Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaandaa mwongozo wa Kitaifa wa Biashara ya Hewa Ukaa utakaotumiwa na wawekezaji, taasisi na watu binafsi wenye nia kufanya biashara hii hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo
wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo Mhe. Justine Nyamoga aliyetaka
kufahamu mpango wa Serikali wa kuomba fedha katika mifuko ya kupunguza hewa
ukaa duniani na kuwalipa wananchi wanaopanda na kutunza misitu katika Wilaya ya
Kilolo.
Dkt. Jafo alisema hewa ukaa ni moja ya
gesijoto ambazo mrundikano wake angani husababisha mabadiliko ya tabianchi na moja
ya njia zinazotumika kupunguza hewa hiyo chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa
wa Mabadiliko ya Tabianchi ni misitu ambayo hunyonya hewa ukaa wakati mimea
inapotengeneza chakula.
Alifafanua kuwa Mkataba huo hauna
Mfuko mahsusi wa kulipa miradi ya hifadhi ya misitu inayotekelezwa katika nchi
wanachama zinazoendelea kwa ajili ya kupunguza hewa ukaa. Badala yake, Mkataba
huo umeweka utaratibu wa kibiashara ambapo makampuni kutoka nchi zilizoendelea
ambazo zinawajibika chini ya Mkataba huo kupunguza gesijoto hulipa miradi ya
kupunguza hewa ukaa kupitia hifadhi ya misitu katika nchi zinazoendelea.
Alitolea mfano wa kampuni kutoka nchi
zilizoendelea ni Carbon Tanzania kutoka Uingereza ambayo hugharamia miradi ya
MKUHUMI katika mikoa ya Manyara na Katavi.
No comments:
Post a Comment