Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza timu ya
taifa ya wanawake chini ya miaka 17 “Serengeti Girls”, kwa kufuzu kucheza
michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Oktoba mwaka huu huko nchini India.
Katika salamu hizo za pongezi, Rais Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa
na juhudi kubwa zilizochukuliwa na timu hiyo tokea yalipoanza mashidano hayo hadi
kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika huko nchini India.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara yake husika ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) itaendelea kuiunga mkono timu hiyo
katika kuhakikisha inaendelea kufanya vizuri kwa kupata ushindi zaidi katika
mashindano yajayo.
Alieleza kwamba hiyo ni faraja kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuweka historia ya timu ya vijana ya wanawake walio chini ya umri
wa miaka 17 “Serengeti Girls”, kufuzu kucheza michuano hiyo ya Dunia.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaendelea kulijengea sifa Taifa na
kuendelea kuitangaza Tanzania kimichezo na kiutalii duniani kote hasa
ikizingatiwa kwamba mashindano hayo yanaendelea kupata washabiki wengi zaidi na
kuendela kupendwa duniani.
“Naipongeza sana timu yetu ya “Serengeti Girls” kwa kuweza kufuzu
kucheza michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Oktoba mwaka huu huko nchini
India, tunaitakia kila la kheria na matarajio yetu kwamba itaendelea kufanya
vizuri katika mashindano hayo na sisi tutaendelea kuiunga mkono na kuiombea dua
timu yetu hii”, alisema Dk. Mwinyi.
Hivyo, timu hiyo ya Tanzania imeungana na Morocco na Nigeria
kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali
hizo za Dunia kati ya Oktoba 11-30 mwaka huu katika miji mitatu nchini India
zikiwa fainali za saba tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mnamo mwaka 2008.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizo kwa timu ya
soka ambapo mpaka timu hiyo ya “Serengeti Girls” inafuzu mashindano hayo
ilizing’oa Botswana, Burundi na kumalizia kwa kuitoa Cameroon baada ya kuibuka
na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya nchi hiyo.
Katika kuonesha ushirikiano kati ya ZFF na TFF kwa kupitia Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya Zanzibar timu hiyo ya “Serengeti
Girls” iliweza kufunga kambi yake hapa Zanzibar kwa takriban wiki mbili
ikijiandaa katika mashindano hayo pamoja na kucheza mchezo wa marudiano katika
uwanja wa Amaan Zanzibar kati yake na Cameroon ambao ulimaliza kwa kutoka sare
ya mabao 1-1 huku wa awali uliochezwa nchini Cameroon “Serengeti Gilrs” ilimaliza
kwa mabao 4-1.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,
Ikulu Zanzibar. OF
RESPONSIBILITY
No comments:
Post a Comment