Habari za Punde

Rais Dkt. Mwinyi: Kupitia wanahabari Kiswahili kitasambaa haraka duniani kote.

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Arusha

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali yake pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo mstari wa mbele kuendeleza jitihada za kuikuza lugha ya Kiswahili zilizofanywa na Serikali za Awamu zote zilizopita.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo Machi 18, 2022 wakati wa kufunga Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani ambalo limefanyika kwa siku tano kuanzia Machi 14-18, 2022 lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.

“Ikumbukwe kwamba Zanzibar inajenga uchumi wa buluu, lugha ni nyenzo muhimu sana katika kufanikisha jitihada zetu za kujenga uchumi huu. Visiwani Zanzibar Kiswahili kimeendelea kutuunganisha na kuwezesha shughuli za utawala, elimu, utamaduni na shughuli za kiuchumi, kwa niaba ya serikali yangu, tutakiendeleza zaidi Kiswahili na kuviwezesha vyuo vyetu vinavyotoa wataalamu wa Kiswahili na kuziwezesha taasisi za ukuzaji wa Kiswahili. “ amesema Rais Dkt. Mwinyi. 

Katika Kongamano hilo, Rais Dkt. Mwinyi amesema vyombo vya habari kupitia wanahabari vitasaidi kukisambaza Kiswahili kitasambaa haraka duniani kote ili malengo ya Serikali yaweze kufikiwa.

“Wanahabari wana uwezo wa kusambaza msamiati kwa haraka na kwa idadi kubwa ya watu kwa muda mfupi sana, tafuteni fursa na kujenga mazingira yatakayoifanya bidhaa hii iuzike kupitia tasnia hii ya habari. Nendeni mkatangaze na kuandika kwa Kiswahili” amesema Dkt. Mwinyi.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa “Mhe. Rais Samia Suluhu Hasani amefanya jitihada kubwa za kukiendeleza Kiswahili kabla na hata alipoingia madarakani kuwa Rais, amekuwa mtu anayekipenda Kiswahili, anayekitumia na anayekosoa matumizi mabaya pale anapogundua kuwa Kiswahili kimebanangwa

Hivyo, kutunukiwa kwake Nishani ya Juu kwa kuwa mstari wa mbele katika kupigania maendeleo ya lugha ya Kiswahili hapa nchini na Barani Afrika kwa ujumla ni udhihirisho kuwa yeye lugha ya Kiswahili katika Serikali yake imepewa kipaumbele kwa manufaa ya taifa ikizingatiwa hiyo ni lugha ya Taifa.

Kulingana na ukuaji wa sayansi na tenknolojia, matumizi ya Kiswahili katika vyombo mbalimbali vya habari yameendelea kuvuka mpaka wa Tanzania kwenda kimataifa kwa kupitia Idhaa za redio mbalimbali duniani, magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii kupitia intaneti hatua inayosaidia kuongeza idadi ya wazungumzaji katika maeneo mbalimbali  duniani.

Ili kufikia malengo mapana ya taifa katika kuendeleza lugha ya Kiswahili, Dkt. Mwinyi amesema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alieleza Mabaraza ya Kiswahili ya BAKITA na BAKIZA kuandaa mikakati mahsusi ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili Serikali iyawezeshe kwa kuyapatia wataalamu na itenge fedha katika bajeti kwa ajili ya miradi ya Kiswahili ya mabaraza hayo.

Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa katika kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wake Dkt. Philip Mpango madarakani, lugha ya Kiswahili kimepiga hatua kubwa sana ambapo Novemba, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza kuwa kila tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani wakati wa mkutano wa 41 wa nchi wanachama wa shirika hilo Novemba 23, 2021.

Hakika Kiswahili kimetambuliwa kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika na kupewa siku yake maalumu ya kuadhimishwa ambayo imepitishwa na kuwa lugha ya kazi ya Umoja wa Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja huo Februari 6, 2022 ambayo ni mafanikio makubwa kwa lugha yetu ya Kiswahili.

“Uamuzi wa Shirika la UNESCO kukipa hadhi Kiswahili kuwa na maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani si suala la bahati, ni suala lililofanyiwa kazi na waasisi wetu likiendelezwa na Serikali zetu na wadau wote wa Kiswahili hadi kufikia  heshima iliyonayo sasa lugha yetu ya Kiswahili” amesema Rais, Dkt. Mwinyi.

Akinukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa Waziri amesema Watanzania wana bahati kuwa na Lugha ya Kitaifa kama njia ya mawasiliano na kama chombo cha ukarabati wa kitamaduni na ukomboz ambayo inandelea kukua na kuenea duniani kote.

Kongamano hilo limehudhuriwa na washiriki takribani 200 likiongozwa na Kaulimbiu inasema, “Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani na Idhaa zilizopata fursa ya kuwasilisha uzoefu wao wa utangazaji kwa Kiswahili ni Radio China Kimataifa, Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), Redio Deutsche Welle (DW), Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Radio Maria, Clouds FM pamoja na WAPO Radio.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.