Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo katika Wilaya ya Mjini akieleza kufarijika kwake kwa namna ujenzi wa mireadi inavyoendelea vizuri  wakati akikagua miradi inayojengwa kwa fedha za  mkopo wa ahueni ya Uviko 19 katika Wilaya ya Mjini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa siku tatu kwa  Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha Mkandarasi anaejenga Hospital ya Mkoa wa Mjini iliyopo Lumumba analipwa fedha zake ili kuweza kuendelea na ujenzi wa Hospital hiyo.

Mhe. Hemed ametoa agizo hilo wakati akiendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa kwa fedha za Mkopo wa kukabiliana na athari za Uviko 19 katika Wilaya ya Mjini.

Amesema mkandarasi wa Hospital hiyo wanafanya kazi nzuri na ya kuridhisha na kueleza kutokufurahishwa kuona Mkandarasi huyo ameshafanya maombi ya fedha kwa mda mrefu bila ya kupatiwa fedha hizo wakati Serikali wameshatenga fedha zote za miradi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwa watendaji wa Wizara husika zilizonufaika na miradi hiyo kuhakikisha fedha zinapatikana kwa mujibu wa mikataba na kuwataka watendaji kuwa tayari kuendana na makubaliano ya Mikataba hiyo.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba watendaji wa Wizara mbali mbali kuacha tabia zisizo na msingi ambazo zinazorotesha utendaji katika Serikali akitolea mfano Fitina na  chuki walizonazo baadhi ya watendaji serikalini.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kusogeza huduma za Afya karibu na makazi ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wake.

Aidha mhe. Hemed ameeleza kuwa kuna watendaji ni wazito katika suala la malipo na kuwataka watendaji hao kubadilika ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Katika ziara hiyo makamu wa pili wa rais wa Zanzibar ametembelea ujenzi wa maeneo mbali mbali ya Wafanyabiashara wadogo wadogo pamoja na ujenzi wa skuli za ghorofa zilizopo  ndani ya Wilaya ya Mjini na kueleza kuwa ujenzi wa maeneo hayo kutapunguza changamoto zote za wafanya biashara na wanafunzi waliyopo nda ya walaya hio.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idriss Kitwana Mustafa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane kuona umuhimu wa kujenga Hospital ya kubwa ya Mkoa ambayo itapunguza changamoto ya Hospital katika Mkao huo pamoja na Maeneo mengine.

Aidha amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watasimamia ujenzi kwa mujibu wa maelekezo waliopewa na  Viongozi ili kumaliza changamoto zilizopo katika miradi hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mjini Mhe. Rashid Simai Msaraka ameeleza kuwa Ofisi ya Wilaya na ya Mkoa zimetoa mashirikiano ya kutosha kwa maeneo yanayojengwa maduka kwa ajili ya Wajasiriamali wadogo ambapo Wajasiriamali hao wameonesha kukubaliana na Maamuzi ya Serikali kuwawekea Maeneo rafiki.

ABDULRAHIM KHAMIS

OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR

12/04/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.