Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma.
Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia utekelezaji wa Mradi wa Bunda Climate Resilience and Adaptation Project katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara ili kukabiliana na athari za ukame.
Hayo yamesemwa leo Mei 18, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma.
Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa
Jimbo la Bunda Mhe. Boniphace Getere aliyetaka kujua ni lini Mradi wa
Mabadiliko ya tabianchi utawafikia wananchi wa Tarafa ya Chamriho wanaokabiliwa
na tatizo la ukame.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Khamis alisema mradi huo utakaosimamiwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) una thamani ya Dola za Kimarekani 1,400,000 na unafadhiliwa na Adaptation Fund.
Alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa wilayani humo katika maeneo ya Kata za Kasuguti, Namhura, Iramba, Neruma, Mahyolo, Igundu na Butimba kwa mujibu wa andiko lililoidhinishwa, hata hivyo Kata ya Chamriho kwa sasa iko nje ya mawanda (scope) ya mradi.
Aidha, naibu
waziri huyo alisema Ofisi
ya Makamu wa Rais itaendelea kutafuta fursa mbalimbali za miradi ya Mazingira
kwa kushirikiana na Halmashauri ya Bunda ili kukabiliana na changamoto iliyopo
katika Tarafa ya Chamriho.
Kwa upande mwingine Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa
Mohammed Issa alitaka kufahamu ni lini miradi ya mazingira itawafikiwa wananchi
wa jimbo hilo kisiwani Pemba ambao wameathirika na changamoto za kimazingira.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis
aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuvuta subira wakati Serikali ikifanya
mchakato wa kutekeleza miradi itayasaidia kuondosha changamoto hiyo.
Pamoja na hayo pia alitoa wito kwa wananchi
kujiepeusha na shughuli za kibinadamu ambazo si rafiki kwa mazingira hasa ukataji
miti ikiwemo mikoko hatua inayosababisha changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Alitoa wito kwa wabunge kuelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kuhifadhi
mazingira.
No comments:
Post a Comment