Na Raya Hamad - OMKR
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dkt Omar D.
Shajak amesema kila mtumishi ni muhimu katika nafasi yake aliyoajiriwa hivyo ni
wajibu wake kuwajibika ipasavyo na kuwa muadilifu ili wakati wa kustaafu
ukifika awache alama nzuri ya utendaji
Dkt Shajak ameeleza hao wakati wa hafla ya kuwapongeza, kuwashukuru na
kuwaaga watumishi wawili wa kada ya ulinzi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
ambao ni Bw Ali Omar Ali na Bw Silima Khamis Machano iliyofanyika kwenye ukumbi
wa mkutano migombani
Amesema kuwa kila anaeajiriwa lazima afahamu kuwa ipo na siku ya
kustaafu hivyo ni vyema watendaji na watumishi wengine kuiga mema na mazuri
yaliyoachwa na wastaafu hao kwa kujifunza uadilifu, uwajibikaji katika
kutekeleza majukumu yao pamoja na kuwatakiwa afya njema
Akitoa wasia kwa wastaafu hao Dkt Shajak amewakumbusha kuwa kuvunjika
kwa koleo sio mwisho wa uhunzi bali maisha yaendelee wakati wakiwa uraiani
pamoja na kuthamini na kuitunza zawadi waliopewa ili iwe ni ushuhuda na
kumbukumbu nzuri ya maisha kutokana na mchango wao walioutoa katika Utumishi.
Akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais Bi Fatma Mohamed amesema mfanyakazi sehemu kubwa ya maisha yake yapo
kazini kwa wafanyakazi wenziwe hivyo subira, mashirikiano na upendo
waliouonesha wastaafu hao umepelekea kuwaaga wakiwa na furaha.
“Kwa kweli kuagana nao ni huzuni kubwa na majonzi kwetu, kwani tayari tulikuwa
tumejenga familia iliyokuwa na upendo na ushirikiano wa kutosha inayoitwa
Familia ya Ofisi wa Makamu wa Kwanza wa Rais”alitilia mkazo
Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi Ndg. Juma Ali Simai amesema utaratibu
wa kuwaaga wafanyakazi wastaafu ni takwa la kikanuni na kisheria ambapo kanuni
ya 132 inaelezea kuwaandaa kwa kuwapa mafunzo maalum kabla ya kustaafu na
kuwaaga wakati wa wastaafu pale inapobidi
Nae Bw Ali Omar Ali kwa niaba ya mwenzake ameushukuru uongozi wote wa
Ofisi pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuwalea hadi kufikia muda wa kustaafu,
amesema kwenye utendaji kazi lazima utangulize subira, kuithamini na
kupenda kazi yako na kutekeleza vyema
majukumu ndipo utaweza kufurahia maendeleo ya kazi yako.
No comments:
Post a Comment