Habari za Punde

Jamani TUTAFIKA MBALI

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Mwaka 2012 nilifika DW Bonn Ujerumani katika jengo linalorusha matangazo ya Idhaa kadhaa ikiwamo ya Lugha ya Kiswahili ambapo idhaa hii ilianza kazi hizo tangu mwaka 1953.

Nilipofika hapo kwa kuwa ulikuwa msimu wa baridi kali ya Februari, mkuu wa idhaa ya Kiswahili ambaye alikuwa mjerumani alinipatia koti la baridi lenye nembo za Idhaa hii ambalo lilinisaidia mno kupambana na baridi kwa siku za mwanzo.

Nilitafutiwa sehemu yakuishi na maisha yakaanza, niliporudi ofisini siku iliyofuata nilipangiwa kufanya kazi katika chumba kimoja cha mwisho mkono wa kushoto katika ofisi za Idhaa hii. Hapo palikuwa na dawati lenye meza na viti kadhaa, simu ya mezani, runinga, kompyuta yenye mtandao muda wote na redio inayotumia satalite inayokamata matangazo ya redio zote za kimataifa.

Nilipokuwa nikilifungua dirisha jirani yangu kipindi kisichokuwa cha baridi upepo mwanana wa Mto Rhine ulinipuliza vizuri huku vyombo vinavofanya shughuli zake katika mto huo navyo niliviona kila uchao. Baada ya siku mbili nilibaini kuwa katika chumba cha ofisi hii sikuwepo mwenyewe bali walikuwapo watu wengine wawili. Nilijiuliza je ni kina nani? Sikupata jibu.

Asubuhi moja macho yangu yalikaribishwa na mama mmoja mrefu wa kadri, mweusi, anayependa kuchana nywele ambaye ni mchangamfu sana. Mama huyu ambaye alikuwa mkweli, muwazi sana, makarimu sana na anayeheshimu dini yake Uisilamu.

“Mwanangu Adeladius, mimi baba yangu alikuwa ni Mkomoro, zamani watu wengi wenye asili ya kwetu walikwenda Zanzibar kutafuta maisha na ndiyo maana nikazaliwa Zanzibar, lakini baada ya mapinduzi nikiwa binti mdogo nikarudi na wazazi wangu Komoro.”

Zanzibar nina ndugu zangu wengi wa upande wa mama na mara nyingi ninakwenda huko kuwasalimu huku watu wengi wakivutiwa mno na sauti yangu wanayoisikia redioni kwa miaka mingi, alisema . “Zanzibar sikuondoka mufilisi; kwanza niliondoka na ujuzi wa kuzungumza, kusoma, kusikia na kuandika Kiswahili na Kiarabu. Mapinduzi ya Zanzibar yaliyosababisha turudi Komoro yalinisaidia sana kujifunza Kingazija na Kifaransa.”

Uwezo wake huo wa kuzungunza lugha hizo nne ulimsaidia kupata kazi Redio ya RFI Kiswahili na baadaye DW Kiswahili alijifunza Kijerumani na hapo ndipo na mimi nilikutana naye.

Msomaji wangu kumbuka kuwa muda wote huo mama huyu anajifunza lugha nne za awali akiwa mtoto. Sijui msomaji wangu watoto wetu wa Kitanzania tunafikiria kuwafundisha lugha ngapi za Kimataifa? Je ni moja, mbili, tatu, nne au tunajipongeza tu na Kiswahili chetu?

Mtu kama huyu unachotakiwa kufanya baada ya kujua uwezo wake wa lugha ni kumpa ujuzi wa kazi unayotaka afanye kwa kumpa taaluma ya ujuzi huo, mathalani iwe ualimu, uanahabari, uuguzi, utabibu au uhandisi. Kazi hiyo ataifanya vizuri sana kwa kuweza kutoa huduma kwa watu wanazungumza lugha zote anazozifahamu.

Nikiwa DW Kiswahili kuna siku mama huyu akanipigia simu akiniambia mwanangu Adeladius kesho nakwenda mahakamani kuna kazi nakwenda kuifanya, kesho kutwa ntakuletea zawadi fulani, nikasema sawa mama ninaiongoja.

“Mwanangu Adeladius, hizi sosoje ni za nyama ya nguruwe, nilipewa zawadi na rafiki zangu nikaona nikuletee wewe kwa kuwa ni mkristo, si unakula nyama ya nguruwe? ” Aliporudi siku iliyofuata aliyasema haya. Nikajibu naam, nilipokea boksi hilo na kurudi nalo kwangu na kuanza kula taratibu. Msomaji wangu kumbuka tu kuwa haramu kwako bali halali kwa mwezako.

Akilini mwangu nikawa ninakumbuka huyu mama jana hakuja kazini alikwenda mahakamani kufanya nini? Nilimuuliza swali hilo.

“Huwa nakwenda kufanya ukarimani hasa hasa Kiswahili, Kifaransa, Kiarabu na Kijerumani.” Msomaji wangu angalia mama huyu anavyoweza kuwa msaada kwa taifa lingine.

Maisha ya Ulaya yanahitaji mno utunzaji fedha, nikiwa huko ikifika jumamosi nilikuwa ninapika chakula changu cha wiki nzima ninakiweka katika jokofu na siku za kazi ninakibeba na kula ofisini kidogo kukwepa gharama ya kula mkahawani. Mama huyu siku zingine alikuwa akiniambia,

“Mwanangu Adeladius, usibebe chakula, leo nimepika wali na kisamvu cha nazi kama mapishi ya nyumbani kwenu Tanzania, tutakula sote.” Siku hiyo kiporo changu kinabaki jokofuni.

Mama huyu ninayemzungumzia si mwingine bali ni Oummilkheiri Hamidou ambaye alikuwa akifanya kazi na DW Kiswahili kama mtangazaji kwa miaka mingi lakini sasa amestaafu.

Msomaji wangu kwa nini siku ya leo ninayakumbuka matukio haya ya mama huyu? Kubwa ni kwa kuwa UNESCO wamekipa Kiswahili siku yake ya kuadhimishwa duniani ya Julai Saba.

“Ooooo, Sikukuu ya Sabasaba, Ilianza Julai saba, Wakoloni kuwakaba, Nyerere na Karume, Walifanya kweli kiume.” Unalikumbuka shairi hili?

Je sisi Watanzania tumejipanga kuwakaba hao wanazungumza lugha ya Kiswahili na lugha zingine? Naomba msomaji wangu mtazameni kwa kina mama huyu ninayemsimulia anazungumza lugha tano za Kimataifa kwa umahiri wote. Mapinduzi ya Zanzibar alikuwa binti mdogo sana. Je sisi akina pangu pakavu tia mchuzi watoto wetu wa elimu ya msingi na sekondari tunawasomesha lugha ngapi?

Kwa sana nashauri Wizara ya Elimu ya Tanzania inapaswa kuandaa mihutasari ya kusomesha masomo ya lugha zingine za kimataifa tangu shule za msingi hadi sekondari kwa haraka mno .

Mathalani kuanzia darasa la tano ongezeni masomo ya lugha zingine kama Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu alafu kidato cha kwanza hadi cha sita masomo hayo ya lugha zingine yafundishwe kwa lazima na mnaweza kuondoa General Studies (GS).Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki wanatakiwa kusaidia kutambua mataifa ambayo walimu hao watapatikana ili waje kuifanya kazi hiyo kwa mikataba hata ya kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2023 hadi 2033, mpaka hapo tutakuwa na uwezo wa ndani wa kujifundisha wenyewe lugha hizo.

Mapendekezo haya makatibu wa wakuu wa wizara hizi mbili yapelekwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga na yeye ayapeleke kwa Rais Samia Suluhu Hassani hili utekelezaji uanze mara moja.

Ikifika mwaka 2033 Mtanzania ambaye amemaliza kidato cha nne tu kama anakuwa dereva wa lori/basi na hata mfanyakazi wa nyumbani anakuwa na uwezo wa kujaribu kuzungummza lugha hata nne za kimataifa kikiwamo Kiswahili chake.Tutapata fursa nyingi kwa kazi zote kama vile wauguzi, matabibu, wahandisi, walimu, mabaharia na wanahabari. Jamani kwa kufanya hivyo wananchi wetu watanufaika sana na Kiswahili na tutafika mbali.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.