Habari za Punde

Wananchi wa Wilaya Kusini Unguja Wapongezwa kwa Muitikio Mkubwa wa Zoezi la Sensa.

Na.Mwandishi Wetu Wilaya ya Kusini Unguja. 

WANANCHI wa Wilaya ya Kusini Unguja wamepongezwa kwa muitikio wao mkubwa wa zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi pamoja na mashirikiano wanayoyatoa kwa Makarani wa zoezi hilo linaloendelea nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Rajab Yussuf Mkasaba aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipofanya ziara ya kuangalia harakati za zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi linavyoendelea katika Shehia mbali mbali za Wilaya hiyo.

Katika ziara yake hiyo Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kutoa shukurani kwa wananchi wa Wilaya hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kuwapa mashirikiano makubwa Makarani wa Sensa ya Watu na Makaazi hatua ambayo inawarahisihia kufanya shughuli zao hizo.

Alisema kuwa hatua hiyo inatoa faraja kwa Wilaya na Mkoa huo kwa kuona kwamba mafanikio makubwa zaidi yatapatikana pamoja na kufikia lengo lililokusudiwa kwani hatua hiyo ndio chachu ya maendeleo endelevu ambayo itasaidia kwa kiasikikubwa kujua idadi ya wakaazi wote nchini.

Mkasaba alitoa wito kwa wananchi wote ambao bado hawajapata fursa ya kuhesabiwa kuendelea kufanya subira kwani Makarani wa Wilaya hiyo watahakikisha wananchi wote wanapata haki yao hiyo ya msingi kwa kuhesabiwa popote pale walipo kama walivyoahidiwa na Serikali.

Nao Masheha wa Wilaya hiyo kwa nyakati tofauti walieleza jinsi zoezi hilo linavyoendelea kwa mafaniko makubwa sambamba na kuwepo kwa amani, usalama na utulivu mkubwa.

Makarani wa Sensa ya Watu na Makaazi wa Wilaya hiyo kwa upande wao walieleza jinsi zoezi hilo linavyokwenda vizuri pamoja na mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka kwa wananchi hali ambayo inawarahishia kwa kiasi kikubwa kufanikisha shuguuli zao hizo kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hayo, Makarani hao walieleza mafanikio waliyoyapata katika dodoso la Jamii kwenye Wilaya hiyo, zoezi ambalo lilifanyika Agosti 21 hadi 22 mwaka huu.

 Mwisho/ Agosti 26,2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.