Habari za Punde

Wahindu Wanaoishi Zanzibar Kuendeleza Kufanyabiashara Kuitangaza Zanzibar Nje ya Nchi Ili Kuvutia Wawekezaji.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Jumuiya ya Wahindu Zanzibar walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 28-5-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wahindu wanaoishi Zanzibar  kuendelea kufanya biashara zao pamoja na kuitangaza Zanzibar nje ya nchi ili kuvutia Wawekezaji.   

Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana wa wanachama wa Jumuiya ya Wahindu Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitowa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ya kukutana na wananchi wa makundina Jumuiya  tofauti ili kubaini changamoto zinazowakabili.

Alisema Serikali inahitaji Wawekezaji wengi kuwekeza nchini kupitia sekta mbali mbali hususan  ya Uchumi wa Buluu, ikiwemo Utalii, Uvuvi, Kilimo cha Mwani, usafirishaji pamoja na biashara kupitia bahari, huku akiwahakikishia ulinzi wa rasilimali na mitaji yao Wawekezaji hao.

Dk. Mwinyi Serikali imeamuwa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuleta amani na mshikamano nchini, ikiwa ni hatua muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi.

“Kinachohitajika hivi sasa ni kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo”, alisema.

Alieleza kuwa matokeo chanya ya kimaendeleo yanayoonekana katikia maeneo mbali mbali ya nchi hivi sasa yanatokana na juhudi za Serikali na hivyo akatumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya ya ‘Hindu Community’ kwa kushirikiana vyema na Serikali.

Rais Dk. Mwinyi alisema serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na Jumuiya hiyo ili kuijenga nchi, kupitia Utumishi wa Umma na nyanja nyenginezo kama vile utoaji huduma na kusisitiza haja ya Jumuiya hiyo kuendelea kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

Alisema Serikali peke yake haina uwezo wa kumfikia kila mwananchi, hivyo michango ya Jumuiya mbali mbali inahitajika.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kupokea ombi la Jumuiya la kupatiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Ukumbi wa mikutano utakaowawezesha  wana Jumuiya  kufanya shughuli zao mbali mbali.

Alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kuipatia Jumuiya hiyo eneo kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi huo pamoja na kuipatia Jengo  katika eneo la Mji Mkongwe kwa ajili ya shughuli mbali mbali.

Aidha, alikubali mwaliko wa kushiriki katika shughuli maalum ya kidini iitwayo  ‘Ganpati Utsav’ inayotarajiwa kufanyika mwezi wa Augosti, mwaka huu.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alishukuru utayari wa mmoja wa mwanachama wa Jumuiya hiyo Joshi Deepak alieomba kupewa fursa ya kutengeneza Bustani ya kisasa katika eneo la  Mji ili kustawisha Mji, na kusema hilo ni jambo la faraja.

Nae, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahindu Zanzibar Arvind Chandulal Asawla, alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi kwa kusimamia vyema ukusanyaji na matumizi ya Fedha za Serikali pamoja na kuiletea nchi maendeleo ya haraka kupitia sekta mbali mbali.

Asawla,  alimpongeza Dk. Mwinyi kwa wito wake wa kuwahimiza wananchi kulipa kodi na kusema Jumuiya hiyo inaunga mkono juhudi hizo .

                

Mapema, Mama Joshi, kwa niaba ya Wanawake wa Jumuiya ya Wahindu Zanzibar  alimpongeza Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuunga mkono Jumuiya hiyo, hali inayowawezesha kuishi kwa amani.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.