Habari za Punde

Mazoezi ni muhimu kuimarisha afya - Mhe Hemed

Makamu wa Pili wa Rais akizungumza na wanamazoezi wa vikundi kutoka Zoni “C” katika kiwanja cha Chakachua Donge Mtambile ambapo amewashauri wananchi kuendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha Afya zao
Mhe. Hemed akiwa pamoja na viongozi wengine wakitembea kwa miguu kutoka Donge mashimo ya mchanga kuelekea Donge Mtambile alipojumuika na wanamazoezi wa Zoni “C” leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mhe. Hemed akiwa pamoja na wanamazoezi kutoka vikundi vya Zoni “C” katika mazoezi ya viungo yaliofanyika Kiwanja cha Chakachua Donge Mtambile Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 Mhe. Hemed akiwa pamoja na wanamazoezi kutoka vikundi vya Zoni “C” katika mazoezi ya viungo yaliofanyika Kiwanja cha Chakachua Donge Mtambile Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewashauri wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kuimarisha Afya zao  badala ya kusubiriri ushauri kutoka kwa Daktari.

Mhe. Hemed alieleza hayo alipojumuika katika mazoezi ya pamoja na wanavikundi vya Zoni “C” yalioanzia Donge mashimo ya mchanga na kumalizia Donge Mtambile katika Kiwanja cha Chakachua Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amewataka wananchi kuendeleza mazoezi kupitia zoni zao kwa kuvitumia vikundi mbali mbali vilivyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha Afya zao na kuepukana na maradhi yasioambukiza.

Makamu wa Pili wa Rais alivitaka vikundi hivyo vya mazoezi kutumia fursa walionayo kuungana na serikali katika kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kwa  kuishauri jamii ili kujenga taifa imara lenye Afya.

Alisema madawa ya kulevya hayana faida katika jamii kwani yamekuwa chanzo cha kupoteza nguvu kazi ya taifa, hivyo jitihada za pamoja zinahitajika katika kupiga vita matumizi ya dawa hizo.

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili Rais amewataka wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa Ujumla kujitokeza kwa wingi muda utakapowadia katika zoezi la sensa ya watu na makaazi inayotarajiwa kuanza mwezi wa Agosti mwaka huu.

Alieleza kuwa, kushiriki katika zoezi hilo la sensa ya watu na makaazi kutaiwezesha serikali kuweza kupanga mipango yake ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake na taifa kwa kipindi cha miaka Kumi ijayo.

Aidha, Mhe. Hemed aliwakumbusha viongozi wa Chama cha mazoezi Zanzibar (ZABESA) kuwaandalia program maalum walimu wa vilabu vya mazoezi ili kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo yatakayosaidia kujenga mfumo wa pamoja kwa vilabu vyote.

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud alimuhakikishia Makamu wa Pili kuwa viongozi wa Mkoa wa Kaskazini wataendelea  kuviunga Mkono vikundi vya mazoezi vilivyomo katika Mkoa huu ili kutoa mskumo katika kuvilea na kuvikuza.

Kwa upande Mwenyekiti wa Chama cha mazoezi Zanzibar (ZABESA) Said Suleiman alisema ugonjwa wa UVIKO-19 upo Zanzibar hivyo amewataka wanamazoezi hao kujitokeza kupata chanjo kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kujikinga na maradhi hayo.

Kushiriki katika mazoezi hayo kwa Makamu wa Pili wa Rais ni muendelezo wa utaratibu aliojipangia katika kuvitembelea vikundi vilivyopo katika Zoni tofauti Unguja na Pemba.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.