Habari za Punde

Waziri Mhe.Nape Atoa Ufafanuzi wa Gharama za Bando

 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi za kimataifa, Tanzania inashika nafasi ya sita kwa Bara la Afrika kwa kuwa na gharama za chini za bando “vifurushi”  huku ikishika nafasi ya 32 Duniani kwa gharama ya chini ya data.

Waziri Nape ametoa ufafanuzi huo wakati aliposhiriki kipindi cha Power Breakfast on Saturday cha Clouds TV na redio, leo Agosti 20, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo amesema bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola 1.71 sawa na shilingi 3990.

“Tanzania kuwa miongoni mwa Mataifa yenye gharama za chini za mawasiliano haimaanishi kuwa itapunguza malalamiko kwa kuwa uchumi wetu haufanani na wananchi wengi wana kipato cha chini”, amesema Waziri huyo

Amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kufanya tathmini ya gharama za uwekezaji, utunzaji na usafirishaji wa data kila baada ya miaka minne na tathmini nyingine inafanyika mwaka huu ili kupata uhalisia wa gharama za bando kama zitapanda au kushuka.

“Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa Serikali yao ni sikivu na inafanyia kazi malalamiko na maoni ya wananchi, lakini pia nitoe rai kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya simu janja hasa kwenye kujiunga na huduma mbalimbali pamoja na program tumizi “applications” ili kupunguza matumizi ya bando”, Amesisitiza Waziri Nape

Aidha, Waziri Nape amesema kuwa Serikali imeruhusu ushindani kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwa na kampuni nyingi zinazotoa huduma za mawasiliano ambapo huduma ya vifurushi ni huduma ya ziada inayotolewa na makampuni hayo na kuleta unafuu wa gharama za mawasiliano.

Ameongeza kuwa kwa ulimwengu wa sasa wa kidijiti huduma nyingi zinapatikana kwa njia ya mtandao, hivyo kuifanya huduma ya intaneti kuwa huduma muhimu na ya msingi katika kuendesha shughuli za uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Katika hatua nyingine Waziri Nape ameielekeza TCRA, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC) na Makampuni ya simu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kujibu au kutoa ufafanuzi wa maswali na malalamiko ya wananchi

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.