Habari za Punde

Benki ya Dunia Yaipongeza Tanzania kwa Kusimamia Vizuri Uchumi Wake

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza jambo alipokutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (hayupo pichani), Jijini Washington D.C, nchini Marekani ambapo Benki hiyo imeimwagia sifa Tanzania kwa Usimamizi mzuri wa uchumi mpana wa nchi (Good Macro Economy Management)

Na Benny Mwaipaja, Washington, DC

MAKAMU Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miujiza na mageuzi makubwa kwenye uchumi.

Bi. Kwaka ametoa pongezi hizo Jijini Washington D.C nchini Marekani alipokutana kwa ajili ya kuagana na ujumbe wa Tanzania, ulioshiriki mikutano yam waka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Alisema kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa tulivu na umekua kwa kasi wakati nchi mbalimbali duniani zikihaha kujikwamua kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo msukosuko wa uchumi unaotokana na vita ya Urusi na Ukraine Pamoja na madhara ya UVIKO-19

Aliipongeza pia Tanzania kwa kuwa na sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye uchumi na kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei akieleza kuwa wakati nchi mbalimbali zikihangaika na janga la mfumuko wa bei wa tarakimu mbili, akitolea mfano wa nchi ya Ghana ambayo mfumuko wa bei umefikia asilimia 30, wakati Tanzania imeweza kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu moja tu ambayo ni asilimia 4.8.

Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia alisema kuwa mfumuko wa bei ni kama kodi mbaya inayowaumiza zaidi wananchi masikini na kwamba Benki yake itaitua Tanzania kama kielelezo na mfano wa kuigwa nan chi nyingine duniani.

“Kwenye nchi nyingi tueshuhudia akiba dhaifu ya fedha za kigeni, lakini ni tofauti kwa Tanzania ambapo mna akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje za kipindi cha takribani miezi mitano, hali kadhalika tumeshuhudia nakisi ya bajeti kwenye nchi nyingine lakini Tanzania nakisi yenu ni asilimia 3.5 pekee ya pato la Taifa. Jambo hili ni la kupongezwa” Alisema Bi. Kwakwa

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa pongezi hizo kwa usimamizi mzuri wa sera za uchumi na fedha na kuahidi kumfikishia pongezi hizo Mheshimiwa samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Dkt. Nchemba alirejea kutoa shukrani zake kwa Benki hiyo kwa msaada mkubwa wa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha, vinavyochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na hivyo kupunguza umasikini wa watu wake.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Tanzania na Benki ya Dunia. 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza jambo alipokutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (aliyeipa mgongo kamera, kushoto), Jijini Washington D.C, nchini Marekani ambapo Benki hiyo imeimwagia sifa Tanzania kwa Usimamizi mzuri wa uchumi mpana wa nchi (Good Management of Macro Economy).
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (katikati), akiwa katika picha ya Pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Salum Mkuya, Jijini Washington D.C nchini Marekani
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tatu kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Salum Mkuya (wa tatu kulia), pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania, Jijini Washington D.C nchini Marekani
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akiondoka katika Ofisi za Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Jijini Washington D.C, nchini Marekani baada ya kumaliza mazungumzo yao ambapo Makamu huyo wa Rais, aliimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi wa nchini. 
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (kushoto), akifurahia jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Salum Mkuya, Jijini Washington D.C nchini Marekani
(picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington D.C, Marekani)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.