Habari za Punde

Zanzibar Kuazishwa kwa Kituo cha Kumbukumbu ya Maonesho ya Historia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa  ya Oman Dr. Hamed Mohd  Al Dhawiani (kulia kwa Rais)  alipofia Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 25-8-2022, akiwa na Balozi Mdogo wa Oman anayefanyia kazi zake Zanzibar Mhe. Said Salim Al-sinawi
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Oman kusaidia upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Dk. Mwinyi ametoa ombi hilo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman, Dk. Hamed Mohd Al-Dhawiani aliefika nchini kwa lengo la kuendeleza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo, hususan  katika suala la uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.   

Alisema kuna umuhimu kwa Taifa la Oman kusaidia upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar ili kuwajengea uwezo.

Alisema hatua hiyo itawawezesha watendaji hao kufanya kazi kwa weledi na ufanisi, hususan pale Zanzibar itakapofanikiwa kuwa na Kituo cha Maonyesho (exhibition centre).

Aidha, alisema Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Oman katika uimarishaji wa hifadhi za nyaraka na kumbukumbu ziliopo ili iweze kufikia kiwango cha kuwa na ‘Exhibition centre’ kama ilivyo kwa miji ya Lamu na Mombasa, nchini Kenya.

Alisema mafanikio hayo  yatasaidia uhifadhi bora wa Historia ya Zanzibar, hususan kwa watu wanaokuja kujifunza au kufanya tafiti mbali mbali.

Nae, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za kitaifa ya Oman Dk. Al- Dhawiani alisema katika kuendeleza ushirikiano na Zanzibar, Oman imetenga bajeti maalum kwa ajili ya kusadia uwekaji wa mazingira bora katika maeneo ya uhifadhi wa Nyaraka na Kumbukumbu ziliopo, huku akibainisha umuhimu wake katika kusaidia watu wenye mahitaji ya kufanya tafiti.

Alisema pia Oman inalenga kuendeleza programu ya kuwapatia mafunzo watendaji wa taasisi hiyo ili kuwa katika nafasi nzuri ya kiutendaji. 

Alieleza kuwa Oman ina uzoefu mkubwa katika suala la uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu, ambapo watendaji kutoka Mataifa mbali mbali Duniani yakiwemo ya Bara za Afrika wamekuwa wakifika nchini humo kwa ajili ya kujifunza.

Alisema Oman haina dhamira ya kuhodhi nyaraka ama kumbu kumbu ziliopo hapa nchini na kusema  kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia nyaraka zake.   

Dk. Al-Dhawiani alisema Oman na Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao kamwe hauwezi kuvunjika kwa vile unatokana na misingi ya dini, mila, lugha pamoja na watu wa pande mbili hizo kuchangiana damu pamoja na  kutembeleana.  

Mapema; Waziri wa Nchi (OR) Ikulu Jamal Kassim Ali  alizungumza na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za kitaifa ya Oman Dk. Al-Dhawiani na kusema kumbukumbu za Zanzibar ni sehemu muhimu ya urithi wa Dunia, zikiwa na umuhimu mkubwa kwa vizazi vijavyo.

Alieleza  kuwa mashirikiano yanayoendelea kati ya Oman na Zanzibar yatatoa fursa ya kuimarisha  uhifadhi bora  wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.   

Aidha, alisema ujio wa ujumbe huo kutoka Oman utakuwa wa manufaa makubwa katika majadiliano yatakayofanyika na Uongozi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar  na hatimae kuleta mustakbali mwema kwa mataifa hayo mawili.

Nae, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kitaifa ya Oman  Dk. Al-Dhawiani alisema nchi hiyo ina matarajio ya kufanya mambo mbali mbali ili kuimarisha uhifadhi wa nyaraka na kumbu kumbu za Taifa , kama ilivyofanyika nchini Kenya katika Miji ya Mombasa na Lamu.

Aliishauri Serikali kuhifadhi vyema nyaraka zote ziliiopo hapa nchini kupitia mfumo wa teknolojia ya kisasa ili ziweze kutumika bila ya kuwepo changamoto za aina yoyote na kusisitiza umuhimu wa Historia kubaki kama ilivyo.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.