Habari za Punde

SMZ Ikitayari Kuwakaribisha Wawekezaji wa Aina Zote Kuzingatia Manufaa Makubwa Yatakayoweza Kupatikana Katika Uwekezaji Wao.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akindoa pazia kuweka Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Mradi na Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Kisasa wa Michezo “Zanzibar International Criket Club and Sports Complex” Fumba Zanzibar , akiwa na Mwakilishi wa  Kampuni ya JHIL Enterprises kutoka India Bw. Sunil Manohar Gavaskar, wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika katika eneo la ujenzi wa mradi huo Fumba Wilaya ya Magharibi”B” Unguja leo 3-6-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa shehiya ya Fumba na Vijiji jirani kuishi vyema na Wawekezaji,  sambamba na kuachana na uvamizi wa maeneo ya ardhi yaliotengwa kwa ya shughuli za Uwekezaji.

Dk. Mwinyi amesema hayo huko Fumba, Wilaya Magharibi ‘B’ unguja, katika Uzinduzi na Uwekaji wa Jiwe la msingi la Mradi  wa Ujenzi wa  Uwanja wa mchezo wa Kriketi pamoja na michezo mingine.

Amesema  Serikali ina taarifa kuwa baadhi ya wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka maeneo hayo (ikiwemo Fumba, Bweleo, Nyamanzi, Dimani na maeneo mengineyo, wameanza kuvamiafanya maeneo hayo, huku wengine wakipanda miti kwa dhamira ya kupata fidia kubwa, pale maeneo hayo yatakapofanyiwa tathmin.

Dk. Mwinyi alisema Serikali iko tayari kuwakaribisha Wawekezaji wa aina zote kwa kuzingatia manufaa makubwa yatakayoweza kupatikana kutokana na  Uwekezaji utakaofanyika; ikiwemo kuibua vipaji kwa vijana na kuweza kucheza ndani na nje ya nchi pamoja na kupata soko la bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Kampuni ya JHIL Enterprises kutoka India; Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo  pamoja  Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale  kwa mashirikiano na Kampuni hiyo, huku akiipongeza kazi nzuri wanayofanya kuhakikisha mipango ya Serikali katika Uwekezaji inafanikiwa.

Dk. Mwinyi  alisema ujenzi wa kiwanja hicho utataoa fursa kwa timu mbali mbali kutoka nje kuja nchini, hivyo kutoa fursa kwa vijana wazalendo kujifunza.

Nae, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed aliipongeza Kampuni ya JHIL Enterprises kwa kushirikiana vyema na Serikali kuweka miundombinu bora ya michezo, ikiwemo kriketi.

Aidha, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema wastani wa vijana 1000 wanatarajiwa kupata ajira  kabla na baada ya ujenzi huo kukamilika, hivyo akatumia fursa hiyo  kuwataka Vijana kuacha kuchagua aina ya kazi.

Alisisitiza azma ya serikali ya kuchukua hatua mara moja dhidi ya mwekezaji huyo endapo atashindwa kutekeleza ipasavyo mradi huo ndani ya kipindi cha meizi sita kama mktaba ulivyoainisha.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatuma Hamad Rajab akisoma Risala juu ya uzinduzi huo na Uwekaji msingi wa Uwanja wa mchezo wa Kriketi pamoja na michezo mingine, alisema pamoja na mwekezaji huyo kujenga miundombinu hiyo, pia ameaahidi kuandaa matamasha mbali mbali ili wana michezo kutoka sehemu mbali mbali Duniani washiriki katika mashindano , hatua itakayokuza Utalii na kuimarisha michezo.

Alisema pamoja na ujenzi wa Uwanja huo wa kriketi Mwekezaji atajenga uwanja wa Mpira wa migu, tenis, mpira wa kikapu, mpira wa Pete, majengo ya biashara pamoja na sehemu za mapumziko, sambamba na kujenga Bwawa la kuogelea la kisasa lenye Viwango vya Olimpik.

Aidha, alieleza Kampuni hiyo itajenga ukumbi wa kisasa wa sanaa utakaokuwa na viti na vifaa vyote muhimu, kwa ajili ya kuwandaa vijana kuwa na stadi za kimataifa katika kutoa huduma za Utalii.

“Ujenzi wa uwanja huu wa Kimataifa ni moja kati ya juhudi na dhamira ya Serikali ya kuvutia Wawekezaji kuja kuwekeza nchini, hatua itakayoleta tija kubwa kwa Vijana wetu”, alisema.

Katibu Fatuma alisema hadi kufikia mwakani, Mwekezaji huyo anatakiwa awe amekamilisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Kriketi, pamoja na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu pamoja na Hoteli kwa ajili ya kulala wachezaji na wageni.

Katika hatua nyengine, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya JHIL Enterprises kutoka India Jilesh Himat Babla alisema ujenzi huo utaiwezseha Zanzibar kufunguka katika Ulimwengu wa michezo pamoja na kuleta ustawi katika sekta ya utalii, huku akiipongeza Serikali kwa kuwa na Dira na kuunga mkono ujio wa  mradi huo.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya  Uwekezaji Zanzibar (ZIPPA) Sharrif Ali Sharrif alisema Mradi huo utahusisha eneo la Hekta 20 kutoka Hekta 87.7 lililotengwa kwa ajili michezo, na kusisitiza azma ya Serikali ya kulirejesha  eneo hilo la Ardhi mikononi mwake endapo Mwekezaji atashindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.

Sharrrif alisema moja ya changamoto kubwa inayolikabili eneo hilo la Uwekezaji ni uvamizi unaofanywa na  wananchi kwa ajili ya shughuli za ujenzi. 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.