Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kireno.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na  Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza lugha ya Kireno (CPLP) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar  leo  wakiongozwa na Mhe.Balozi  Sandro de Oliveira  (wa tatu kulia) kutoka  Nchini Angola.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akikabidhiwa zawadi ya Kitabu  kutoka kwa Balozi wa Brazil Mhe.Antonio Cesare, akiungana na Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza lugha ya Kireno (CPLP) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar  leo  kwa mazungumzo. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiwa  katika picha ya pamoja na  Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza lugha ya Kireno (CPLP) baada ya mazungumzo walipofika Ikulu Jijini Zanzibar  leo, Mhe.Balozi  Sandro de Oliveira(wa tatu kushoto) kutoka  Nchini Angola (kushoto) Balozi Mdogo wa Mozambiq anayefanyia Kazi Zanzibar Mhe.Agostino Abacar Trinta,Balozi wa Brazil Mhe.Antonio Cesare (wa pili kulia) na Balozi wa Heshima wa  Brazil hapa Zanzibar  Abdulsamad Abdulrahim

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la   Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewashauri Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza Lugha ya Kireno (CPLP) kutoa fursa ya masomo ya juu katika nchi hizo (scholarship) kwa Wazanzibar, ikiwa ni hatua ya kufanikisha azma ya kukuza  matumizi ya lugha hiyo.

Dk. Mwinyi ametoa ushauri huo Ikulu Zanzibar, alipokutana na Mabalozi wa Jumuiya ya Nchi zinazozungumza lugha ya Kireno (CPLP), wakiongozwa na Balozi wa Angola nchini Tanzania Sandro de Oliveira, ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia haja ya kukuza matumizi ya Lugha ya Kireno HAPA nchini.

Mabalozi wengine wa CPLP ni pamoja na Antonio Cesare wa Brazil, Konseli Mkuu wa Msumbuji Agostino Abakar Trinta pamoja na Mwakilishi    wa Heshima nchini Brazil Abduswamad Abdurahim.

Dk. Mwinyi alisema Serikali inaunga mkono  dhamira ya CPLP ya kutoa fursa kwa Wazanzibari kujifunza lugha ya Kireno na kubainisha umuhimu wa kuanzia programu hiyo katika ngazi za Vyuo Vikuu.

Alisema ili kufanikisha dhana hiyo ni vyema kwa Mataifa hayo yakatoa fursa za masomo (scholarship) kwa Wanafunzi wa vyuo Vikuu nchini, hatua itakayowawezesha wanafunzi hao kujifunza lugha hiyo kikamilifu katika mwaka wa mwanzo wa masomo yao.

Alisema utaratibu kama huo ndio unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani, ikiwemo Uturuki; China; Urusi na mengineo, ambapo wanafunzi kutoka nje ya nchi hujifunza lugha za mataifa hayo katika mwaka wa mwanzo wa masomo, kabla ya kuanza masomo ya fani husika.

Alieleza kuwa Zanzibar kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) inayo taasisi inayohusika na masuala ya lugha; ‘Taasisi ya  Kiswahili na Lugha za Kigeni’, na kusema ni kiungo muhiumu katika kufanikisha dhamira hiyo. 

Aidha, alisema kuwepo kwa filamu zilizoandaliwa kwa lugha ya Kireno na  kuwekewa maelezo ya lugha ya Kiswahili au kiingereza  chini yake na hatimae  kuonyeshwa katika matamasha mbali mbali hapa nchini, kama vile Tamasha la Nchi za Jahazi (ZIFF) itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza matumizi ya lugha hiyo.

Nao, Mabalozi hao walimueleza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi dhamira ya kuendeleza ushirikiano na Zanzibar kupitia ukuzaji wa matumizi ya Lugha ya Kireno.

Aidha, waliahidi kuendeleza ushirikiano na kufanya kazi pamoja na serikali ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.