Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi akaribisha wawekezaji kutoka Iran


 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                                26 Agost,2022

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inawahitaji Wawekezaji kutoka Jamuhuri ya Kiislamu ya  Iran, kuja nchini kwa ajili ya  kuwekeza katika sekta mbali mbali za Uchumi wa Buluu.

 

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipokutana na Ujumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo  Hossein Amir Abdollahian, ambapo pamoja na mambo mengine mkutano huo ulibainisha maeneo mbali mbali ambapo nchi hiyo inalenga kuisaidia Zanzibar.

 

Alisema Zanzibar ina sera nzuri za Uwekezaji, huku ikiwa na mahitaji makubwa ya kupata wawekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu ili kuimarisha uchumi wake.

 

Aidha, aliwataka wataalamu wa nchi hiyo kuja nchini kuangalia namna ya kuimarisha sekta za uvuvi pamoja na biashara.

 

DK. Mwinyi alilipongeza Taifa kwa mashirikiano ya kihitoria kati yake na Zanzibar pamoja na kusaidia juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, katika nyanja mbali mbali ikiwemo biashara, vyuo vya amali, kilimo, utibabu na madawa.

 

Alisema Zanzibar ina mahitaji makubwa ya nishati hya umeme, ambapo hivi sasa inapata huduma hizo kupitia Waya wa chini ya Bahari (marine Cable) kutoka Tanzania Bara, hivyo amepongeza azma ya Iran inayolenga kushirikiana na Zanzibar  kupitia sekta hiyo.

 

Aidha, Dk. Mwinyi alishukuru Iran kwa kuazimia kushirikiana na Zanzibar katika suala la upatikanaji wa fursa za masomo nje ya nchi (scholarship), na kusema ni jambo jema litakalowawezesha wanaafunzi wa Zanzibar kujifunza, hususan katika masomo ya Sayansi.

 

Rais Dk. Mwinyi aliiomba Iran kuleta watendaji wake ili kukaa pamoja na wenzao wa Zanzibar ili kuona kwa namna gani wataweza  kusaidia uimarishaji wa sekta za Viwanda ili kutoa fursa za ajira kwa vijana pamoja na kutaka wataalamu wa nchi hiyo kuja kuanzisha viwanda hivyo.

 

Ailipongeza juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Taifa hilo za kusaidia uimarishaji wa sekta ya kilimo kwa kuipatia Zanzibar zana na vifaa mbali mbali ikiwemo Matrekta pamoja na  ‘Power Tiller’ ili kuendeleza kilimo cha kisasa.

 

Aidha, alitoa shukrani kwa mualiko aliopewa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran Ebrahim Raissi wa kulitembelea Taifa hilo hapo baadae.   

 

Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir Abdollahian alibainisha maeneo mbali mbali ambapo Taifa hilo linalenga kushirikiana na Zanzibar, ikiwemo suala la kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Watu wa Jamii ya Shirazi walioko Iran na wale wa Zanzibar.

 

Alieleza kuwa Iran ina azma ya kuanzisha ushirikiano na Zanzibar katika suala la upatikanaji wa Nishati na kusema nchi hiyo ina uzoefu mkubwa katika suala la Nishati ya umeme, huku akatolea mfano wa mradi mkubwa  unaoendelea kutekelezwa na Taifa hilo nchini Iraq unaohusisha umeme wa Megawati 4000.

 

Hossein alisema  eneo jengine ambalo taifa hilo linalenga kushirikiana an Zanzibar ni la upatikanaji wa fursa za masomo nje ya nchi, ili kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kwenda nchini humo kujifunza katika nyanja mbali mbali za kitaalamu.

 

Aidha, alieleza  eneo jengine ambapo Irani inaweza kushirikiana na Zanzibar ni juu ya ujenzi wa miundombinu, ukihusisha ujenzi wa barabara, njia za reli pamoja na viwanja vya ndege.

                     

Kuhusiana na sekta ya Biashara, Waziri huyo alisema ni eneo  ambalo Taifa hilo liko tayari kushirikiana na Zanzibar, na kusema nchi hiyo inashika nafasi ya tano Duniani.

 

Katika hatua nyengine, Waziri Hossein alitoa mapendekezo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuitaka kuandaa Kamati ya Jumuiya ya Wafanya Biashara kwa lengo la kubainisha maeneo yanayopasa kushirikiana.

 

Aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo katika sekta za Utalii, uchumi wa Buluu, Afya, pamoja  na kuandaa majukwaa yatakayofanikisha kufanyika uchambuzi ili kubaini fursa za ushirkiano.

 

Aidha, alitoa pendekezo linalotoa nafasi ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Zanzibar pamoja na kutoa fursa ya kuwakutanisha na wenzao wa Iran kwa lengo la kupata uzoefu katika nyanja za  elimu ya juu pamoja na Sayansi.

 

Alisema Taifa hilo lina azma ya kuanzisha Chuo kikuu hapa nchini ili kutoa fursa kwa wanafunzi wazalendo kujifunza nyanja mbali mbali ambazo Serikali ina mahitaji makubwa, kama vile sekta ya mafuta na gesi asilia.

                                                                  

Pendekezo jengine ni la kubadilisha uzoefu katika shughuli za Mabunge hususan katika Dilomasia ya Uchumi”, alisema.

 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.