Habari za Punde

SIKU HIZI TUNACHEZA

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Jumamosi Mei 28, 2022 nilimtembelea mama mmoja wa Kigongo anayeitwa Mdala Anna, mwenye umri wa miaka kama 80, nilifika nyumbani kwake kununua mbolea ya samadi ambapo gunia moja linauzwa kati ya shilingi 1500/- na 2500/-.

Mama huyu aliniambia kuwa mbolea ipo lakini ngoja amngoje mtoto wake mkubwa anayefahamika kama Hamisi, kwa kuwa yeye ndiye mchungaji wake na yeye ndiye atayakepanga bei na kuchukua pesa hiyo.

Nilisubiri kwa muda, kwa kuwa mie kabwela uwezo wa kununua mbolea ya chumvi chumvi siyo kimo changu, kimo changu kiligota katika samadi tu. Natambua mbolea ya samadi haina kipimo kama ile ya chumvi chumvi, maana natakiwa kuiweka kwa uchache nisije kuyaunguza mazao yangu shambani.

Ndugu Hamsi alipofika nilimkabidhi pesa yake na kunipatia viloba vitatu, nikiwa pale napimiwa ile mbolea, Mdala Anna alisema kuwa bei ya mbolea lazima ipande kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan kapandisha mishahara.

Baba wafugaji kwenye eneo hilo tunapata tabu hasa eneo la kuchungia, tuliitwa katika kikao kimoja pale kijijini alikuwepo injinia mmoja wa barabara alikuwa mkali mno, akisema kuwa kama mtu anataka kufuga ng’ombe zake basi awe anachukua gari anazibeba na kuzipeleka malishoni na siyo kuzipitisha katikati ya barabara maana  zinafanya uharibifu.

Wafugaji wa Kijiji cha Chamwino Ikulu walicheka kweli, mtu ana ngombe saba hadi 15 azibebe katika gari kuzipeleka malishoni, ataweza? Alisema Mdala Anna. Tukiwa tunaongea na huku nikijaza viloba hivyo vya mbolea akapita mfugaji mwingine anaitwa Mwuha Manoza.

“Hata wale wenye makundi makubwa ya ng’ombe ambao walikuwa Chamiwno Ikulu walihamisha makundi yao, huko mashambani wanateseka mno kwa kukosa maji ya kunywa ng’ombe zao.”

Ndugu huyu akiwa na mkewe wakazungumzia na Mdala Anna juu ya TASAF mradi wa kuhudumia kaya masikini alafu wakaenda zao. Walipokuwa wanazungumza walitumia lugha ya Kigogo kwa hiyo sikuweza kuyabaini yote vizuri lakini neno TASAF nililisikia mara nyingi.

Walipoondoka ndugu hawa, nikamuuliza Mdala Anna kuwa na yeye ananufaika na TASAF? Alinijibu ndiyo. Nikasema wewe una ngombe 15, una ardhi ndani ya Chamwino ikulu kati ya Ekari 3-5, wewe siyo kaya masikini, wewe siyo fukara bali wewe tajiri.

Mdala Anna akacheka, akasema wewe mkonongo(mswahili) hautaki ninufaike na TASAF ehe? Nikamwambia hapana, kwenye mbolea umeshachukua zaidi ya shilingi 6000/, bado mahindi umevuna, nikasema wewe TASAF imeshakukomboa.

Moyoni nikasema kuwa wale wanaofanya tathimini ya kaya masikini tunapaswa tuwathimini.

Nikamwambia Mdala Anna, wewe una watoto kadhaa wa kike kwa wakiume na wajukuu kadhaa wa kike kwa wakiume, waambie kila mmoja akuletee debe la mahindi hapa utajaza ghala lako. Akacheka sana, akasema, baba hao watoto wote wananitegemea mimi, si unaona wajukuu walivyojaa kwangu? Nikamwambia mbona ninasikia umekula ng’ombe kadhaa za posa za mabinti zako na wajukuu?

“Baba, mahari tulitolewa sisi zamani, yaani mimi wakati ninaolewa ziliswagwa ng’ombe 25 kubwa kubwa, madume matano na majike 20. Zikaswaga hadi nyumbani kwa baba, zikapokelewa. Nikaogoshwa vizuri na ndipo nikakabidhiwa kwa mume wangu ambaye ndiye babu wa hawa wajukuu. Siku hizi hakuna mahari, mnacheza tu.”

Mara baada ya kuletwa ngombe hizo, kaka yangu mkubwa na yeye alikuwa anaoa, baba na kaka wakaziswaga kwenda kuolea kaka yangu, nyumbani zikabakia ngombe tano, zimezaliana hadi kesho kaka zangu wanazo.

Nilimaliza kujaza mbolea yangu katika viloba hivgo vitatu. Niliibeba mbolea yangu na kuondoka zangu kwangu, nilipofika niliangalia bei ya fahari mmoja katika minada ya mifugo ilikuwa kati ya shilingi 1,100,000/- na shilingi 1,500,000/-Kwa hesabu ya ngombe 25 ni zaidi ya shilingi milioni 37.5 ya Kitanzania, kwa mwezi Mei 2022.

Kwa bei ya dhahabu ya Tanzania sokoni kwa Mwezi  Mei 2022 gram moja ni shilingi 138,832/- ambapo kwa shilingi milioni 37,500,000/-na sawa  na  gram 270.1 ya dhahabu ambayo  ni sawa na robo kilo na ushehe wa dhahabu.

Mwanakwetu ninaiweka kalamu yangu chini kwa maswali mawili tu.

Je wewe ulioa au kuolewa kwa kiasi gani?

Je ni kweli siku hizi tunacheza?

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.