Habari za Punde

Safari ya Uchumi wa Buluu Imeaza Rasmin na Kazi Bado Itaendelea Dk.Hussein Mwinyi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk, Hussein Ali Mwinyi amesema  kuwa safari ya uchumi wa buluu imeanza rasmin na kazi bado itaendelea.

Hayo aliyasema huko katika bandari ya Shumba Mjini, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,  katika hafla ya ugawaji wa boti, mashine zilizotolewa na benki ya Amani pamoja na hundi ya TZS milioni 192 zilizotolewa na Benki ya CRDB kwa ushirika wa Uvuvi Tumbe ikiwa ni utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu sambamba na ahadi yake hiyo aliyoitoa.  

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba huu sio wakati tena wa wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi  kulalamikia ukosefu wa vifaa na mitaji kwani Serikali ikishirikiana na wadau mbali mbali imeshaanza kutekeleza azma ya kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutowa vifaa mbali mbali .

Alisema pamoja na vifaa hivyo vilivyotolewa leo tayari ziko Banki mbali mbali na mashirika mengine kama ZAFICO wameshatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitaji ambayo itatolewa kwa wavuvi ili kufikia safari ambayo inalengo la kuwabadilisha kimaisha.

Alitolea mfano wa mabenk hayo ikiwa ni pamoja Benki ya Amana  iliyotenga Bilion 10, Wizara ya Uchumi wa buluu Bilioni 36, Benki ya CRDB iliyotenga Billion 31 na Kampuni ya ZAFICO iliyotenga Bilioni 30.

“ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na wahisani mbali mbali yakiwemo Mabenki ili kuwajengea mbinu za maendeleo wananchi ikiwemo kuwapatia nyenzo mbali mbali za kujikwamuwa na Umasikini,”alisema.

Dk, Mwinyi alieleza kuwa zoezi hilo la utowaji wa boti na vifaa vyake ni miongoni mwa kufikia safari ya ajira laki tatu (300,000) zilizotangazwa na Serikali ambazo miongoni mwake zitatoka katika sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi.

Alieleza haja kwa Benki ambazo zimeshatenga fedha kwa ajili ya kuwaezesha wananchi kufanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wengine ambao bado hawajapatiwa vifaa vya uvuvi ili kuungana na wenzao katika safari hiyo ya kutumia raslimali zitokanazo na  bahari ili kufaidika na sera ya uchumi wa Buluu.

Rais Dk.  Mwinyi pia, alieleza azma ya Serikali kuirasimisha bandari hiyo ya Shumba Mjini ili iweze kufanya shughuli zake vizuri na kutoa faida zaidi kwa wananchi.

Alisema tayari imeweza kushirikiana na wahisani mbali mbali ikiwemo Mabenk ili katika kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo vifaa vya uvuvi ili kufikia uchumi wa buluu sambamba na kutowa mitaji kwa wafanyabiashara mbali mbali.

Aliwataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi wanapewa fedha kutoka benki ya CRDB na Benki ya Amana kwa ajili ya shughuli zao za uvuvi kama ilivyokusudiwa na kupangwa na Serikali.

Dk. Mwinyi aliuagiza uongozi wa Wizara ya Maji kuhakikisha kijiji cha Shumba ya mjini kinapata huduma ya maji safi na salama haraka iwezekanavyo na kipindi atakacho fika kijiji hapo hataki kusikia tena changamoto hiyo.

Aidha, alieleza kwamba hivi karibuni Wizara ya Fedha itaanza kuwalipa fidia wananchi ambao wamepisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya  barabara.

Alieleza hatua na ushirikiano atakaoutoa katika kuhakikisha ZAFICO inaimarika na kuweza kuvua na kununua samaki, kusarifu kwa kujenga viwanda ikiwa ni utekelezaji wa uchumi wa buluu.

Pia, kutatolewa boti 577 za uvuvi, kujengwa kwa viwanda vya kusarifu samaki na mwani huko kisiwani Pemba.

Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu Suleiman Masoud Makame alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

Akitowa maelezo Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZAFIKO Dk. Ameir Haidar Mshenga alieleza kuwa mashine 16 za boti ni kwa ajili ya wavuvi wa Shumba Mjini na boti ni kwa ajili ya wavuvI wa Makangale na Kengeja ikiwa ni mwendelezo wa kutimiza ahadi aliyoitoa Rais  tarehe 31.08.2022.

Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na mazungumzo waliyoyafanya kati yao na Benki ya Amana kupitia USAID ambayo hatimae yamezaa matunda, pamoja na kufanya mazungumzo na ZSSF ili kuwasajili wavuvi hao kwenye mfuko wa Hiari kwa lengo la kujiwekea hakiba ya hapo baadae.

Alisema kuwa ZAFICO imejipanga kutoa mashine za boti kwa wavuvi 650 na kuwapatia boti na mitego wavuvi 887 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa ambapo tayari imeshaanza mazungumzo ya kuwapatia mashine 20 za boti wavuvi wa Tumbe kupitia Mpango huo kwa kuwashirikisha benki ya Amana kupitia USAID na ZSSF.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Amana Abubakar Athman Ali alisema kuwa benki hiyo imechukuwa hatua hiyo ya kutoa vifaa hivyo ikiwa na azma ya kumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wa buluu.

Kwa upande wa wananchi wa Shumba ya mjini Mkoa wa Kaskazini Pemba walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza ahadi zake .

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi pia, aligawa sadaka ya futari kwa wenye mahitaji maalum huko  Micheweni pamoja na kuwagaiya wananchi wenye mahitaji maalum wakiwemo mayatima, wajane, walemavu huko ukumbi wa Jamhuri Wete ambapo alitoa shukurani kwa wale wote wanaoendelea kutoa sadaka zao kwa wananchi Unguja na Pemba.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.