Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu Michezo Zanzibar Akifungua Kikao cha Kamati Tendaji ya Michezo ya Majeshi Tanzania.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Khamis Abdalla Said amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inathamini juhudi zinazofanywa na BAMMATA  katika kuhakikisha nchi inabakia salama na  kupata mafanikio katika Michezo.

Hayo ameyaeleza wakati akifungua kikao cha kamati Tendaji Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania huko katika ukumbi wa Makao Makuu ya KVZ  Mtoni Zanzibar.

Alisema Serikali zote mbili zinatambua umuhimu wa kuundwa chombo cha michezo ambacho tokea kuundwa kwake mwaka 1977 kimekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji vya wanamichezo na kuviendeleza hadi kufikia kuiwakilisha vyema nchi katika Mashindano ya kimataifa.

Aidha alisema wanamichezo wengi wa Tanzania ambao wamefanikiwa kuiletea sifa na kuitangaza vyema nchi kupitia michezo wametoka katika vyombo vya ulinzi na usalama na kuibuka katika mashindano ya BAMMATA amabyo kamati ndio inayosimamia.

‘’Serikali zote mbili zitaendelea kutoa ushirikiano kwa BAMMATA ili kuleta ufanisi na mafanikio mema  kwenye sekta ya Michezo” alisema

Aliwataja wachezaji ambao wametokea katika vyombo vya ulinzi na wamefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania akiwemo Filbert Bai,Juma Ikaangaa,Simbu,Suleiman kigunda.

Alisema sera ya michezo inaelekeza Wizara zinahusika na zinasimamia vyombo vya ulinzi na usalama kuandaa na kutekeleza mipango ya muda mfupi na  mrefu ya Maendeleo ya Michezo.

“Kuwepo kwenu hapa leo hii,munaisaidia Serikali kutekeleza sera ya Michezo ,Naamini kamati hii ndio inayojadili na kupitisha mikakati ya maendeleo ya Michezo katika vyombo vya ulinzi na Usalama” alisema.

Alipongeza klabu ya KMKM ya Zanzibar kwa kuchukua Ubingwa wa soka ligi kuu Zanzibar kwa msimu wa mwaka 2021 -22 pamoja na klabu ya Kipanga inayomilikiwa na Jeshi la wananchi wa Tanzania kuwa bingwa wa FA msimu wa mwaka 2021 /2022 ambapo klabu hizo zitaiwakilisha Zanzibar katika Mashindano ya Kimataifa.

Mwenyekiti wa BAMMATA ,Bregedia Jeneral Suleiman Bakar Gwaya alisema  kuundwa kwa Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania ili kuwafanya Majeshi na Askari kuwa pamoja na kushirikiana katika Majukumu na kufanya kazi kwa ufanisi huku wakizingatia Amani.

Alisema katika Shughuli hizo wamekuwa na michezo mbali mbali ikiwemo wavu,shabaha kuogelea ,wavu,mpira wa miguu ,kikapu ,netballa  mpira wa mikono ,riadha ,magongo lakini pia wana mpango wa kuongeza michezo mengine kutokana na maendeleo ya dunia.

Aidha alisema baraza lina mpango wa kufanya mashindano mwezi Septemba ili kusudi kuimarisha afya zao katika majukumu yao lakini pia  wakishirikiana na taasisi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.