Habari za Punde

Tanzania Yatwaa Tuzo katika Maonesho ya Utalii Nchini Korea Kusini ’THE 23RD BUSAN INTERNATIONAL TRAVEL FAIR’

Na.Mwandishi Maalum. 

Banda la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata tuzo ya kuwa Banda lenye Ubunifu wa Kipekee katika Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii nchini Korea Kusini yajulikanayo kama ‘Busan International Travel Fair (BITF)’ yaliyofanyika Jijini Busan kuanzia tarehe 13 - 16 Oktoba, 2022.

Katika Maonesho hayo ya kimataifa, na ya pili kwa ukubwa nchini Korea Kusini, wadau wa utalii kutoka katika nchi zaidi ya 30 walishiriki kutoka sehemu mbalimbali duniani.  Mwaka huu Tanzania ilikuwa nchi pekee kutoka barani Afrika kushiriki katika maonyesho hayo na kuweza kujinyakulia Tuzo hiyo.

 

Aidha, sambamba na Ubalozi wa Tanzania Seoul, Kampuni tatu (3) za utalii kutoka Tanzania Bara na Visiwani, zilishiriki katika maonyesho hayo. Kampuni hizo ni pamoja na: ZARA Tanzania Adventures, SAFANTA Tours & Travel, na CHOUM Tours & Safari.

 

Tuzo hii ni ya pili kwa mwaka huu 2022, ambapo awali mwezi Julai 2022 katika Maonyesho ya Utalii ya Seoul (Seoul International Travel Fair – SITF 2022), Banda la Tanzania lilitunukiwa tuzo ya “Best Marketing Award”. Katika Maonyesho hayo Ubalozi wa Tanzania Seoul, Bodi ya Utalii na wadau wengine walishiriki kikamilifu.

                                                  Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.