Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Akizungumza na Kukabidhi Boti kwa Wavuvi wa Samaki na Wakulima wa Mwani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi baada ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Malindi Wilaya ya Mjini Unguja akiwa katika ziara yake kutembelea Miradi ya Maendeleo katika Wilaya hiyo leo 18-7-2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa soko la samaki liliopo Malindi na baadae aligawa boti za uvuvi pamoja na boti kwa ajili ya wakulima wa mwani pamoja na kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya madau.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ndoto za uchumi wa buluu zinaanza kutekelezeka na kuyataja mambo makubwa matano yanayoimarisha sekta hiyo yakiwemo zana, soko, uhifadhi wa samaki, bandari maalum za uvuvi pamoja na viwanda.

Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kutoa boti 577 kwa ajili wa wavuvi wa Zanzibar pamoja na hatua za kujenga masoko zaidi huku akieleza hatua za ujenzi wa kiwanda cha mwani huko Pemba na baadae kujengwa hapa Unguja.

Alisema kuwa Serikali imewakabidhi benki ya CRDB kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwa kutambua kwamba wana uzoefu mkubwa huku akieleza jinsi Serikali ilivyobeba riba katika mikopo ya fedha kwa wajasiriamali.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi katika eneo la maduka la Darajani Bazaar na kusisitiza kuwa mara baada ya kukamilika wka ujenzi huo watakaowekwa kufanya biashara ni wale waliokuwepo awali na baada ya hapo ndio watapewa wafanyabiashara wengine.

Alieleza kwamba Serikali tayari imeshawawekea mazingira mazuri wajasiriamali wakiwemo wafanyabiashara huku akitumia fursa hiyo kukipongeza chama cha CCM kwa kukubali kubadilisha eneo hilo na kuekeza.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.