Habari za Punde

Dkt.Mabula Aagiza Kukamilika vUthamini wa Fidia Mgodi wa Nyanzaga Sengerema.

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini Dkt Steven Kiruswa (wa pili kulia) na Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha (Kulia) wakati wa ziara ya kufuatilia program ya kuhamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza Juni 9, 2022.

Na Munir Shemweta, WANMM SENGEREMA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mthamini Mkuu wa Seriali Evelyne Mugasha kukamilisha uthaminishaji fidia kwenye eneo la mradi wa mgodi wa Nyanzaga uliopo Sengerema mkoani Mwanza baada ya wananchi wa eneo hilo kuelewa taratibu za fidia kwenye eneo hilo.


Mgodi wa Nyazaga unaoendeshwa kwa njia ya ubia kati ya kampuni ya OreCorp Tanzania Limited (84%) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (16%) upo kata ya Ngoma kwenye vijiji vya Sota na Nyabila na kufunguliwa kwake kunaenda sambamba na zoezi la utwaaji ardhi kwa eneo lote lililoidhinishwa katika leseni ya uchimbaji madini.

Changamoto katika programu ya kuwahamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga lenye ukubwa wa ekari 5,683 ni baadhi ya wananchi wachache kutoridhika na kiasi cha kiwango kilichoidhinishwa kutumika katika malipo ya fidia ya ardhi na uwepo wananchi wanaodai kuwa na haki ya umiliki maeneo ya milima.


Hata hivyo, tayari wananchi 1,236 sawa na asilimia 85 wamechukua form namba tatu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kulipwa fidia kupisha program ya kuanza kwa mradi wa mgodi wa Nyanzaga na wananchi 216 sawa na asilimia 15 bado hawajachukua form hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula aliyekwenda kutoa ufafanuzi wa fidia kwa watu wanaotakiwa kuhamishwa katika eneo la mgodi huo, kwa wale wananchi waliokubali kuchukua fomu namba tatu taratibu za kuthaminishwa zikamilishwa haraka ili waweze kulipwa fidia na wale wasiokuwa tayari taratibu za uthamini ziendelee mpaka watakaporidhika.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati wa kufuatilia zoezi la kuwahamisha watu na makazi kwenye mgodi wa Nyazaga Juni 9, 2022, Dkt Mabula alisema, uamuzi wa serikali katika kulipa fidia ya kuwahamisha wananchi wa   eneo hilo umezingatia taratibu zote za kisheria zikiwemo za kimataifa na hakuna mtu atakayepunjwa au kukopwa.


"Mthamini Mkuu wa Serikali alifanya mapitio na kuongeza kiasi cha malipo ya fidia ya ardhi hadi milioni mbili kwa ekari moja sambamba na aina ya miti nane kufanyiwa kazi kwa miti mitano kuongezwa katika jedwali, miti mitatu imeongezwa kiasi cha kiwango cha malipo" alisema Dkt Mabula.


Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Dkt. Steven Kiruswa katika ziara hiyo aliwaeleza wananchi wa kijiji cha Sota kuwa, tamko la sera ya ardhi linaeleza wazi kuwa maeneo ya milima hayapaswi kumilikiwa na mtu binafsi na zaidi ya sera maeneo hayo yanapaswa kulindwa hivyo ni maeneo ya umma.

"Kama kuna mtu yeyote anamiliki mlima na mwenye hati tutakuwa tayari kumlipa, maana sera inaeleza wazi kuwa maeneo ya milima hayapaswi kumilikiwa na mtu ni maeneo nyeti" alisema Waziri Dkt Mabula.


Aliwatahadharisha wananchi kuhusu maendelezo kwenye eneo la mradi maarufu kama TEGESHA kwa lengo la kutaka kulipwa fidia huku kukiwa na tarehe ya mwisho ya katazo la kufanya maendelezo.


Utegeshaji katika eneo hilo la mradi wa Nyanzaga umefanyika kwenye mazao aina ya alovera, katani, mibono, nanasi na migomba, miti mfano mikalibea na mikaratusi pamoja na utegeshaji wa nyumba mfano ujenzi wa nyumba mpya mahali palipokuwa nyumba ya zamani.

"Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza asingependa kuona migogoro katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa unaonufaisha watanzania" alisema Dkt Mabula.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Dkt Steven Kiruswa alisema, kuna fursa nyingi zitakazopatikana baada ya mradi mkubwa wa mgodi wa madini ya dhahabu wa Nyanzaga kuanzishwa.

"Fursa zitakazopatikana baada ya mgodi kuanza zitawasaidia wananchi wa kijiji cha Sota na nimpongeze muwekezaji ambaye kabla ya kuanza kazi ameanza kuisaidia jamii ya kijiji hicho hata kabla kuwekeza". alisema Kiruswa


Alimtaka muwekezaji kuandaa mpango kazi utakaonesha kila mwaka atachangia kiasi gani katika maendeleo ya eneo la mradi huku akibainisha moja ya faida watakayonufaika wananchi wanaoishi eneo la kuzunguka mgodi ni fursa ya ajira.


Moris Omoro mkazi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema ambaye ni mlemavu wa miguu alieleza kuwa bado hajapata uhakika wa ajira kwa watu wenye ulemavu na kuomba muwekezaji wa mgodi kufikiria namna ya kuwapatia ajira pale mgodi utakapofunguliwa.

Naye mkazi mwingine wa kata ya Igagula Rebecca Wajihi alieleza kuwa, wanachotegemea baada ya kuanzishwa mgodi anaamini wananchi wataondoka  kupisha mgodi na  kuachia maeneo na sasa wanachotegemea ni vijana kupata ajira ili waishi katika maisha mazuri.

Eneo la mgodi wa Nyanzaga wilayani Sengerema limegusa sehemu ya vijiji viwili vya Sota na Nyabila ambapo jumla ya vitongoji vitano kutoka katika vijiji hivyo vimeguswa ambavyo ni Kaningu B, Kadashi, Sota A, Nyanghona na Nyashimba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.