Habari za Punde

ZAECA Kufanya Uchunguzi Upotevu wa Fedha za Makusanyo ya Mapato ZRB

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Salum Yussuf Ali ili kupisha uchunguzi wa kina wa upotevu wa  fedha za makusanyo ya mapato zilizopotea.

Rais Dk. Mwinyi amefikia maamuzi hayo leo wakati akiwa katika Ofisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini Zanzibar ambapo alipata fursa ya kuzungumza na uongozi wa Bodi ya Mapato, Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mapato  pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mamlaka hiyo.

Wakati huo huo, taarifa maalum iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said ilieleza utenguzi wa kiongozi huyo alioufanya Rais Dk. Mwinyi hivi leo Februari 17, 2022.

Pia, Rais Dk. Mwinyi akiwa katika Ofisi hizo za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), aliiagiza Bodi ya Mamlaka hiyo kumsimamisha kazi na kupisha ukaguzi wa kina wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, Hashim Kombo Haji kupisha ukaguzi wa kina wa maelekezo yake ya kuondoa taarifa za ukaguzi ambazo hatimae hazikupelekwa kwenye Bodi.

Sambamba na hayo, aliiagiza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na watendaji waliofanya uchunguzi pamoja na kushirikiana na vikosi vyote vya ulinzi na usalama watakavyovihitaji ili kujua fedha hizo zimeendea wapi.

Alisisistiza haja ya taarifa zote za kitengo cha Uchunguzi, kufanyiwa uchunguzi, zifuatiliwe ili kujua ripoti zilizotolewa na Kitengo hicho hatima yake ni kitu gani.

Pamoja na hayo, alitaka uchunguzi ufanywe wa lita za mafuta zenye gharama ya TZS Milioni 58, ushuri wake umelipwa wapi huku akiiagiza Bodi kutokana na unyeti wa Kitengo cha Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, kwamba kitendo hicho kijitegemee na kiripoti na kiwe chini ya Kamishna Mkuu na kisiripoti sehemu nyengine yeyote.

Alieleza kwamba ukaguzi maalum ufanyike kuchunguza utendaji wa mfumo wa ukusanyaji mapato ambao unaonekana unahujumiwa huku akitaka kufuatiliwa kwa akauti za benki ambazo mlipa kodi hulipa ada ya bandari ili kujua hizo fedha za Kampuni ya usafiri wa meli zimeingia katika akaunti gani.

Aliongeza kuwa hatua hizo ndizo zinazopelekea utendaji wa kazi ufanyike kwa kiwango cha chini na kusema kwamba hatomuonea mtu na ndio maana anataka kufanywe uchunguzi na ikithibitika kwamba waliotuhumiwa hawana kosa haki itatendeka na ikithibitika kwamba wana makosa lazima sheria ifuate mkondo wake.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa amepokea taarifa za kusikitisha kutoka kwa Kitengo cha Uchunguzi cha Bodi hiyo ambapo jukumu lake ni kufanya uchunguzi wa ulipaji wa kodi na kikishafanya uchunguzi ni jukumu la (ZRB) kufanya uchunguzi zaidi wa taarifa hiyo lakini kinachotokea ni kuzimwa kwa uchunguzi huo.

Akieleza miongoni mwa mifano ni uchunguzi uliofanywa wa moja ya Kampuni ya meli ya usafirishaji wa abiria ambapo kunaonesha tofauti ya ulipaji wa Bilioni 9.65 ambazo hazikulipwa ambapo uchunguzi ulifanyika na ikaonekana kwamba muhusika kalipa lakini fedha hazikuonekana.

Akiendelea na mifano hiyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Mkurugenzi wa Usajili, Ukaguzi na Upelelezi wa Walipa Kodi, Hashim Kombo Haji aliamuru ripoti hiyo iondolewe na isipelekwe katika uongozi lakini hata hivyo, ripoti hiyo ilipelekwa kwenye uongozi na kilichofuata ripoti haikupelekwa kwenye Bodi ambapo uongozi kwa kibali cha Kamishna Mkuu haikupeleka ripoti hiyo kwenye Bodi hiyo.

Aliongeza kwamba kuna Kampuni zilikwenda kukaguliwa na kuonekana kwamba hazikulipa Kodi kutoka mwaka 2016 hadi 2021 ambapo  ripoti ilipekekwa lakini Mkurugenzi huyo alitoa kauli na kusema mambo ya nyuma yaachwe na badala yake kuangaliwa zaidi taarifa za 2021.

Aidha, alisema kwamba kuna kampuni ya mafuta haikulipa Kodi ya lita zenye gharama ya TZS Milioni 58 huko Tanzania Bara ambapo uchunguzi ulifanywa na TRA na maelezo ya Kampuni hiyo ni kwamba fedha hizo haziwezi kulipwa Tanzania Bara kwa sababu mafuta hayo yameletwa Zanzibar lakini baada ya Rais kuagiza kufuatiliwa kama kweli fedha hizo zimelipwa Zanzibar ilionekana kwamba fedha hizo hazikulipwa sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Bodi ya Mapato ndio moyo wa Serikali kwani ufanisi wa chombo hicho ndio unaopelekea Serikali kuweza kutekeleza majukumu yake ya kimaendeleo na uendeshaji wake.

Alisema kuwa ufanisi ukiwa mzuri ndio Serikali inapoweza kutekeleza majukumu yake na kukiwa na tatizo katika chombo hicho Serikali nzima hufeli katika majukumu yake.

Mapema Rais Dk. Mwinyi alipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa ZRB lakini hata hivyo alisema kwamba changamoto zote za Bodi zilizoelezwa jukumu bado linabaki katika Mamlaka hiyo husika katika kuzitatua.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tatizo lilitokea wakati wa janga la UVIKO 19 ambapo dunia nzima iliathirika na tayari hivi sasa hali hiyo imeanza kutengamaa lakini hata hivyo, bado kumekuwepo kwa visingizio vya janga hilo katika ukusanyaji wa mapato.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.