Habari za Punde

SMZ Itaendelea Kuimarisha Huduma Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali Kuu ya Rufaa ya MnaziMmoja sambamba na kutekeleza malengo yaliyokuwepo ya kujenga hospitali ya Rufaa na kufundishia katika eneo la Binguni pamoja na hospitali za Wilaya katika Mikoa yote Unguja na Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  ameyasema hayo leo  katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuimarisha huduma za maji safi na salama pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti, katika Hospitali ya MnaziMmoja Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ujenzi wa hospitali ya Binguni, hospitali ya Mkoa katika eneo la Lumumba pamoja na hospitali za Wilaya utakuwa na mchango mkubwa katika kuipunguzia mzigo hospitali ya Mnazi Mmmoja.

Alisema kuwa hivi sasa wananchi wanalazimika kufuata huduma katika hospitali ya MnaziMmoja hata kwa huduma za tiba ambazo si za rufaa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa miradi yote ya ujenzi wa hospitali za Wilaya imeshaanza na inaendelea kwa kasi kwani dhamira ya Serikali ni kuona kwamba hospitali hizo zinakamilika na zinazinduliwa mwaka huu.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza mwekezaji mzalendo Mohamed Abdallah Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Cable TV kwa kujitolea kujenga jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya MnaziMmoja.

Aliongeza kuwa juhudi za mwekezaji mzalendo huyo zimechochea ari na hamasa ya wafanyabiashara wenzake na wananchi wengine kujityokeza kutoa misaada kwa jamii. “Umedhihirisha ukweli kwamba mjenga nchi ni mwananchi”,alisema Dk. Miwnyi.

Alisema kuwa hospitali hiyo ilijengwa zamani na mahitaji yake yalizingatia mahitaji halisi ya wananchi kwa wakati huo ambapo jengo la kuhifadhia maiti nalo lilikuwa na uwezo mdogo wa kuhifadhi maiti sita tu.

Kwa hivyo, alieleza kuwa msaada huo wa chumba cha kuhifadhi maiti chenye majokufu ya kuhifadhia maiti 20 unathamini sana.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Taasisi ya “Lady Fatema Foundation” kwa msaada wake wa huduma ya maji katika hospitali ya MnaziMmoja.

Alisema kuwa ni habari njema kuona kwamba kupitia mradi huo sasa hospitali ina uwezo wa kuzalisha lita 240,000 kwa siku moja ikiwa mahitaji ni lita 400,000 ambapo tayari umeshaipunguzia mzigo mkubwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), hasa pale miundombinu ya maji inapoharibika.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa taasisi hiyo kwa kuratibu na kutafuta wafadhili wa mradi huo na kuchimba visima, pia, aliipongeza Kampuni ya DEG ya Ujerumani kwa kuleta mitambo ya kuchuja chumvi na mitambo ya kuzalisha umeme wa jua.

Aidha, alitoa pongezi kwa Kampuni ya “Water kiosk Limited” kutoka Kenya kwa kukubali kuzifungamashine na mitambo mbali mbali ya mradi huo pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kuhakikisha inawawekea mazingira mazuri wafanyakazi wa sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara yao, maposho,maposho kwa wafanyakazi wanaoshughulikia huduma za maiti pamoja na ajira mpya ili kuongeza nguvu kazi hospitalini hapo.

Nae Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui alisema kuwa jengo hilo la kuhifadhia maiti lililozinduliwa hivi leo lina Majokofu ya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi maiti 20, pamoja na sehemu ya kuoshea maiti, sehemu ya kufanya uchunguzi wa maiti na vyumba vya kutoa huduma mbali mbali.

Alipongeza hatua na juhudi zilizochukuliwa na Taasisi ya “Lady Fatemah Charitable Trust” katika kuhakikisha inasaidia huduma ya maji kwa kuhakikisha inasaidia huduma hiyo kupitia mradi wa kuyatoa maji chumvi na kuyafanya kuwa maji safi na salama na kuweza kutumika katika shughuli zote muhimu za kibinaadamu.

Nao uongozi wa Ubalozi wa Ujerumani pamoja na wafadhili wa mradi huo wa maji safi na salama walimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba bado wana nia ya kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuendeleza miradi kadhaa huku Serikali ya Ujerumani ikieleza jinsi ilivyorejesha uhusiano wake na ushirikiano na Zanzibar na kuahidi kusaidia katika sekta ya maji, afya na michezo.

Wafanyakazi wa Hospitali hiyo ya Mnazi Mmoja nao kwa upande wao walieleza kufarajika kwao na hatua ya ujenzi wa chumba hicho cha kuhifashia maiti utasaidia kutatua changamoto zilizokuwepo hapo mwanzoni huku wakikiri kwamba sekta ya afya imepiga hatua.

Mwekezaji mzalendo Mohamed Abdallah Mohamed ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Cable TV alieleza mashirikiano aliyoyapata katika ujenzi wa mradi huo wa chumba cha kuhifadhia maiti na kuahidi kuendelea kujenga sehemu kwa ajili ya kubadilishia nguo kwa wafanyakazi wa chumba hicho cha kuhifadhia maiti.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.