Habari za Punde

Wawekezaji Wazawa Wahimizwa Kuwekeza Sekta ya Mifugo

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Mtangeki (kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) kuhusu mitambo iliyofungwa katika kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh namna itakavyofanya kazi alipotembelea kukagua maendeleo ya kiwanda hicho kipya kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Agosti 25, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila (kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) alipokutana na Waziri huyo ofisini kwake Mkoani Kagera Agosti 25, 2022. Waziri Ndaki alikuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku moja kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazohusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Na Mbaraka Kambona, Kagera

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza wawekeza kutoka Sekta binafsi nchini kuwekeza katika sekta ya mifugo kwa sababu kuna fursa kubwa ya kukuza mitaji yao na kupata faida.

Alitoa wito huo alipotembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Agosti 25, 2022. 

Waziri Ndaki aliwahimiza wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya mifugo nchini kwa sababu inawezekana  akitolea mfano muwekezaji huyo wa Kahama Fresh ambaye alianza uwekezaji katika shamba alilopewa na serikali na mpaka sasa amefungua kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo.

"Niseme tu kwamba sisi Wizara ya Mifugo tuko tayari kumuunga mkono mwekezaji yeyote atakayeweza kufanya uwekezaji mahiri kama alivyofanya Kahama Fresh ili  shughuli ya ufugaji iwe ya  kibiashara zaidi na kuleta tija kwao binafsi na Taifa kwa ujumla," alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa wawekezaji hao binafsi wakiwekeza katika sekta ya mifugo na kufanya ufugaji wa kibiashara watasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi lakini pia watakuza pato la taifa.

Aidha, alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji wao watasaidia Wafugaji wengine ambao wanafanya ufugaji wa kujikimu kujifunza kupitia kwao na kufanya ufugaji wenye tija kubwa zaidi.

Kwa upande wake Mwekezaji wa Kiwanda cha Kahama Fresh, Josam Mtangeki alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya maji na chakula cha mifugo hasa wakati wa kiangazi hivyo aliiomba Wizara kumuongezea eneo la lisilopungua hekta 2000 ili aweze kulima malisho kwa ajili ya mifugo yake na malisho mengine atawakopesha wafugaji wadogowadogo ambao wanamuuzia maziwa kwa ajili ya kuyachakata kiwandani hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.