Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuhubirin Amani -Alhaj DkHussein Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi  amewasisitiza wananchi kuendelea kuhubiri amani.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika salamu zake alizozitoa mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Arafa, Mombasa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema kwamba wakati wote yeye atasimama katika upande wa kuhubiri amani na kueleza kwamba wananchi wote wanadhima ya kuhakikisha nchi inakuwa salama.  

Alieleza kwamba hivi karibuni kumejitokeza  baadhi ya watu kuanza kutoa maneno ya kuashiria kuvunja amani hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kukumbushana umuhimu wa kuhubiri amani.

Aliwataka wananchi wale wote wanaoguswa na maneno hayo kuwa na subira na kuwataka wale wanaoendeleza maneno hayo kutofanya hivyo kwani hawajengi na wala hawaitakii mema nchi hii.

Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza amani kama inavyoelezwa katika Qur-an kwenye na kunukuu sura ya 25 Suratul Furkaan aya ya 63 na kueleza kwamba yeye anachotaka ni salama.

Alisema kwamba yeye ataendelea kusimama upande wa kuhubiri amani na kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele ili amani iendelee kudumu nchini.  

Alisema kwamba umoja, mshikamano na amani katika nchi ni jambo la kuzungumzwa wakati wote kutokana na umuhimu wake katika maisha na maendeleo ya jamii.

“Mkisikia kuna vita katika nchi havianzi kwa bunduki huanza kwa maneno hivyo, ni wajibu wetu kama wananchi wanaoitakia mema nchi hii kuednelea kukumbushana kuhubiri amani na kuachana na maneno yenye kuweza kuvunja amani na kuleta machafuko”, alisisitiza Alhaj Dk. Mwinyi.

Alieleza kwamba watu wanaochafua nchi mara nyingi huwa makundi matatu ambayo ni wanasiasa, viongozi wa dini na waandishi wa habari na kueeleza kwamba machafuko ya nchi nyingi huanza kwa maneno na baadae kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kufarajika kwake kwa msikiti huo kulenga makundi yote ya jamii ili kuwasaidia na kutimiza mambo ambayo misikiti inafanya na kuomba kuwa sehemu ya kusaidia kituo hicho katika ujenzi huo.

Alilipokea ombi la ujenzi wa kituo hicho na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuwa wastahamilivu wakati ujenzi huo ukiendelea kutokana na usalama wao kwani eneo hilo litazungushwa mabati.

Alhaj Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Sheikh Ahmad Mohamed Al Falasi kwa misaada yake mbali mbali anayoitoa kwa jamii hapa Zanzibar.

Akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Imamu wa Masjid Arafa, Sheikh Ali Yunus alisisitiza haja ya kuendeleza umoja na mshikamano sambamba na kuwa na subira.

Sheikh Ali Yunus alisisitiza haja ya Waislamu kusaidiaana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan unaokuja kwani waumini wote hawako sawa.

Mapema Profesa Hamed Rashid Hikmany akitoa maombi kwa Rais kwa niaba ya msikiti huo alisema kuwa msikiti wao umekuwa ni kituo cha maendeleo ya shughuli za kidini na kijamii ambapo umekuwa ukilenga kwenye kuendeleza maisha ya watu, kiroho na kiuchumi.

Alisema kuwa dhamira yao ni kusaidia watu wanaozunguka msikiti huo ili waweze kuishi katika hali ya kuwa na kiwango cha juu cha imani ya kidini kama ilivyoanishwa kwenye Kur-an Tukufu na mfumo wa Mtume Muhammad (S.A.W) na kumuomba Rais ashirikiane nao katika kutimiza malengo yao ili wapate matunda endelevu.

Profesa Hikmany alieleza kwamba ili waweze kutimiza dhamira yao, msikiti huo umeasisi miradi mitatu muhimu inayowiana ajenda ya maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu.

Alisema kuwa msikiti huo una Umoja wa Vijana ambao moja ya mafanikio yao ni kufanya kazi nao ambao awali walikuwa wamejiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na kufanikiwa kuwabadilisha baadhi yao na kuwa wananchi wema wanaojitambua na wenye mwelekeo wa kidini.

Pia, alieleza kuwa msikiti huo una programu inayoendelea kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti ya kupima na kutoa ushauri nasaha kwa wanajamii kuhusu Ukimwi pamoja na kuchunguza maradhi ya sukari na shindikizo la damu ambapo pia, unafanya utafiti kwa wanawake, wasichana, wazee, mayatima, wajane na watu wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya familia, jamii na maendeleo ya taifa.

Alieleza azma ya msikiti huo kuanzisha kituo kitakachojumuisha harakati zote za kidini na kimaendeleo ya jamii, kikilenga masuala ya afya, vijana, wanawake na makundi yote yanayoweza kuathirika na kutennga eneo la ujenzi ambalo liko karibu na msikiti wao.

Akiwa msikiti hapo Alhaj Dk. Mwinyi aligawa misahafu kwa waumini wote waliofika msikiti hapo iliyotolewa na Ahmad Mohamed Al Falasy kutoka Falme za Kiarabu (UAE) ambaye nae aliungana na Alhaj Dk. Mwinyi kusali pamoja na waumini wa msikiti huo.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.