Habari za Punde

DC TANGA AWATAKA MAOFISA BIASHARA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA


Na Oscar Assenga,TANGA

MKUU wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amewataka maofisa biashara kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini kujiepusha na vishawishi vya kuomba na kupokea rushwa katika utoaji wa huduma zao ili mafunzo waliyoyapata yaoneshe matokeo chanya kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mgandilwa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa biashara kutoka mikoa ya Arusha,Manyara,Kilimanjaro na Tanga yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) ambapo alisema badala yake wahakikishe wanatoa huduma saidizi kwa wananchi kwa waledi na uaminifu mkubwa.

Alisema kwamba wanaamini mafunzo hayo yatakuwa chachu kwao ya kuweza kusambaza elimu waliyoipata kwa wananchi ikiwemo nyenzo ya kupunguza kero mbalimbali na gharama za urasimishaji biashara suala ambalo mara kwa mara Serikali imekuwa ikilipigiwa kelele kwa nguvu zote.

Aidha alisema mpango huo wa mafunzo umezingatia umuhimu wa maafisa biashara kuwa karibu na wananchi kwa kutoa huduma bora saidizi na elimishi kwa wafanyabiashara ili kipato chao kikuwe na hatimaye Serikali ipate kodi na uchumi wa nchi uweze kukua na kuimarika.

" Kwa utafiti uliofanya kuhusu utendaji wa maafisa biashara umebainika kumekuwa na uelewa hafifu wa sheria ya leseni za biashara sura 208 na wengi kutumika kama wakusanyaji mapato hasa sehemu za biashara,vilabu na kwenye nyumba za kulala wageni badala ya kuwa wasaidizi washauri kwa wafanyabiashara na wawekezaji"Alisema DC Mgandilwa

Mkuu huyo wa wilaya aliwaambia kwamba ni matumaini yake kwamba kupitia mafunzo hayo yatawasaidia kubadili fikra na mitazamo yao na watendaji wa Serikali kuwa watoa huduma na msaada kwa wafanyabiashara na hivyo yawe chachu ya uwekezaji,ukuaji na uanzishwaji wa biashara.

Awali akizungumza Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Leseni BRELA Andrew Mkap alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha huduma zinazotolewa na maofisa hao zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi na hivyo kupunguza kero na usumbufu na gharama zisizokuwa na ulazima katika urasimishaji wa biashara nchini.

Alisema wao pamoja na mamlaka za Serikali wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria moja ambapo awali hawajawahi kufanya hivyo huku akieleza mafunzo hayo sasa yamewakutanisha ili kubadilishana uzoefu jambo ambalo litasaidia wao kufanya kazi kwa waledi huku wakizungatia sheria.

Hata hivyo alisema kupitia mafunzo hayo maafisa biashara wapatao 80 kutoka mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini na Halmashauri zao wamepatiwa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wa utendaji kazi kwa uelewa mkubwa.

Naye kwa upande wake Afisa Biashara kutoka ofisi ya Rais Tamisemi Linda Mabele alisema mafunzo hayo yatatakuwa na tija pale ambapo maaofisa hao watafuata sheria na utaratibu na kuhakikisha wanakuwa na mahusiano mazuri kwa wanachi na wafanyabiashara

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.