho tumepata mafanikio mengi na vile vile tumekabiliana na changamoto kadhaa
katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.
Ni
utamaduni uliojengeka na tuliourithi kutoka kwa viongozi wa Awamu zilizopita, kutumia
sherehe za Mapinduzi kwa kutathmini na kutafakari mafanikio tuliyoyapata katika
kujenga nchi yetu pamoja na kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano. Vile vile, huwa tunatumia wakati huu kwa kuzitathmini
changamoto mbali mbali zilijitokeza kwa nyakati tofauti na kupanga mikakati ya kuzitafutia ufumbuzi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane itaendeleza utamaduni huu
muhimu kwa maendeleo yetu.
Kwa
msingi huo, ni vyema tukaendelea kutathmini maendeleo tuliyoyapata katika utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020, MKUZA Awamu ya 3, Dira ya Maendeleo ya
Zanzibar 2050 pamoja na Mipango ya maendeleo ya Kimataifa katika mwaka 2021
uliomalizika.
AMANI NA
UTULIVU
Ndugu
wananchi,
Moja ya mafanikio tuliyoyapata na tunayopaswa kujivunia ni
kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano. Kwa hakika hii ndiyo
misingi muhimu inayotuwezesha kuzidi kupiga hatua katika sekta zote za
maendeleo.
Natoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi wa kisiasa,
viongozi wa dini na asasi za kiraia, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama
vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja
na wananchi wote kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini kwa faida ya
kizazi cha sasa na baadae. Nawahakikishia wananchi na wageni wote
wanaotutembelea kwamba, nchi yetu ipo salama na kwamba Serikali zetu zote mbili
zitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulinda
amani, utulivu na maisha ya wananchi wote na mali zao.
UCHUMI
Ndugu
Wananchi,
Kuwepo kwa hali ya amani na ya utulivu kumetuwezesha
kutekeleza mipango yetu ya maendeleo, ingawa sio kwa kasi tuliyoitarajia
kutokana na kuwepo kwa janga la maradhi ya UVIKO- 19, ambalo limeathiri sana
hali ya kiuchumi ya mataifa yote duniani.
Katika mwaka 2021, kasi ya ukuaji wa uchumi iliimarika
ikilinganishwa na mwaka 2020, ambapo athari za Maradhi ya UVIKO, zilikuwa kubwa
zaidi. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 (Januari – Machi) uchumi wa Zanzibar
ulikuwa kwa wastani wa asilimia 2.2 ikilinganishwa na asilimia 1.8 ya kipindi
kama hicho kwa mwaka 2020. Kwa kipindi cha robo ya pili (Aprili – Juni) uchumi
umeendelea kuimarika zaidi na kufikia ukuaji wa wastani wa asilimia 6.5
ikilinganishwa na wastani wa asilimia 1.4 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020.
Katika robo ya tatu ya mwaka 2021, (Julai – Septemba) uchumi wetu ulikua kwa
asilimia 8.8 ikilinganishwa na asilimia 3.3 kwa kipindi kama hicho katika mwaka
2020. Ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji,
kuimarika sekta ya utalii pamoja na shughuli za biashara.
Juhudi kubwa zimefanywa na Serikali za kudhitibiti mfumuko
wa bei, ikiwa ni pamoja na kuweka bei elekezi kwa baadhi ya bidhaa muhimu. Kasi
ya mfumuko wa bei kwa kipindi cha Januari – Novemba 2021 ilifikia wastani wa
asilimia 1.7 ikilinganishwa na wastani wa
asilimia 3.4 kwa kipindi kama hicho cha mwaka 2020.
Ndugu
wananchi,
Kwa kipindi cha Januari- Novemba 2021, Serikali
ilikusanya jumla ya Shilingi billioni 745.1, sawa na ongezeko la asilimia 22
ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi bilioni 610.5 zilizokusanywa kwa
kipindi cha Januari – Novemba 2020. Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa
uchumi pamoja na kuanza kutumika kwa mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa
mapato iliyoanzishwa. Mifumo hiyo inaziunganisha taasisi mbali mbali za
Serikali, baina ya Taasisi za Serikali na Wafanyabiashara.
Vile vile, Serikali imefanya marekebisho ya sheria za
kanuni za kodi kwa lengo la kuondoa malalamiko ya kuwepo kwa utitiri wa kodi na
ada. Ni matumaini yangu kwamba, hatua hiyo itashajiisha ulipaji wa kodi kwa
hiari, kukuza ajira na kuongeza usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Vile vile, marekebisho ya sheria tuliyoyafanya yamesaidia
kutoa unafuu wa ushuru wa stempu kwa wafanyabiashara wadogo na wakati kwa kupunguza
viwango maalum kutoka Shilingi 200,000 hadi Shilingi 100,000, kutoka Shilingi
732,000 hadi Shilingi 200,000 pamoja na kupunguza kiwango cha ushuru wa stempu
kutoka asimilia 3 hadi asilimia 2 kwa mwaka.
UWEKEZAJI
Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Disemba 2021, Serikali
kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), imesajili jumla ya miradi 120 yenye mtaji wa
Dola za Kimarekani Milioni 787. Miradi hiyo inatarajiwa kutoa zaidi ya ajira
elfu 7. Tayari wawekezaji wamejitokeza katika visiwa 10 vilivyotangazwa
kukodishwa. Jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 261 zitawekezwa kwenye visiwa
hivyo ikiwa ni uwekezaji wenye hadhi ya juu. Aidha, ZIPA imefanikiwa kukusanya
Dola za Kimarekani Milioni 14 ikiwa ni malipo ya awali (Lease Acquisition Cost)
kutoka kwa wawekezaji hao.
Vile vile, huduma za uwekezaji zinazotolewa katika Kituo
cha Huduma kwa Wawekezaji (One Stop Centre) zimeimarishwa, ambapo hivi sasa Muwekezaji
hupatiwa cheti cha Uwekezaji ndani ya siku (3) na kibali cha kazi hupatikana
ndani ya siku moja. Kadhalika, huduma za Usajili wa Kampuni, usajili wa TIN,
VAT, kibali cha Kazi na Ukaazi, na ushauri wa kimazingira zinapatikana katika
kituo hicho.
Kwa lengo la kuimarisha uwekezaji nchini, Serikali imekamilisha
mapitio ya Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi katika Maeneo Huru ya Uchumi Fumba.
Hatua hiyo, imelenga kupanga matumizi sahihi ya ardhi na kuimarisha haiba ya
eneo hilo.
MATUMIZI YA FEDHA ZA MKOPO KUTOKA IMF NA MKAKATI MAALUM
WA KUONDOA MDORORO WA UCHUMI
Ndugu
wananchi,
Kama nilivyoeleza kwenye hotuba niliyoitoa kwenye sherehe
za maadhimisho ya kutimia mwaka mmoja tangu Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya
Nane ilipoingia madarakani, Serikali inaendelea kupanga na kutekeleza mikakati
mbali mbali ya kuimarisha uchumi. Tumefikia hatua nzuri hivi sasa ya kuanza
kutekeleza miradi tuliyoipanga kutekelezwa kwa kutumia fedha zilizotolewa na
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa njia ya mkopo kwa ajili ya kukabiliana
na athari za Ugonjwa wa Uviko 19.
Fedha hizo zenye thamani ya Shilingi bilioni 231 sawa na
(Dola za Kimarekani milioni 100) zitatumika katika Miradi ya Afya, Elimu,
Uwezeshaji, Maji na Nishati, kama nitakavyoelezea wakati nitakapozizungumzia
sekta hizo.
Aidha, Serikali iko katika mazungumzo ya kukopa fedha
nyengine zenye thamani kama hiyo Shilingi bilioni 230 kwa ajili ya kuziingiza
kwenye uchumi wetu kwa lengo la kuondoa mdororo wa uchumi uliopo. Mazungumzo na
taasisi za fedha kwa ajili ya utelezaji wa lengo hilo yanaendelea na tumefikia
hatua nzuri.
Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atuondolee janga la
maradhi ya UVIKO 19, ili malengo haya ya kuimarisha uchumi wetu yaweze
kutekelezeka kwa ufanisi na kuyafanya maisha ya wananchi kuwa bora zaidi.
UTALII
Ndugu Wananchi,
Serikali imeendeleza juhudi mbali mbali za kuimarisha
sekta ya utalii na kuitangaza Zanzibar. Serikali imeandaa na kurahisisha
ushiriki wa taasisi za Serikali na Kampuni binafsi katika maonesho, mikutano na
makongamano ndani na nje ya nchi. Juhudi
zetu hizo zimetuwezesha kuongeza idadi ya watalii kutoka 260,644 mwaka 2020
hadi kufikia 393,512 Mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 50.97.
Vile vile, zimetuwezesha kuongeza idadi ya Kampuni za Ndege
zinazofanya safari za kuja Zanzibar kutoka 27 hadi 34. Ndege hizo zilizoongezeka
zinakadiriwa kuleta zaidi ya watalii 50,000 kwa mwaka.
Katika kuhakikisha kwamba, wageni na watalii
wanaotutembelea wanakuwa katika mazingira yaliyo salama, Serikali imeanzisha Kikosi
maalum cha Askari wa Utalii ambacho nikimekizindua rasmi tarehe 19 Novemba,
2021.
Aidha, tumetekeleza mipango maalumu ya kuhifadhi na
kuendeleza Mji Mkongwe na majengo ya kihistoria ya daraja la kwanza ambayo ni
Beit al-Ajaib na Makumbusho ya Kasri la Wananchi yaliyopo Forodhani. Jengo la Beit
Al Ajaib ujenzi rasmi unatarajiwa kuanza mwezi Februari mwaka huu, 2022.
BIASHARA
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka 2021, mwenendo wa biashara ulikuwa ni wa
kuridhisha. Bidhaa za chakula, vifaa vya
ujenzi na nyengine muhimu kwa maisha ya Wananchi wa Zanzibar zimeweza kupatikana
katika hali ya kawaida, licha ya kuwepo kwa changamoto mbali mbali duniani
zilizosababishwa na janga la maradhi ya UVIKO 19.
Kuimarika kwa uzalishaji wa baadhi vya viwanda vya ndani
kumechangia sana upatikanaji wa uhakika wa baadhi ya bidhaa hizo. Upatikanaji
wa unga wa ngano umeimarika kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa
hiyo katika Kiwanda cha Zanzibar Milling, ambapo jumla ya tani 43,883 zilizalishwa
na tani 9,656.75 zimeagizwa kutoka nje ya Zanzibar kwa mwaka 2021. Vile vile,
jumla ya tani 7, 000 za Sukari zimezalishwa na Kiwanda cha Sukari Mahonda ambapo
jumla ya tani 28,704 ziliingizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wa biashara ya karafuu, Serikali imeendelea
kununua karafuu kutoka kwa wakulima kwa bei ya Shilingi 14,000 kwa kilo moja ya
karafuu kavu za daraja la kwanza, Shilingi 13,000 kwa daraja la pili na Shilingi
12,000 kwa karafuu za daraja la tatu. Jumla ya tani 7,645.61 zenye thamani ya Shilingi
bilioni 99.446 zilinunuliwa. Vile vile, jumla ya tani 1,658.75 za makonyo zenye
thamani ya Shilingi bilioni 2.487 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima.
Kwa upande wa mauzo, Serikali imeuza jumla ya tani 6,585
za karafuu zenye thamani ya Dola za Kimarekani 49,387,500. Vile vile, katika kipindi cha mwaka 2021
(Januari- Disemba), Serikali imelipa madeni ya muda mrefu ya wanunuzi wa
karafuu yenye thamani ya USD 2,894,550, sawa na Shilingi bilioni 6,657,465,000.
Kuhusu biashara ya zao la mwani, katika kipindi cha Januari
hadi Disemba 2021, Serikali imenunua kutoka kwa wakulima tani 43.95 za mwani kwa
gharama ya TZS 37,995,600.00; ambapo kwa mwani aina ya Cottonii Serikali
ililipa Shilingi 1,800 kwa kilo moja na bei ya Shilingi 700 kwa
kilo moja aina ya Spinosum.
VIWANDA
Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kufanya juhudi za kuhakikisha kwamba,
sekta ya viwanda inaimarika. Mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa
umeongezeka kutoka asilimia 18.1 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 19.6 mwaka
2021.
Katika mwaka 2021, jumla ya viwanda ya sita vimezinduliwa
na vitatu kuwekewa mawe ya msingi. Viwanda hivyo vinatarajia kutoa wastani wa
ajira zipatazo 400. Mafanikio haya yanaonesha njia katika juhudi zetu za
kuendeleza sekta ya viwanda hapa Zanzibar.
Serikali imeshawekeza jumla ya Shilingi bilioni 1.04 katika
eneo la Viwanda la Chamanangwe - Pemba
kwa kulipa fidia za wananchi wenye mashamba. Juhudi za kuweka miundombinu muhimu
katika eneo hilo zinaendelea.
UCHUMI
WA BULUU ( Uvuvi Mafuta na Gesi)
Ndugu
Wananchi,
Katika utekelezaji wa mpango mkakati wa uchumi wa buluu,
Serikali imeshakamilisha na kutunga sheria ya sera muhimu kwa maendeleo ya
uchumi huo. Serikali imeandaa mpango endelevu wenye thamani ya Shilingi bilioni
149 kwa ajili ya kuwawezesha wadau wa sekta ya Uchumi wa Buluu wakiwemo wavuvi
na wafugaji wa mazao ya baharini Zanzibar.
Awamu ya kwanza ya mpango huo tayari imeshatengewa jumla ya
Shilingi bilioni 36.5, ikiwa ni sehemu ya Fedha za Mkopo kwa ajili ya
kuimarisha uchumi baada ya kuathirika kutokana na maradhi ya UVIKO 19. Aidha,
taratibu za manunuzi ya jumla ya boti 577 za Uvuvi, boti 500 za wakulima wa
mwani na vifaa mbali mbali zimekamilika. Kazi inayoendelea hivi sasa ni
kuwapatia mafunzo wadau wa sekta ya Uvuvi ili waweze kuzitumia vizuri nyenzo
muhimu watakazopatiwa.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa kuwawezesha
wadau wa sekta ya Uvuvi utawanufaisha moja kwa moja jumla ya wananchi 26,000 mpango
huo utawajumuisha wavuvi 5,777, wakulima wa mwani 5,000, wafugaji wa samaki
400, wafugaji wa kaa 110, wafugaji wa majongoo bahari 160 na wastani wa
wajasiriamali wa madagaa wapatao 10,000. Aidha, faida za ujumla za mpango huo zinatarajiwa
kuwafikia wananchi wapatao 130,000.
MIUNDOMBINU
YA KIUCHUMI
Ndugu Wananchi,
Jitihada zimefanywa katika kuimarisha miundombinu ya
kiuchumi nchini. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali
ya Japan kupitia Shirika la maendeleo la Japan (JICA) inakamilisha ujenzi wa
diko na soko jipya la samaki katika eneo la Malindi kwa thamani ya Shilingi bilioni
24. Fedha hizo zimechangiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo imetoa
jumla ya Shilingi bilioni 3.6 na Serikali ya Japan imetoa Shilingi bilioni
21.4. Aidha, soko hilo la kisasa litawekewa miundombinu ya mitambo ya barafu na
litaweza kuhudumia wafanyabiashara na wananchi wasiopungua 6,500 kwa wakati
mmoja.
Vile
vile, Serikali imefanikiwa kupata jumla ya Dola za Marekani Milioni 8.8 kati ya
Dola za Kimarekeani milioni 58.8
zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo IFAD kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Fedha hizo
zitatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuweka miundombinu ya usarifu
wa samaki, kuendeleza zao la mwani, kujenga vituo viwili vya kutoa taaluma ya uvuvi
Unguja na Pemba pamoja na kununua meli za uvuvi nne (4) ili kuongeza uzalishaji
wa samaki nchini.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa sekta ya mafuta na gesi, muwekezaji amekamilisha
awamu ya kwanza ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya 2D na sasa yupo
katika mchakato wa kuendelea na utafutaji mafuta na gesi asili kwa njia ya 3D
katika maeneo ya bahari na nchi kavu katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Sambamba
na hatua hiyo, Mamlaka ya Usimamzi ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa mafuta
na gesi asilia (ZPRA) imeendelea na matayarisho ya ugawaji wa vitalu vipya kwa
ajili ya kufungua maeneo mapya ya uwekezaji.
Ndugu Wananchi,
Katika
kipindi cha mwaka 2021, Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuendeleza
miundombinu ya barabara. Ujenzi wa barabara ya Kinduni – Kichungwani – Kitope
(km 4) na barabara ya Sharifu msa- Mwanyanya- Bububu skuli (km 3.8) umefanywa
kwa kiwango cha lami. Aidha, barabara za Kwahajitumbo - Mlandege hadi Mbuyu
Taifa na barabara ya Hospitali ya Global – Mnazi mmoja zimefanyiwa matengenezo
makubwa.
Aidha,
Serikali imeingia mkataba na mkandarasi wa ujenzi wa barabara za ndani zenye
urefu wa km. 300 na mkataba wa ujenzi wa barabara ya Wete – Chake (km 22.1).
Vile vile, kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika kwa ajili ya ujenzi wa
barabara mbalimbali zikiwemo za Kitogani – Paje (km. 11), Mahonda – Donge –
Mkokotoni (km .13), Dunga – Kipilipini – Pongwe hadi Chwaka Spur (km.30) na
Kinyasini- Kiwengwa (km.13). Nyengine ni barabara ya Mshelishelini – Pwani
Mchangani (km.7.5), Muyuni- Nungwi (km.12) na Kizimkazi – Makunduchi (km. 13).
Hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya barabara hizo kutoka kwa washirika wa maendeleo
inaendelea.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu bandari na usafiri wa baharini, jitihada kubwa
zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha bandari zetu zinaongeza ufanisi na
mchango wake wa mapato katika uchumi. Serikali imeendeleza mpango Mkuu wa
Ujenzi wa Bandari jumuishi ya Mangapwani, ambao upo katika hatua ya mapitio kwa
ajili ya kuanza kwa mchakato wa kuwapata wawekezaji wa ujenzi wa bandari hiyo
kubwa ya kisasa. Aidha, ujenzi wa gati katika bandari ya Mkokotoni umekamilika.
Vile
vile, Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) imeruhusiwa tena kusajili meli
za Kimataifa baada ya kukosekana kwa muda kwa fursa hiyo ambayo inachangia
mapato ya Serikali na kutoa fursa kwa mabaharia wa Zanzibar kuweza kupata ajira
katika meli tunazozisajili.
Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha viwanja vya ndege na usafiri wa anga,
kazi ya ujenzi wa jengo jipya la abiria la Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani
Karume Terminal 3 imekamilika na Serikali imesaini mkataba na Kampuni ya DNATA
ya Dubai kwa ajili ya kuendesha uwanja huo.
Hatua
hii ya Serikali ina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora uwanjani
hapo zinazoendena na viwango vya Kimataifa, na kuongeza mapato Serikalini.
Kuhusu uwanja wa ndege wa Pemba, hatua ya kufanya upembuzi yakinifu
imekamilika. Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango tayari imeshatiliana
saini (MoU) na Kampuni ya PROPAV ya Hispania ambayo imeonesha nia ya kujenga
uwanja huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuimarisha huduma na kuwa na uhakika wa
nishati ya umeme, Serikali imeingia makubaliano na Benki ya Dunia kwa ajili ya
utekelezaji wa Mradi wa Uimarishaji na Uboreshaji wa Sekta ya Nishati Zanzibar.
Mradi huo utakaogharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 142, utajumuisha
ujenzi wa laini ya umeme yenye uwezo wa 132 KV. Vile vile, utahusisha miundombinu
ya kuzalisha umeme wa jua MW 18 ambapo maeneo ya vijiji vya Makunduchi, Paje na
Matemwe kwa Unguja na Mwambe na Micheweni kwa Pemba, yanapendekezwa kujengwa
vituo vya kuzalisha umeme huo. Utekelezaji wa mradi huo utakuwa na mchango
mkubwa katika kueneza huduma za umeme katika maeneo na vijiji ambavyo bado
havijafikiwa na huduma hiyo.
Kadhalika, Serikali imetenga jumla ya TZS bilioni 11.00
kati ya Fedha za Mkopo wa IMF kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zilizojitokeza kwenye sekta ya umeme. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya
kuwapunguzia wananchi gharama za uvutaji umeme. Wastani wa wateja elfu
thelathini (30,000) wanatarajiwa kufikiwa na kunufaika na mpango huo. Mpango
huu utajumuisha ujengaji wa miundombinu ya umeme mkubwa pamoja na ununuzi wa
vifaa mbali mbali vitakavyotumika katika kazi hizo. Katika mpango huu, muombaji wa umeme
atachangia Shilingi 200,000 badala ya Shilingi 600,000. Gharama zilizobaki,
zitafidiwa na Serikali. Lengo la uamuzi huu wa Serikali ni kuwapunguzia
wananchi wetu gharama hizo na kuweza kumudu huduma hiyo muhimu kwa maisha ya
kila siku.
ARDHI NA MAKAAZI
Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuimarisha matumizi bora ya ardhi na
utekelezaji wa mipango miji, Serikali imeyaorodhesha baadhi ya maeneo na
kuyaweka katika ardhi ya akiba kwa ajili ya matumizi maalum ya baadae. Hatua hiyo, imelenga kupunguza migogoro ya
ardhi, uvamizi wa maeneo, utunzaji wa mazingira na kuimarisha haiba ya miji na
vijiji vyetu.
Maeneo ambayo yameshapimwa kwa malengo hayo hasa makaazi
yapo Kibele kwa Unguja na Mfikiwa na Finya huko Pemba. Aidha, Serikali
imeshapima na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo na
vya kati; Dunga hekta 61 na Pangatupu hekta 135. Vile vile, katika kufanikisha
dhana ya Uchumi wa Buluu, Serikali tayari, imeshatenga eneo kwa ajili ya
bandari huko Kizimkazi lenye ukubwa wa hekta 24 na maeneo ya Viwanda vya
kusarifu samaki huko Fungurefu lenye ukubwa wa hekta 6.
Kwa lengo la kukabiliana na migogoro ya ardhi, katika
mwaka 2021, jumla ya migogoro ardhi 197 imepatiwa ufumbuzi na Mahakama ya Ardhi
na migogoro 301 imeshughulikiwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi. Aidha,
Serikali imeunda Tume maalum kwa ajili kushughulikia migogoro ya ardhi kwa
ufanisi zaidi. Kwa pamoja, tuipe Tume
hiyo ushirikiano unaohitajika ili iweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
KILIMO
Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya Kilimo
ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa na
serikali katika mwaka 2021, imefanikiwa kutekeleza kwa asilimia 85, mradi wa
ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 1,053 kwa mabonde 6 ya Unguja
na Pemba. Mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji ni Mkopo
kutoka EXIM Bank ya Korea na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2022.
Utekelezaji wa miradi huo umelenga kuongeza uzalishaji wa mpunga hapa Zanzibar
kwa kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.
Shughuli
za utafiti zinaendelea kutiliwa mkazo kwa lengo la kuchochea mapinduzi katika
sekta ya kilimo. Ni taarifa njema kuwa mtafiti wetu wa Taasisi ya Utafiti wa
kilimo Zanzibar, Ndugu Salum Faki Hamadi ametunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mwana
sayansi bora kwa uzalishaji wa mbegu za mpunga kutoka Shirika la Nguvu za
Atomiki lenye makao makuu yake Vienna- Austria. Tunampongeza kwa mafanikio hayo
na kuitangaza nchi yetu kimataifa.
HUDUMA ZA JAMII
Ndugu Wananchi,
Uimarishaji wa huduma za jamii zikiwemo elimu, afya na
maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nane kwa
kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na uongozi wa Awamu zilizotangulia katika
kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma hizo.
Kwenye
sekta ya elimu, katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa madawati katika skuli
zetu, Serikali imenunua jumla ya seti za viti na meza 35,610 kutoka nchini
China. Seti hizo zimeshawasili nchini na zinatarajiwa kusambazwa Unguja na
Pemba ili kutatua tatizo la uhaba wa vikalio katika Skuli za Sekondari za
Serikali. Kadhalika, Serikali imenunua
jumla ya kompyuta 1,364 na kuzisambaza katika vituo 22 vya ubunifu kwa lengo la
kushajiisha ufundishaji na matumizi ya TEHAMA.
Kwa lengo la kuzifanyia kazi changamoto ziliopo katika
sekta ya elimu, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 69.0, sawa na Dola
za Kimarekani bilioni 30 za mkopo shirika la IMF za UVIKO - 19.
Kwa kutumia fedha hizo, Serikali itakamilisha ujenzi
wa madarasa 425 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi. Shughuli hii itagharimu
jumla ya Shilingi bilioni 7.656. Vile vile, tumepanga kujenga madarasa mapya
706 katika Wilaya zote 11 Unguja na Pemba kwa ngazi ya Maandalizi, Msingi na
Sekondari. Madarasa haya yanajumuisha ujenzi wa madarasa mapya na yale ambayo
yatajengwa kupitia ujenzi wa skuli mpya 35 zikiwemo skuli 22 za maandalizi
(skuli 2 kwa kila Wilaya) na skuli 13 za Msingi na Sekondari Unguja na Pemba.
Skuli saba (7) kati ya hizi zitakuwa ni za ghorofa na
zitajengwa katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Mtopepo, Bweleo na Kwahani kwa
Unguja na Mwambe, Kwale na Makangale kwa Pemba. Aidha, skuli mbili zitajengwa
eneo la Jendele kwa Unguja na Chake chake kwa Pemba ambazo zitakuwa ni maalum
kwa ajili ya elimu mjumuisho. Maeneo mengine ya ujenzi wa skuli hizi ni
Mpendae, Kipapo, Pujini na Mgelema. Ujenzi huu utagharimu jumla ya Shilingi
bilioni 43.973.
Vile vile, tumeamua kuelekeza jumla Shilingi bilioni
6.871 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo 1,693 vya wanafunzi katika ngazi zote za
elimu. Kadhalika, jumla ya Shilingi bilioni 7.898 zitatumiwa kwa kufanya
ukarabati wa skuli 22. Skuli zitakazofanyiwa matengenezo makubwa ni skuli ya
Haile Sellasie, Chaani, Mlimani, Matemwe na Uzini kwa Unguja na Skuli ya Konde,
Chasasa na Kiwani Mauwani kwa upande wa Pemba.
Vile vile, tutanunua vikalio 8,000 (madawati ya
wanafunzi watatu) kwa ajili ya skuli za msingi vitakavyogharimu jumla ya Shilingi
bilioni 2. Pia, tutajenga jumla ya nyumba 10 za walimu katika maeneo ya visiwa
vidogo vidogo vikiwemo Tumbatu, Uzi, Njau, Kokota na Ng’ambwa. Ujenzi huo
utagharimu jumla ya Shilingi milioni 600.
Serikali itatumia wakandarasi wakubwa wa daraja la I,
II na III kuhakikisha ujenzi huu unakuwa wenye ubora mzuri. Taratibu za
kuwapata wakandarasi hao zinaendelea. Aidha, gharama zote za ujenzi kwa kila skuli
pamoja na michoro ya majengo
imekamilika. Serikali ina matengemeo makubwa ya mafanikio ya utekelezaji wa
miradi yote hii na hatimae kuweza kutoa elimu bora kwa watoto wetu ambao ndio
warithi wa Taifa letu. Katika hatua nyengine,
Serikali imeamua kurudisha tena darasa la saba kama zamani kwa kuzingatia maoni
ya wadau wengi wa elimu na wazazi hali ambayo itawapa fursa watoto wa Zanzibar
kupata elimu ya msingi kama ilivyokuwa zamani. Vile vile, hatua hiyo inalenga
kuwapa fursa nzuri Zaidi wanafunzi ya kujitayarisha na mitihani ya Taifa.
Kwa
lengo la kuimarisha uwezo wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha SUZA na kiwango cha
elimu kinachotolewa na chuo hicho, Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia
inaendelea na hatua za kuimarisha miundombinu ya Chuo hicho. Mradi huo utagharimu
jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 20.
Ndugu Wananchi,
Jitihada zimefanywa ili kuhakikisha hudumba za afya
zinatolewa katika Hosptali na vituo vya afya zimekuwa bora. Serikali
imeimarisha miundombinu ya afya. upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuongeza
idadi ya madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa sekta hiyo.
Kwa
lengo la kutatua Changamoto zinazoikabili sekta ya afya na kuweza kuimarisha
vyema sekta hii, tumetenga jumla ya Shilingi bilioni 69, zinazotokana na
Shilingi bilioni 230 za Mkopo wa IMF. Tumepanga kutumia kiwango hicho
kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali
mpya ya ngazi ya Mkoa katika Mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba.
Hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja na
itakuwa ya ghorofa tano.
Hospitali
hiyo itawekwa vifaa tiba vya kisasa, ikiwa ni pamoja, CTscan, MRi, Huduma za
Uchunguzi wa Maabara za Kisasa na huduma za afya za dharura. Aidha, itakuwa na
uwezo wa kutoa huduma mbali mbali za kibingwa pamoja na huduma za macho na
meno. Itakuwa na kliniki na wodi za kulaza wagonjwa mbali mbali kwa nia ya
kuongeza wigo wa kutoa huduma bora na kupunguza idadi ya watu wanaokwenda
Hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo nayo itaendelea kuboreshwa kupitia msaada wa
Benki ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu- (BADEA) ili ikidhi hadhi yake ya kuwa
Hospitali ya Rufaa. Ujenzi wa Hospitali mpya ya Lumumba utagharimu jumla ya Shilingi
bilioni 14. Ujenzi huo utaanza mara moja.
Sambamba
na hilo, Serikali imeamua kwa makusudi kutumia fedha hizo za IMF kuiboresha kwa
kuipatia vifaa vya kisasa na madaktari wataalamu wa kutosha Hospitali ya
Abdalla Mzee iliopo Mkoani Pemba na kuipandisha hadhi kuwa ni Hospitali ya Mkoa
ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini na Kisiwa cha Pemba
kwa ujumla.
Pamoja
na ujenzi huo, Serikali itajenga
hospitali 10 katika ngazi ya Wilaya zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kwa
wakati mmoja kila moja, pamoja na kujenga nyumba za wafanyakazi zitakazotosha
kuhudumia familia 16 kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.00. Hospitali hizo
zitajengwa katika Wilaya zote Unguja na Pemba isipokuwa kwa Wilaya ya Mkoani
ambapo itahudumiwa na Hospitali ya Mkoa. Hatua za ujenzi wa hospitali hizi
zimeshaanza katika maeneo mbali mbali ya Wilaya zote.
Hospitali
hizi zitatoa huduma za uchunguzi kwa kutumia vifaa vya kisasa (X-ray ya
kijiditali, Utrasound, na maabara za kisasa). Huduma zitakazopatikana katika
Hospitali hizi ni za ICU au wodi maalum kwa wagonjwa wanaohitajia uangalizi wa
karibu, magonjwa ya wanawake, upimaji wa mimba, uzazi wa kawaida na huduma za
upasuaji.
Ndugu Wananchi,
Kadhalika,
Serikali itanunua gari 12 za kubeba wagonjwa (ambulances). Gari hizo
zitasambazwa katika hospitali zote za Wilaya na mbili za Mkoa. Vile vile,
Serikali itanunua gari 5 za kusambazia dawa katika hospitali na vituo vya afya
Unguja na Pemba kutoka Bohari ya Dawa. Huduma hii itaondosha gharama
zinazotumika hivi sasa za kukodi gari za kampuni binafsi kwa kufanya kazi hiyo
na pia kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba vinavyosafirishwa.
Aidha,
Serikali itanunua mitambo ya kuchomea taka za Hospitali (Incinerators) kwa
hospitali zote za Wilaya na Mikoa. Aidha, kati ya mitambo hiyo, miwili itakuwa
ni yenye uwezo mkubwa wa kuchoma taka hatarishi nyingi kwa wakati mmoja na
itafungwa katika hospitali za Mikoa ili iweze kutoa huduma kwa hospitali za
karibu za Serikali na pia sekta binafsi.
Huduma
za damu salama zitaimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyoendana na
mahitaji husika ili kuweza kutoa huduma muda wote, hali ambayo kwa sasa,
kitengo cha damu salama hakina vifaa hivyo. Uwepo wa vifaa hivyo utaongeza
upatikanaji wa damu wa kuridhisha iliyopimwa na kuwa tayari kupewa wagonjwa
wanaohitaji.
Serikali
itanunua pia mitambo miwili katika Hospitali za Pangatupu na Abdalla Mzee ya
kuzalisha gesi tiba (oxygen), kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi
400 kwa siku, itakayotumika kwenye hospitali nyengine Unguja na Pemba
zitakazohitaji huduma hii.
Matarajio
yetu ni kwamba faida zitakazopatikana baada ya kukamilika miradi hii ni kuwa na
huduma za Afya zilizo bora karibu na wananchi. Vile vile, tutaweza kutekeleza
dhamira yetu ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya Zanzibar kwa
kufuata matibabu.
Ndugu Wananchi,
Katika
mwaka 202I, Serikali imeongeza kasi katika mapambano dhidi ya maradhi ya UVIKO
19. Huduma za chanjo dhidi ya maradhi
hayo zilianza kutolewa rasmi tarehe 17
Juni, 2021. Juhudi kubwa zimefanywa ya kusogeza vituo vinavyotoa huduma hiyo
karibu na wananchi na meneo ya utalii, ambapo hadi hivi sasa jumla ya vituo
vituo 41 vimeshafunguliwa; kati ya hivyo 29 viko Unguja na 12 viko Pemba. Kwa
mara nyengine, nawahimiza wananchi tuendelee kuchukua hadhari dhidi ya maradhi
ya UVIKO 19 ambayo bado yanaendelea kuwa ni tishio kwa maendeleo ya kiuchumi na
kijamii duniani kote.
Katika mwaka uliopita, jumla ya wafanyakazi wa kada mbali
mbali za afya 243 wamemaliza masomo na kurejea kazini. Aidha, jumla ya wafanyakazi 135 wameajiriwa
kwa njia ya mikataba. Wafanyakazi hawa watasaidia sana kupunguza tatizo la
uhaba wa wafanyakazi wa sekta ya afya na kuimarisha upatikanaji wa huduma za
afya kwa wananchi.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio yameendelea kupatikana nchini katika kupunguza
vifo vinavyotokana na uzazi kutokana na Serikali kuchukua hatua za kuziimarisha
huduma hizo. Vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua na kufikia 120 kwa kila
vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na vifo 166 kwa kila vizazi hai
100,000 kwa mwaka 2019. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia ya waja wazito
wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka 65.8 mwaka 2019 hadi
asilimia 66.3 mwaka 2020.
Ndugu Wananchi,
Upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni miongoni
mwa vipaumbele vya Serikali kwa
kuzingatia kuwa maji ni uhai. Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa
Uhuishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar.
Mradi
huu unagharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 92.18 ambazo ni mkopo kutoka
Benki ya Exim ya India. Mradi huu ambao utekelezaji wake ushaanza, unatarajiwa
kukamilika baada ya kipindi cha miezi 18 na utakuwa na jumla ya visima vya maji
64, matangi ya chini ya ardhi 7 na matangi ya juu 8. Mradi huu unatekelezwa
katika Wilaya tatu ambazo ni Magharibi ‘A’, Magharibi ‘B’na Wilaya ya Kati na
utawanufaisha wananchi wa Shehia 36.
Katika
kipindi hiki, Serikali kupitia ZAWA imefanikiwa kurudisha huduma ya maji safi
na salama katika maeneo 25 sawa na asilimia 89 ya malengo ya kufikia maeneo 28.
Hatua hii imefikiwa baada ya kununua na kufunga pampu mpya 50 katika visima
vilivyokuwa na hitilafu.
Kwa kutumia fedha za mkopo nafuu kutoka IMF, tumetenga
jumla ya Shilingi bilioni 34.2 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya maji. Fedha
hizo zitatumika kwa uchimbaji na uendelezaji
wa visima, ununuzi wa pampu na
vifaa pamoja na ujenzi na
ukarabati wa matangi katika sehemu mbali
mbali za Unguja na Pemba.
Wito
wangu wananchi waendelee kuwa na subira wakati jitihada za kukabiliana na
changamoto ya huduma ya maji safi na salama zinaendelea. Aidha, nawaomba
wananchi kuwapa ushirikiano wakandarasi wa miradi ya maji wakati huu ambao
shughuli mbali mbali zinaendelea kutekelezwa katika maeneo yenu ya
makaazi.
UTUMISHI NA UTAWALA BORA
Ndugu Wananchi,
Katika
kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imechukua hatua mbali mbali za kuimarisha utawala
bora. Tumeendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma na
kuweka mkazo katika nidhamu ya matumizi ya fedha ya Umma. Serikali imechukuwa
hatua dhidi ya watuhumiwa wa fedha za Serikali wasio zingatia matakwa ya
kisheria na taratibu.
Mamlaka
ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) imepokea tuhuma 289 za
makosa ya rushwa na uhujumu wa uchumi katika mwaka 2021. Majalada 29 ya kesi
hizo yamefikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashataka
(DDP) na kesi 4 zimetolewa maamuzi. Kazi ya uchunguzi kwa kesi nyengine
zilizobakia inaendelea. Vile vile, katika kipindi hiki, jumla ya
Shilingi 341,666,695 zinazohusiana na makosa mbali mbali zimeokolewa na
kurejeshwa Serikalini kutoka Mamlaka ya
kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar.
Katika
kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi ya muhimili wa Mahakama, Serikali
imekamilisha mradi wa jengo la Mahakama
Kuu lilioko Tunguu ambalo nimelizindua rasmi tarehe 9 Januari, 2022. Jengo hilo
ni kichocheo cha kuimarika kwa ubora na ufanisi wa kazi za Mahakama na litarahisisha
upatikanaji wa haki za kisheria kwa wananchi. Aidha, kwa lengo la kukabiliana na tatizo la
udhalilishaji Serikali imeanzisha Mahakama maalumu ya kusikiliza kesi zinazohusiana
na udhalilishaji.
HIFADHI YA JAMII NA
KUYAENDELEZA MAKUNDI MAALUM
Ndugu Wananchi,
Serikali imeendeleza utaratibu wa kuwapatia posho wazee wote waliofikia umri wa miaka 70.
Hadi kufikia mwezi Disemba 2021, jumla ya wazee 28,953 wamesajiliwa na kulipwa
pencheni. Aidha, kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) kwa upande
wa Zanzibar, katika kipindi cha mwaka uliomalizika, jumla ya Shilingi
4,541,763,530 zilizotolewa kwa walengwa Unguja na Pemba.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu hifadhi ya jamii dhidi ya udhalilishaji, kati ya
Januari hadi Septemba 2021, jumla ya matukio ya ukatili na udhalilishaji
kijinsia 928 yameripotiwa katika vyombo vya sheria. Idadi hiyo imepungua
ikilinganishwa na matukio 1,363 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka
2020. Nawasihi wananchi tuendelee kushirikiana katika kukomesha vitendo hivyo
vya aibu. Serikali itaendelea kuchukua hatua za ufuatiliaji wa kesi katika
vituo vya Polisi na Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka, kutoa ushauri nasaha kwa
waathirika na kuhakikisha Mahakama maalum iliyoanzishwa dhidi ya vitendo vya
udhalilishaji inafanya kazi kwa ufanisi.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya, tayari Baraza
la Wawakilishi limejadili na kupitisha mswada wa Sheria ya kuundwa kwa Mamlaka
yenye nguvu za kisheria za kuchunguza, kukamata, na kushtaki Mahakamani washukiwa
wote wa Dawa za kulevya Zanzibar. Hatua hii ina lengo la kuokoa maisha ya
vijana wetu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya kutokana na athari kubwa
tunazozipata ikizingatiwa kuwa vijana ndio tegemeo la nguvu kazi ya Taifa.
MAZINGIRA
Katika
hifadhi ya mazingira na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, hatua
mbali mbali zimechukuliwa na Serikali katika kukabiliana na hali hiyo. Serikali
imechukua hatua za kuhami maeneo yaliyoathiriwa kwa mmong’onyoko wa fukwe na
uingiaji wa maji ya chumvi katika maeneo ya kilimo na makaazi ya watu. Hivi
sasa, kazi ya ujenzi wa ukuta wenye urefu wa mita 500, inaendelea katika ufukwe
wa bahari ya Msuka Pemba. Vile vile, ujenzi wa tuta lenye urefu wa mita 450
unatarajiwa kuanza karibuni katika eneo la bonde la kilimo la Tovuni Mkoa wa
Kaskazini Pemba.
Ndugu Wananchi,
Katika kuzingatia haki za makundi maalum na kuwasaidia
kimaisha, Serikali imeendelea kusimamia haki na fursa za watu wenye Ulemavu
Zanzibar. Katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Mfuko wa uwezeshaji
wananchi Kiuchumi imeamua kuwajumuisha Watu wenye Ulemavu kuwa ni miongoni mwa
makundi yatakayonufaika na uwezeshaji huo. Aidha, katika kipindi cha mwaka
mmoja uliomalizika, jumla ya visaidizi 532 vya aina mbali mbali vimetolewa kwa
watu wenye ulemavu.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Ndugu Wananchi,
Uwezeshaji wa wananchi wa makundi mbali mbali kiuchumi, ni
miongoni mwa hatua za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2020 na ahadi
tulizozitoa katika kampeni za uchaguzi wa 2020. Serikali inafahamu kwamba
mahitaji ya wananchi ya kuwezeshwa kiuchumi ni makubwa zaidi ya uwezo wa Mfuko
wa Uwezeshaji tangu ulipoanzishwa.
Kupitia
Mfuko huo wa Uwezeshaji, jumla ya mikopo 1,080 yenye thamani ya Shilingi
bilioni 1.3 imetolea kwa mwaka uliopita.
Jumla ya ajira 11,045 zimezalishwa
katika shehia mbali mbali za Unguja na Pemba kupitia mikopo hiyo.
Kwa
lengo la kukuza ujasiriamali na kuondokana na tatizo kubwa la upatikanaji wa
mitaji liliopo, Serikali imeamua kutenga jumla ya Shilingi bilioni 81.8, kwa ajili ya kuwaweza wajasiriamali na
wafanyabiashara mbali mbali kwa kutumia fedha za Mkopo wa Shirika la Fedha la Dunia za UVIKO –19. Hatua
ya kwanza ya kuvihakiki vikundi vya ujasiriamali imeshafanyika, ambapo jumla
vikundi 3,494, Unguja na Pemba, vimehakikiwa. Katika uhakiki huo imebainika
kwamba jumla ya vikundi 2.907 vina sifa za kufaidika na mkopo huo na vikundi 587
vinahitaji kujengewa uwezo zaidi ili viweze kukopesheka. Zoezi la kufanya usajili na utoaji wa mafunzo
ni endelevu ili kutoa fursa kwa wananchi ambao wanataka kujishughulisha na
ujasiriamali.
Kwa
lengo la kuimairisha mazingira ya kufanya biashara, Serikali imewajengea soko la
muda wafanyabiashara wadogo wadogo katika eneo la kibanda Maiti ambapo jumla ya
watu 1,558 wataweza kuendesha shughuli zao katika eneo hilo.
Kadhalika,
Serikali inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa masoko mawili makubwa katika
eneo la Chuini kwa Nyanya na Jumbi ambapo mikataba ya miradi itasainiwa mwezi
huu. Vile vile, mradi wa ujenzi wa maduka ya kisasa kwa ajili ya wajasiriamali
wadogo katika eneo la Darajani utaanza baada ya kukamilika kwa hatua ya kusaini
mkataba na muwekezaji hivi karibuni. Tayari hatua za kulisafisha eneo hilo la
ujenzi zimeanza.
Kadhalika,Serikali
ilizindua mfumo wa usajili wa wajasiriamali tarehe 23 Septemba,2021 kwa lengo
la kuondoa usumbufu wa tozo za mara kwa mara na kuwatambua rasmi wajasiriamali
waliopo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Hadi kufikia tarehe 17 Disemba 2021 , jumla ya wajasiriamali 14,118 wameshasajiliwa na
kupatiwa vitambulisho vyao.
HABARI, MICHEZO NA UTAMADUNI
Ndugu Wananchi,
Katika sekta ya habari, Serikali kupitia Shirika la
Utangazaji Zanzibar (ZBC) imeendelea kuwapatia wasikilizaji na watazamaji, habari
za matukio mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa. Hatua hiyo imewawezesha
wananchi kufahamu na kupata uelewa wa masuala mbali mbali ya kijamii, kiuchumi,
kisiasa, michezo na burdani.
Katika kuendeleza shughuli za utamaduni na muziki, matamasha
mbali mbali ya utamaduni yameratibiwa kwa mafanikio yakiwemo Tamasha la 26 la
Utamaduni wa Mzanzibari, Tamasha la ZIFF, Sauti za Busara, Tamasha la Mwaka Kogwa
na Tamasha la Kimataifa la Muziki wa Taarab. Vile vile, Serikali kupitia Afisi
ya Haki miliki imeendelea kusimamia haki za wasanii ambapo kazi 1,028 za
wasanii zimesajiliwa. Pia, Mirabaha yenye thamani ya Shilingi Milioni 95.5
imekusanywa kutoka kwa watumiaji wa kazi zilizosajiliwa ambapo fedha hizo
zimegawiwa na kuwanufaisha wasanii 1,500.
Kwa
upande wa sekta ya Michezo, Serikali iliyaratibu kwa mafanikio mashindano ya
Kombe la Mapinduzi katika maadhimisho ya miaka 57. Kadhalika, katika
maadhimisho haya ya miaka 58, mashindano ya Kombe hilo yameandaliwa kwa mara
nyengine kwa ufadhili wa wadau wa michezo. Napenda niwapongeze wadhamini wa
Mashindano haya kwa kuonesha moyo wa uzalendo na kuhakikisha yanazidi kupata
msisimko na kuwa moja wapo wa matukio muhimu katika sherehe hizi muhimu kwa
Taifa.
Nalipongeza
Shirika Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kuendelea kuyaratibu Mashindano
yaliyopata umaarufu mkubwa ya Yamle Yamle na mashindano ya watoto ya Mapinduzi.
Mashindano hayo yana mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza vipaji.
Kadhalika, kwa mara nyengine tumeweza kufanya Bonanza la Kitaifa la kuhamasisha
kufanya mazoezi kwa mafanikio na kushirikisha wanamichezo zaidi ya elfu 7 kutoka vikundi mbali mbali vya
Zanzibar na Mikoa ya Tanzania Bara.
TUKIO
MAALUM LA SENSA
Ndugu Wananchi,
Moja kati mambo muhimu tuliyoyatekeleza katika mwaka 2021
ni matayarisho ya Sensa ya Watu na
Makaazi ya 2022. Hadi kufikia Disemba 2021, matayarisho hayo yalikuwa yamefikia
asilimia 65 ya kazi yote, ambapo zoezi la majaribio lilifanyika mwezi Septemba
2021 Katika maeneo 10 yaliyochaguliwa Unguja na Pemba na kazi ya uchambuzi
inaendelea. Natoa wito kwa wananchi
sote tuhakikishe tunashiriki zoezi hilo
wakati litakapofanyika kwa kutoa
taarifa sahihi ili tuweze kupanga na
kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa uhakika na ufanisi zaidi.
UHUSIANO NA DIPLOMASIA
Ndugu Wananchi,
Wakati nchi yetu inaadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi ya
mwaka 1964, tunafurahia kuendelea kuimarika kwa Muungano wetu wa Tanzania kwa
kufanikiwa kudumisha uhusiano wetu wa kihistoria na wa damu wa wananchi wa
pande hizi mbili za Jamhuri ya Muungano. Serikali zetu kwa jitihada kubwa
zimekuwa zikichukua hatua mbali mbali za kukabiliana na changamoto za Muungano.
Kadhalika,
katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Nane tumeimarisha uhusiano kwa kufanya mazungumzo na
wageni mbali mbali wakiwemo Mabalozi, Wawakilishi wa Serikali na Taasisi za
Kimataifa pamoja na watu mashuhuri, wanamichezo na wasanii. Wageni wote hawa
wamevutiwa na hali ya usalama iliopo na wameonesha utayari wao wa kushirikiana
na Zanzibar katika masuala mbali mbali ya maendeleo na ustawi wa jamii. Aidha,
tumeweza kupata ushirikiano mzuri miongoni mwa wana Diaspora kwa kuonesha
dhamira yao ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar. Serikali itaendelea kutoa
ushirikiano kwa Serikali za Mataifa mbali mbali, taasisi na wadau wote wa
maendeleo kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Ndugu Wananchi,
Namalizia risala yangu ya Maadhimisho ya miaka 58 Mapinduzi
kwa kutoa shukurani zangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama
Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuongoza vizuri, na kwa kunipa ushauri
katika masuala muhimu ya maendeleo yetu.
Vile vile, natoa shukurani kwa viongozi
wa ngazi zote, watendaji na watumishi wa Serikali pamoja na wananchi wote kwa
jitihada zenu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Ni vyema tuongeze kasi katika
kutekeleza wajibu wetu kwa misingi ya haki, uadilifu, mapenzi na mshikamano.
Sote tuamini kuwa mafanikio na maendeleo tunayoyadhamiria yanategemea mchango
wa kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Natoa
shukurani kwa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho inayoongozwa na Makamo wa
Pili wa Rais, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Wajumbe wake wote, Makamanda
na wapiganaji wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, watendaji mbali mbali wa
Serikali na Taasisi binafsi, waandishi wa habari, wanamichezo na wasanii kwa
mchango wa kila mmoja wao katika kufanikisha sherehe za maadhimisho ya miaka 58
ya Mapinduzi. Shukurani maalumu nazitoa kwa wananchi kwa kuonesha furaha na
kushiriki katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa katika maadhimisho haya.
Wito
wangu tuendelee kuwa pamoja katika siku ya kilele; kesho kwenye uwanja wa Amani
na ili tudhihirishe kuyathamini, kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Nakutakieni
nyote maadhimisho mema
MUNGU
IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU
IBARIKI TANZANIA
MUNGU
IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment