Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana.
Asalam Alaykum
Awali ya yote
tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaaliya afya njema na kutuwezesha kuifikia
siku hii ya leo tarehe 28 April 2022, ambayo ni siku ya Maadhimisho ya Kimataifa
Usalama na Afya Kazini.
Ndugu Wananchi, Siku hii imewekwa maalum na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kuhamasisha ukingaji wa ajali na maradhi yatokanayo na sehemu za kazi, duniani kote. Nia hasa ni kwa Waajiri, Wafanyakazi na Serikali, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa usalama na afya na mabadiliko yanayotokea katika sehemu za kazi.
Ndugu Wananchi, kila mfanyakazi anatakiwa kuwa salama na mwenye afya njema kimwili na kiakili kwenye sehemu yake ya kazi kwa muda wote anapokuwepo kazini.
Hivyo mazingira ya kazi yanapokuwa hatarishi kwa usalama au afya humfanya mfanyakazi kuwa dhaifu. Hali hii inapotokea humuathiri mfanyakazi mwenyewe kiusalama na kiafya, na hushindwa kutoa huduma inavyotakiwa. Jamii inashauriwa kujenga utamaduni wa kutunza mazingira ya kazi yasiharibike na kuleta madhara.
Ndugu Wananchi, ukuwaji wa sayansi na teknolojia unaonekana kurahisisha uzalishaji na utoaji huduma kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwengine umeleta changamoto nyingi zinazohatarisha usalama na afya za wafanyakazi.
Changamoto
kubwa zaidi ni madhara ya kiafya yanayoweza kuonekena mara moja na yale yanayochukua
miaka mingi kujulikana.
Ndugu Wananchi, Kauli Mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Kazini kwa mwaka huu 2022 ni “Act Together to Build a Positive Safety and Health Culture” yaani “Tushiriki Pamoja Katika Kujenga Utamaduni Chanya wa Usalama na Afya kazini.
Kaulimbiu hii inalenga kuweka mikakati ya kuimarisha mifumo ya kitaifa ya usalama na afya (OSH) ili kujenga uimara wa kukabiliana na hatari zilizopo na zinazoweza kutokea kwa siku zijazo, kama ambavyo tulivyojifunza na kupata uzoefu kutokana na Janga la UVIKO-19.
Janga hili limegusa karibu kila sehemu ya ulimwengu wa kazi, kutoka hatari ya kuambukiza virusi katika maeneo ya kazi, hadi hatari za usalama na afya kazini ambazo zimeibuka kama matokeo ya hatua zilizochukuliwa za kupunguza kuenea kwa virusi.
Ndugu Wananchi,
Usalama na afya kazini
ni muhimu kimaadili, kisheria na kiuchumi. Taasisi zote
ziwe za umma au binafsi zina wajibu wa
kuhakikisha kwamba, wanawatunza wafanyakazi na mtu mwingine yeyote ambaye
anaweza kuathiriwa na sehemu zinazofanyiwa kazi, wanabaki salama wakati wote.
Wajibu wa kimaadili utahusisha ulinzi wa maisha na afya ya mfanyakazi. Hatua za kisheria za usimamizi wa Usalama na Afya pahali pa kazi ziimarishwe na zizingatie kuzuia, kuadhibu na kufidia ili kuhakikisha zinalinda usalama na afya ya mfanyakazi.
Hii itamsaidia kila muhusika kujua haki na wajibu
wake na taathira inayoweza kutokea pale taratibu za Usalama na Afya Kazini
zitakapokiukwa.
Ndugu Wananchi, Afisi ya Raisi, Kazi, Uchumi na Uwekezaji itaendelea kushirikiana na wadau wengine wanaohusika na masuala ya kazi Kimataifa na Kitaifa kuhakikisha matatizo yanayowakabili wafanyakazi kwenye sekta zote za kiuchumi yanapewa umuhimu unaostahiki.
Usimamizi wa masuala haya unaweza kufikiwa kwa kushirikiana pamoja kukuza utamaduni wa kuimarisha viwango vya usalama na afya kazini ili tupate mazingira ya kazi yaliyo salama, na kukuza ajira zenye staha.
Napenda kuchukua fursa hii, kuwaomba viongozi wa Taasisi zote za kazi za umma na binafsi, kushirikiana na Serikali kuweka mfumo mzuri wa utawala wa usalama na afya kazini. Tuweke rasilimali za kutosha katika mipango kazi yetu ili kukinga ajali na maradhi kwenye maeneo yetu ya kazi kwa kuzingatia kwamba muda mwingi wa wananchi wetu unatumika kazini.
Hivyo, tuwashirikishe wafanyakazi wenyewe katika kufanya tathmini za hatari zinazowakabili katika kazi zao, utoaji wa taarifa za hatari na katika kupanga hatua madhubuti za kukabiliana na hatari hizo, bila ya kuacha kuwapatia elimu ya kutosha juu ya namna bora ya kujikinga na ajali na maafa mbalimbali yanayoweza kutokea wakiwa kazini pamoja na athari za kiafya zinazohusishwa na kazi wanazozifanya.
Ndugu Wananchi, Afisi ya Raisi, Kazi, Uchumi na Uwekezaji inaungana na Jamii ya Kimataifa kuadhimisha siku hii inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 28 Aprili kwa kusimama imara kuendelea kupambana na ajira mbaya katika maeneo ambayo bado suala la kuwalinda wafanyakazi na hatari za usalama na afya, halipewi umuhimu kwa ustawi wa maisha yao, familia zao na nchi kwa jumla kiuchumi na kijamii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Utekelezaji wa Kauli mbiu ya mwaka huu, utaleta mafanikio na tija katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu, ambayo katika utekelezaji wake tunaweza kupata changamoto nyingi za kiusalama na kiafya.
Hivyo, kwa pamoja tunahitaji kuwa na mikakati na mipango madhubuti katika kujenga utamaduni wa usalama na afya kazini Kuepuka ajali na maradhi katika maeneo ya kazi, ikiwa ni sehemu ya kuengeza mapato kwa wafanyakazi, Waajiri na Serikali kwa jumla.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment