Baadhi ya waandishi wa habari wakifuwatilia maelezo yanayotolewa na Mkurugenzi Mwanaisha Ali hayupo pichani waliyofika katika kikao kinachohusu matumizi ya nyumba kinyume na sheria za Shirika la nyumba hizo Zanzibar.
Picha na Miza Othman-Maelezo Zanzibar.
Na.Maelezo Zanzibar. 10.10.2022
Shirika la Nyumba Zanzibar limetoa onyo kwa wapangaji na watumiaji wa Nyumba za shirika hilo wanaovunja taratibu kwa makusudi na kuamua kuziuza, kuzikodisha au kuzifanya Madanguro nyumba hizo kinyume na taratibu.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Mwanaisha Ali Said ametoa onyo hilo wakati akizungumza na Wanahabari katika ofisi yao iliyopo Darajani mjini Zanzibar
Amesema kumejitokeza tabia na mazoea mabaya kwa baadhi ya wananchi kuzitumia vibaya nyumba za shirika kwa kuvunja taratibu kwa makusudi jambo ambalo halivumiliki.
Mkurugenzi Aisha amesema Shirika halitosita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekwenda kinyume na Mikataba ikiwemo kuichukua nyumba yake katika maeneo yote zilizopo nyumba za Shirika Unguja na Pemba.
Pamoja na kuichukua nyumba pia hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekwenda kinyume na sheria na utaratibu wa upangishwaji.
“Wapo wanaoziuza maarufu kama “kilemba” kuzikodisha, kuzikodisha, nyumba za kuishi kuzibadilishia matumizi na kuzifanya za biashara, kufanya danguro au kuvutiwa madawa ya kulevya, kuzifunga bila kuzitumia, na kupishana kiholela” alifafanua Mkurugenzi.
Amefahamisha kuwa maeneo ya Kikwajuni na Mji mkongwe ndio maeneo yaliyokithiri kwa watu kuvnja taratibu za shirika ikiwemo kuzigeuza nyumba za Shirika na kuzifanya Danguro na sehemu ya kuvutia madawa ya kulevya.
Shirika linatoa wito kwa wananchi wote kufuata sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kuzitunza, kulipa kodi kwa wakati kwani shirika halina nia ya kumdhalilisha wala kumnyanganya nyumba mwananchi yeyote anayefuata sheria na taratibu.
Mkurugenzi Aisha alisisitiza wapangaji wote kusoma mikataba yao ya upangishaji kwa umakini na kufuata taratibu zote zilizowekwa na shirika hilo.
Shirika la Nyumba Zanzibar ni Taasisi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoanzishwa kwa sheria namba 6/2014 ya Zanzibar likiwa na mamlaka pekee ta kuzisimamia nyumba zote za shirika.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment