Habari za Punde

Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/23

 Dodoma                                                                              Tarehe: 9 Agosti 2022                                                                                                          

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wanahabari, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana nanyi siku hii ya leo tukiwa na afya njema. Ndugu zangu Waandishi wa Habari tumewaita hapa leo kwa ajili ya kueleza utekelezaji wa shughuli za Shirika la Nyumba la Taifa na Mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa mwaka 1962 kwa sheria Na.45 likiwa na jukumu la kuwezesha ujenzi wa nyumba na majengo mengine kwa matumizi mbalimbali hususan makazi, Ofisi na biashara.  Mwaka 1990 Shirika hili liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba(Rob) iliyoanzishwa mwaka 1971 kwa sheria Na. 13 ili kusimamia majumba yaliyotwaliwa na serikali. Ili kulifanya Shirika hili kujiendesha kibiashara mapitio ya sheria ya NHC ya mwaka 1990 na sheria ya ardhi Na.4 ya mwaka 1999 yalifanyika mwaka 2005 kupitia sheria Na. 2.

 Majukumu ya Shirika yanatekelezwa kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Shirika wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25) ambao unalenga kusukuma mbele ujenzi wa nyumba zipatazo 10,000 na kuwezesha ukuaji wa sekta ya nyumba kupitia ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Shirika la Nyumba lina mtaji(capital base) wa Shilingi trilioni 5.04 hivi sasa unaotokana na rasilimali ya majengo yake 2,650 yenye nyumba(Units) zipatazo 18,654 zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini.

MIRADI ILIYOTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2021/22 NI KAMA IFUATAVYO:-

(a)Ujenzi wa Nyumba

1.   Katika mwaka 2021/22, Shirika lilipanga kukamilisha Mradi wa Morocco Square Jijini Dar es Salaam. Napenda kuwataarifu kuwa hadi tarehe 30 Juni, 2022, utekelezaji wa Mradi huo umefikia asilimia 94.

- Ili kukamilisha mradi huu uliosimama tangu 2018 kwa kukosa fedha, Serikali imeruhusu Shirika kukopa fedha za kukamilisha mradi huu na miradi mingine ikiwemo Kawe 711. Mpaka sasa Shirika limekopa shilingi bilioni 44.7 kwa ajili hiyo. Mradi wa Morocco Square utakamilika Desemba 2022.

2.  Mradi wa ukandarasi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mwalimu Nyerere (Mara) Awamu ya IV umekamilika kwa asilimia 99 na Mradi wa ujenzi wa Soko la Kimataifa la Mifugo la Buzirayombo (Geita) umekamilika kwa asilimia 100 na tumeukabidhi.

(b) Uandaaji wa Mipango Kabambe

Mwaka 2021/22, Shirika lilitekeleza Mpango wa uandaaji wa Mipango Kabambe ya Uendelezaji wa maeneo ya Kwala (Pwani) na Mji wa Tanzanite wa Mirerani (Manyara). Aidha, uandaaji wa Mpangokina kwa ajili ya uendelezaji wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma ulifanyika na unaendelea.

(c) Ujenzi wa Viwanda vya Vifaa vya Ujenzi

Ili kutimiza azma ya kujenga nyumba za gharama nafuu nchini hususan kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini, hadi tarehe 30 Juni, 2022, Shirika limenunua maeneo kwa ajili ya uchimbaji mchanga na uzalishaji wa kokoto. Mpango wa Shirika ni kuhakikisha viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi kutosheleza miradi yake na baadae watanzania wengine unaanza kutekelezwa kwa siku zijazo.

(d) Ukarabati wa Nyumba

Ndugu Wanahabari, sambamba na ukusanyaji wa kodi ya nyumba, Shirika limeendelea kufanya ukarabati wa nyumba zake kupitia Mpango Maalum wa Ukarabati.  Katika mwaka 2021/22, Shirika llilitumia shilingi bilioni 3 kukarabati nyumba 180 katika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Katavi.

  MWELEKEO WA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023

- Ndugu Wanahabari, katika siku 100 za Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemiah Kyando Mchechu tangu alipoteuliwa mambo kadhaa yamefanyika ikiwemo kufanya mikutano ya mashauriano(engagements) na wadau muhimu wa sekta ya nyumba ili kupata uelewa wa pamoja wa sekta na uungwaji mkono. Kazi hiyo imeshakamilika kwa mafanikio makubwa.

Katika mwaka 2022/23, Shirika litatumia shilingi bilioni 413.7 kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:-

      i)          Kutekeleza Mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati chini ujulikanao Samia Housing Scheme (SHS). Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Rais na tunatamani watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo. Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar esSalaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30. Nyumba hizi zitaanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam (nyumba 500) na Medeli Jijini Dodoma (nyumba100). Mradi huu utakaotekelezwa kwa awamu utagharimu takriban Shilingi bilioni 466 sawa na dola za Kimarekani milioni 200.

    ii)          Kukamilisha  ujenzi wa Mradi wa Morocco square ambao ujenzi upo kwenye hatua ya uboreshaji wa mandhari (landscaping na ufungaji wa lifti na viyoyozi kazi ambazo kufikia mwezi Desemba 2022 zitakamilika. Aidha, sambamba na ujenzi huo, Shirika litaendelea na kukamilisha miradi ya Kawe 711 na Golden Premier Residence (GPR) iliyopo Kawe.

   iii)          Kuanza utekelezaji wa Sera ya Ubia itakayoruhusu Sekta Binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya Shirika. Sera hii ina lengo la kuharakisha uendelezaji wa maeneo yaliyo wazi katikati ya miji yetu kwa kujenga nyumba za vitega uchumi na hivyo kuliongezea Shirika na nchi mapato makubwa. Mpango huu unaounga mkono sera ya Mheshimiwa Rais ya kuvutia uwekezaji nchini, utazinduliwa Septemba 2022 na mtaarifiwa.

   iv)          Kuanzisha miradi mingine ya ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi;

    v)          Kuendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara nane (8) Jijini Dodoma,  ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ujenzi wa majengo matano (5) ya  Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la TANZANITE Mirerani, ujenzi  wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) na miradi mingine itakayojitokeza;

  vi)          Kuendelea kukusanya mapato na kodi ya pango ya nyumba za Shirika. Tunatoa wito kwa wapangaji na wadaiwa sugu wa kodi ya pango kuhakikisha wanalipa kodi na malimbikizo wanayodaiwa kwa kuwa Shirika kuanzia sasa linajiandaa kukusanya kodi hii kwa asilimia 100.

vii)          Kuendelea kutekeleza Mpango Maalum wa miaka mitano wa ukarabati wa nyumba za Shirika unaoishia mwaka 2027, kukarabati nyumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga, Mbeya, Mwanza, Singida na Kagera kwa gharama ya shilingi bilioni nane (8).

viii)          Kusaidiana na Wizara na wadau wa sekta ya Miliki nchini kubuni sera na sheria zitakazoifanya sekta ya miliki na nyumba kuchangia uchumi wa nchi yetu. Kazi hii tumeshaianza.

  ix)          Kuendelea na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi wa nyumba za NHC hususan kokoto na matofali;

    x)          Kununua ardhi ekari 400 katika maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na akiba ya ardhi;

  xi)          Tunaendelea kuhamasisha wananchi na wapangaji wetu kujitokeza Agosti 23, 2022 kuhesabiwa. Sensa ya watu na makazi ni kwa ajili ya kuleta maendeleo.

xii)          Kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya nyumba na Sekta ya Milki nchini. kupitia vyombo vya habari; vyombo vya habari ni mhimili muhimu wa upashanaji habari kwa Wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya Shirika.

 MANUFAA YA MIRADI YA UJENZI WA NYUMBA

1.   Kutoa ajira kwa watanzania- mradi wa SHS wa nyumba 5000 pekee unatarajiwa kutoa ajira zipatazo 26,400(direct 17,600 na indirect 8,800)

2.   Kukuza mapato ya serikali mfano mradi wa SHS 5000 unatarajiwa kutengeneza mapato ya kodi mbalimbali za serikali TZS bilioni 50 (mauzo ya nyumba) bilioni 10(  ununuzi vifaa vya ujenzi), PAYE TZS 17.8 bilion, Kodi ya majengo TZS milioni 55, corporate Tax kutoka  NHC na wajenzi wengine bilioni 77, VAT 60bilioni

3.   Kukuza sekta ya fedha kupitia mikopo ya nyumba watengenezaji, wauzaji na wakondarasi watakopa asilimia hadi 60 ambayo ni sawa na TZS 194.8 bilioni(SHS)

4.   Kukuza soko la sekta za huduma kama umeme, maji, gesi, simu, media (matangazo), ulinzi nk

5.   Kuongeza maisha bora kwa wananchi. Taarifa ya UN Habitat ya hali ya Idadi ya watu, inasema kuwa asilimia 50 ya watu waliishi mijini mwaka 2020 na ifikapo 2050 idadi ya watakaokuwa wakiishi mijini itafikia 70%. Tanzania itakuwa na watu135m na mwaka 2100 itakuwa na watu 286m na kuwa nchi ya 9 duniani. Hii inahitaji mipango madhubuti ya kupanga miji na upatikanaji wa nyumba.

6.   Tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 75

7.   Kukuza ukuaji wa Viwanda -  sementi, mbao, kokoto nondo marumaru mitambo(concrete mixers) vioo, samani, mabati, bomba na umeme

8.   Kuwa na mandhari nzuri na miji iliyopangwa- 70% ya miji yetu haijapangwa

9.   Kudumisha amani na utangamano-kupunguza uhalifu mijini, rejea Kibera, Nairobi 2012

 Ndugu zangu Wanahabari, niwashukuru sana kwa ushirikiano wenu mnaotupatia mara kwa mara. Nawaomba muendelee kutuunga mkono.

                            IMETOLEWA NA:

Muungano Kasibi Saguya

                        Meneja Habari na Uhusiano

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.