Habari za Punde

Wawekezaji Wamsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu kwa Mazingira Bora ya Uwekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge, akizungumza kwenye Kongamano la Wiki ya Uwekezaji na Biashara Pwani lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Uongozi Mwalimu Julius Nyerere Leadership School

Na.Khalfan Said - Pwani

WAWEKEZAJI Mkoani Pwani wamemsifu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yanayofanya chachu ya kuwekeza na kuzalisha na hatimaye kukuza mitaji ya biashara.

Wawekezaji hao kutoka makampuni ya nje na ndani ya nchi wamesema kati ya mambo mengi mazuri, wanafurahishwa sana na ushirikiano wanaopata kutoka Uongozi wa Mkoa wa Pwani ambao unawapa amani na kuona kuwa eneo walilochagua ni sehemu nzuri sana, rafiki na salama kwa kuwekeza mitaji yao.

Wakizungumza wakati wa Kongamano la Wiki ya Uwekezaji na Biashara Pwani lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Uongozi Mwalimu Julius Nyerere Leadership School Oktoba 8, 2022, Sino Tan industrial Park wamewaalika wawekezaji wengine kwenda kuwekeza mkoa wa Pwani kwani wao ni mashuhuda wa jinsi wanavyopata ushirikiano katika masuala mbalimbali yahusuyo uwekezaji hapa nchini.

“Pwani ni sehemu sahihi ya kuwekeza, tumeshuhudia wenyewe na nitoe wito kwa wawekezaji wengine kuja Pwani, ‘’Tumekuwa tukipatiwa ushirikiano mzuri sana kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na Taasisi zilizopo Mkoani hapa.” Amesema Mwenyekiti wa Sino Tan Industrial Park, Bw. Janson Huang.

Sino Tan industrial park wanaendelea na ujenzi wa kongani kubwa ya kisasa yenye eneo la viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo simu za mkononi, viwanda vya madawa (Pharmaceutical) na viwanda vya kuunganisha magari.

‘’Huko nyuma tulikwama kwa takriban miaka 8, tukaambiwa ni vigumu kuwekeza kiwanda cha sukari Bagamoyo, lakini kutokana na ushirikiano ambao tumepata na tunaoendelea kuupata kutoka Serikali Kuu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, mradi umeweza kutekelezwa kwa kipindi kifupi cha miaka minne tu na sasa tumeanza uzalishaji wa sukari.” Alisema Bw. Sufiani Ally, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Azam Group.

Amesema ukiacha viwanda vingine vya Sukari vilivyopo hapa nchini ambavyo vilijengwa miaka mingi iliyopita, Bagamoyo Sugar kinachomilikiwa na makampuni ya Bakhresa Group, wawekezaji kutoka hapa nchini, ndio kiwanda kipya kabisa kujengwa tangu Tanzania kupata Uhuru.

Naye mwakilishi wa King Lion Motor Cycle Limited, amesema kampuni hiyo ambayo inajihusisha na uwekezaji wa vyombo vya moto zikiwemo pikipiki pamoja na spea zake, inakusudia kuanzisha kiwanda cha kuzalisha Nondo, Bati na bidhaa zingine za ujenzi. Mwekezaji huyo amethibitisha kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kutoka kwenye uongozi wa Mkoa wa Pwani na Wilaya.

“Kwa ushirikiano wa Mkuu wa Mkoa pamoja na Watumishi wa Ardhi, tumeweza kupatiwa heka 75 na tunatarajia kujenga kiwanda kitakachokuwa kikubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.” Amesema.

Naye Mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Zachy Mbenna, amesema hivi sasa Mkoa wa Pwani ni ‘brand’ kubwa sana katika eneo la uwekezaji hapa nchini na akatoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zote zinazozalishwa au kuchakatwa Pwani kuhakikisha zinaandikwa na kutambulika kwa jina la Pwani.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge amehimiza ushirikiano baina ya Wizara na Ofisi za Mikoa ili kuharakisha utoaji huduma kwa wawekezaji. 

“Wawekezaji wanawekeza kwenye mikoa na eneo la kwanza ambalo mwekezaji anatarajia kupata ufumbuzi (solution) ya masuala mbalimbali ni ofisi ya mkoa, hivyo wizara zikiwa karibu na mikoa na kufahamu mipango yao, itasaidia sana kujenga uelewa wa pamoja kutoa huduma kwa wepesi lakini pia itawawezesha wawekezaji kuwa na matumaini na ofisi za mikoa. Amefafanua.

Mhe. Kunenge amesema katika mkoa wa Pwani wameweka utaratibu wa dirisha moja (One stop centre) la kuwahudumia wawekezaji ambapo kuna taasisi 19 zinazotoa huduma siku mbili kwa wiki, Jumanne na Alhamisi na kwamba licha ya changamoto za hapa na pale utaratibu huo umekuwa na manufaa katika kuwahudumia wawekezaji wanaofika mkoani Pwani. 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Bw. Sufiani Ally, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano Azam Group.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Ally Gugu (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe.Nickson Simon. 
Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Mhandisi Martin Temo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Khadija Nasir Ali.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge akimsikiliza Katibu Tawala Mkoa huo Bi. Zuwena Jiri.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Ahmed Abbas na washiriki wengine wakifuatilia kongamano hilo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Ally Gugu (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Prof. Marcellina Mvula Chijoriga.
Washiriki
Mhe. Alhaj Aboubakar Kunenge akizungumza na Mwenyekiti wa Sino Tan Industrial Park, Bw.Janson Huang.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Baadhi ya Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani na washiriki wengine wakifuatilia majadiliano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.