Habari za Punde

Elimu Inatafutwa na Mwenye Kuipata ana Wajibu wa Kuifundisha kwa Familia na Jamii yote bila ubakhili wala hiana.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Hauli ya miaka 100 ya Marehemu Alhabib Ahmad bin Abubakar bin Sumeyt, iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Unguja Jijini Zanzibar leo 15-5-2022.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa maisha ya Al Habib Ahmad Bin Sumait yanafundisha kwamba elimu inatafutwa na mwenye kuipata ana wajibu wa kuifundisha kwa familia na jamii yote bila ubakhili wala hiana.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo katika Hauli ya Alhabibi Ahmad Bin Sumait ya kutimiza miaka 100 tokea kufariki kwake, hafla iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Malindi Zanzibar, ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa kiserikali pamoja na viongozi wa dini kutoka nchi mbali mbali duniani.

Katika hotuba yake Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba marehemu alifundisha na kuendesha darsa mbali mbali ndani na nje ya nchi jambo ambalo liliiwezesha Zanzibar kuendelea kuwa chimbuko la Wanazuoni waliobobea na maarufu duniani.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba jambo jengine ambalo inapaswa kulizingatia katika maisha ya Alhabib Ahmad Bin Sumait ni jukumu la Wanazuoni na Wasomi la kuhakikisha kwamba wanaitumia elimu waliyonayo kwa kuandika vitabu.

Alisema kuwa Marehemu ameandika vitabu pamoja na maelezo ya tafsiri na ushereheshaji vitabu vya wanazuoni wakubwa ambapo elimu yake na kazi za uandishi alizokuwa akizifanya zilimuwezesha kutunukiwa zawadi na tunzo mbali mbali jambo ambalo lilimzidishia umaarufu duniani.

Alisema kuwa historia ya maisha ya Sheikh huyo, juhudi zake katika kutafuta na kufundisha elimu ya Kiislamu, michango yake katika shughuli za utawala na uongozi, akhlaki na mwenendo wake mambo yote haya yana mazingatio makubwa na muhimu kwa umma wa Kiislamu sio hapa Zanzibar tu bali duniani kote.

“Kwa mazingatio hayo nawahimiza Maulamaa, Mashekh na Wasomi wa elimu ya dini na sekula tulionao katika fani mbali mbali kuiga mfano huu....uandishi wa vitabu una mchango mkubwa katika kuendeleza elimu sambamba na kuipatia sifa nchi husika ya mwandishi”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa kazi ya kuitafsiri Qurani tukufu na kuiandika tafsiri hiyo iliyofanywa na Sheikh Abdullah Saleh al-Farsy na ile iliyofanywa na Sheikh Al-Barwani pamoja na masheikh wengine wa Zanzibar zina mchango mkubwa katika kufundisha Qur-an kwa Waislamu wanaozungumza Kiswahili duniani kote.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Zanzibar Masheikh, Wanazuoni pamoja na wageni wote waalikwa kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa kwa upande mwengine viongozi wanapaswa kujifunza kuongoza na kusimamia majukumu waliyokabidhiwa kwa misingi ya uadilifu na uwajibikaji kama alivyofanya Marehemu.

Aliongeza kuwa Marehemu aliaminika na akakabidhiwa nafasi ya Ukadhi mara mbili, kabla ya kwenda masomoni na baada ya kurudi ambapo mara ya mwisho alipokabidhiwa alidumu katika nafasi hiyo muhimu kwa takriban miaka 37.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Kamati za misikiti na viongozi na Maimamu wana wajibu wa kuandaa mipango imara kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa darsa na kuendeleza historia za misikiti na madrasa ziliopo.

Alisisitiza haja ya kuitangaza Zanzibar ili iwe ni mionghoni mwa vivutio kwa wageni Waislamu na wasiokuwa Waislamu huku akieleza haja ya kujifunza kwa Mataifa mengine kama vile Uturuki ambayo yameweza kuitumia vizuri historia ya Uislamu katika kukuza uchumi wa taifa hilo kupitia sekta ya utalii.

Akitoa historia ya Alhabib Sayyid Ahmad Bin Sumait Sheikh Mudh hir Mudh hir Kulatein, alisema kuwa Alhabib anatokana na ukoo wa Masharifu na wanachuoni wakubwa wa Hadhramout huko Yemen na kizazi chake kinatokana moja kwa moja na Mtume Muhammad (S.A.W), kupitia kwa Mjukuu wa Mtume Sayyidna Hussein bin Ali bin Abi Talib.

Kwa mujibu wa Sheikh huyo Alhabib amezaliwa tarehe 17 Januari 1861 A.D ambayo ni sawa na mwezi 5 Rajab 1277 A.H huko katika kisiwa cha Ngazija, Comoro na kuweza kujipatia elimu ya dini katika nchi mbali mbali duniani.

Akitoa neno la shukurani Sheikh Muhammed Bin Omar Sheikh (Judah), alimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa ukarimu wake mkubwa alioufanya kwa wageni hao tokea kuwasili nchini sambamba na kuunga mkono matayarisho yote ya Hauli hiyo.

Mapema Alhaj Dk. Mwinyi alizuru kaburi la Alhabib Sayyid Ahmad Bin Sumait na kumuombea dua akiwa pamoja na Masheik, Maulamaa na Makadhi Wakuu kutoka nchi mbali mbali za Afrika na nje ya bara la Afrika.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.