Habari za Punde

DC Wete apongeza Mradi wa VIUNGO kusaidia kuimarisha Uchumi wa Wakulima Zanzibar

 

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Dk. Hamad Omar Bakar akimkabidhi mkulima miche  wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa mbegu na Miche kwa wakulima wa wanufaika wa mradi huo Zanzibar.

Kitalu cha miche kilichopo Shehia ya Gando, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba ambacho ni moja ya vitalu vya mradi wa Viungo vinavyotumika kuzalisha mbegu kwaajili ya wakulima wanufaika wa mradi huo.

Na.Mwandishi Wetu Pemba.

Mkuu wa Wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba, Dkt. Hamad Omar Bakar amepongeza juhudi zinazofanywa na watekelezaji mradi wa VIUNGO, Zanzibar kwa kuwekeza katika uimarishaji wa kilimo cha Viungo, Mboga na Matunda kwa wananchi ili kufanya kilimo hicho kuwa msingi wa maendeleo ya wakulima na taifa.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa mbegu na Miche kwa wakulima wa wanufaika wa mradi huo Zanzibar ikiwa ni awamu ya pili ya zoezi hilo katika utekelezaji wa mradi unaolenga kukuza na kutanua fursa za kilimo cha Viungo, Mboga na Matunda visiwani Zanzibar.

Alisema kuwepo kwa mradi huo ni njia moja wapo ya kuwaondolea umasikini wananchi walio wengi kwa kujiingiza katika shughuli za uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuisaidia serikali kurahisisha utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu kwa haraka kutokana na wananchi kuondokana na hali duni za maisha.

“Serikali inaamini na inaunga mkono juhudi hizi ambazo mradi huu wa VIUNGO inazichukua kwa wakulima kwani shughuli hizi zinaongeza kasi ya utekelezaji wa sera ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Rais Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi ya kuwaodolea wananchi umasikini ili kufikia Uchumi wa Buluu,” alieleza.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza watekelezaji wa mradi huo kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa kila mkulima aliyepata mbegu na miche hizo ili ziwasaidie kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alieleza, "jambo la muhimu sasa ni kihakikisha tunafanya ufuatiliaji wa karibu wa miche na mbegu hizi ambazo tunazigawa kwa wakulima ili kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo hiki na kuhakikisha kuna uendelevu wa kile ambacho mradi umekianzisha ili kuisaidia serikali kupambana na tatizo la umasikini kwa wananchi.”

Mapema mkurugenzi wa Community Forests Pemba (CFP) ambao ni miongoni mwa taasisi watekelezaji wa mradi huo, Mbarouk Mussa, alieleza kuwa zoezi hilo ni awamu ya pili amapo awali mradi wa VIUNGO kwa upande wa Pemba uligawa miche 25,000 kwa wakulima na mbegu kilo 1,707 sawa na tani1.5 kwa wakulima 2500 wa kanda za Unguja na Pemba.

Alifahamisha, "Hivi sasa mradi umezalisha miche mbalimbali kwa Unguja na pemba, ambapo tuna vitalu vinne kutoka Pemba na vinne Unguja."

Aidha alieleza kuwa mradi huo pia unatarajia kusambaza mbegu mbalimbali kwa wakulima ikiwemo Tangawizi, minanasi, migomba na mbegu za mboga mboga kwa zaidi ya wakulima 1,000 ambapo kati yao walengwa wakuu ni wanawake kwaajili ya kuboresha shamba za nyumbani.

Nae meneja uendeshaji wa mradi kanda ya Pemba, Sharif Maalim, alisema kwa upande wa Pemba idadi ya miche 28,156 imezalishwa katika vitalu vinne ambapo miche hiyo ina thamani ya Tsh Milioni 28,156,000 ambayo inagaiwa kwa wakulima bure kwa lengo la kuongeza uzalishaji na wigo wa kilimo cha hicho Zanzibar.

Alitaja miche ambayo imezalishwa, “Miche hii ni miche ya Viungo kama vile Vanilla, Midalasini, na Mihiliki. Miche ya matunda kama vile Mishokishoki, Miembe, Mipension, na Miparachichi.

Aidha aliongeza kuwa mradi huo umelenga kusambaza miche hiyo kwa wakulima takribani 2,000 ambao watafikiwa katika zoezi la usambazaji huo wa awamu ya pili hadi kufikia mwisho wa mwezi wa June.

Mradi wa BIUNGO unatekelezwa kwa mashirikiano ya taasisi za Peoples Development Forums (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia mpango wa AGRI-CONNECT Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) ukiwa na lengo la kufungua fursa katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Viungo, Mboga na Matunda Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.